Friday, November 15

MATAMU HAYA HAPA RIPOTI YA ‘CAG’ MASHIRIKA YA UMMA ZANZIBAR

NA HAJI NASSOR, PEMBA.

MOJA ya mashirika ya serikali yaliotajwa kuongeza mapato yake, kupitia ripoti ya Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, ni Shirika la Umeme Zanzibar ‘ZECO’ lililongeza mapato yake, kutoka zaidi ya shilingi bilioni 33.579 mwaka 2019/2020, hadi kufikia zaidi ya shilingi bilioni 34.344 mwaka 2020/201.

Hayo yamebainika, kwenye ripoti hiyo ya mwaka 2020/2012, ambayo iliwasilishwa mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za serikali, Dk. Othman Abass Ali.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa, kwa upande wa ZECO kulikuwa na ongezeko la zaidi ya shilingi milioni 764.207 sawa na asilimia 2, huku kwa mwaka 2020/2021, shirika hilo limepata faida ya zaidi ya shilingi bilioni 16.171, ikilinganishwa na faida iliyopatikana mwaka 2019/2021, ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni 19.863 na upungufu ikiwa ni shilingi bilioni 3.692 sawa na asilimia 19.

Shirika jengine ambalo mapato yake yametajwa kuimarika ni kupitia ripoti hiyo, Shirika la Bima Zazibara ‘ZIC’ ambapo yameongezeka, kutoka zaidi ya shilingi bilioni 19.853 kwa mwaka ulioishia disemba 2019, hadi kufikia shilingi bilioni 20.020 kwa mwaka 2020.

Ripoti hiyo ikafafanua kuwa, ZIC kwa kipindi hicho, imepata faida ya shilingi bilioni 2.358 ikilinganishwa na faida iliyopatikana, kwa mwaka ulioishia 2019 ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni 2.939 kukiwa na upungufu wa shilingi milioni 580.078 sawa na asilimia 19.7.

Kwa upande wa Shirika la Bandari Zanzibar ‘ZPC’ mwaka fedha 2020/2021, limepata mapato ya shilingi bilioni 39.897 kutokana vyanzo vya mapato, ikilinganishwa na makusanyo ya zaidi ya shilingi billion 34.848 kwa mwaka 2019/2020 kukiwa na ongezeko la shilingi bilioni 5.048.

Aidha ripoti hiyo ya Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za serikali imeitaja Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar ‘ZSTC’ katika kipindi cha mwaka 2020/2021, limepata shilingi bilioni 11.217 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi bilioni 56.795 kwa mwaka 2019/2020, sawa na upungufu wa shilingi bilioni 45.577 sawa na asilimia 80.

Aidha shirika hilo linadai wakulima wa zao la karafuu shilingi milioni 7.005 kwa ajili ya mkopo wa zao hilo, ambapo ilikuwa kinyume na mkataba ya ukopeshaji uliofanyika.

Ambapo wa wilaya ya Chake chake ‘ZSTC’ wanawadai wakulima shilingi milioni 4,050,000, Wete shilingi 945,000, Micheweni shilingi 2010, 000 na wilaya ya Mkoani shilingi milioni 1.800 kuanzia mwaka 2011 hadi 2018.

Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar ZECO, tawi la Pemba Mohamed Juma Othman, amesema wamefarajika kuona kunaongezeko la mapato kwa shirika hilo.

Alisema, moja ya kichecheo cha kukuza mapato yao, ni kuondosha gharama za nguzo na kuwepo kwa mkopo wa huduma ya umeme kwa wananchi.

‘’Tunaendelea kujipanga ili kuhakikisha mapato ya ZECO yanaongezeka mara mbili, na vipo vijiji vyenye wastani wa nyumba 80 hadi 120 katika wilaya ya Micheweni na hata Mkoani hazijafikiwa na huduma yetu,’’alieleza.

Baadhi ya wananchi wakizungumza na mwandishi wa habari mjini Chake chake, wamesema kama mashirika yameongeza mapato, hakunabudi kuandaliwa mazingira zaidi ili kuimarisha kazi zao.

Hassan Omar Haji ambae ni mfanyabiashara wa chakula, alisema wakati umefika sasa kwa serikali, kuhakikisha hakuna shirika la serikali litakaloporomoka kimapato.

Nae Aisha Hilali Makame wa Mtambile, alisema kama mashirika yameongeza mapato, yake hakuna budi kuimarisha miradi na miundombinu ya jamii.

Kazija Himid Mohamed wa Mizingani alisema, anamatumaini makubwa na uongozi wa rais Dk. Mwinyi kuwa, kuongezeka huko kwa mapato, iwe chanzo za kuimarisha miundombinu.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alitaka wote waliotajwa kwenye ripoti hiyo kuchukuliwa hatua.
 Mwisho