NA HAJI NASSOR, PEMBA.
WAZAZI na walezi wanaoishi na watoto wenye ulemavu kisiwani Pemba, wametakiwa kuzidisha ulinzi zaidi kwa watoto wao, kwani wadhalilishaji wamekuwa wakiwatumia zaidi, kumalizia shida zao za kibinadamu, kutokana na mazingira yao.
Ushauri huo umetolewa na Afisa Mipango wilaya ya Chake chake Kassim Ali Omar, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, kufuatia kuwepo kwa wimbi kubwa la watu wenye ulemavu kudhalilishwa, wilayani humo.
Alisema, pamoja na shughuli za kila siku walizonazo wazazi na walezi za kutafuta maisha, lazima wajiwekee utaratibu wa kuwawekea ulinzi maalum, watu wenye ulemavu.
Alieleza kuwa, haiwezekani wazazi au walezi, wawatelekeze watoto wao majumbani, kwa muda mrefu, bila ya kuwepo mwangalizi maalum.
‘’Shughuli za kutafuta maisha ni nzito, lakini suala la kuwapa ulinzi watu wenye ulemavu, hutakiwa lifanywe mara dufu, maana sasa wadhalilishaji wamehamia kwao, wakijua hawawezi kujitetea mahakamani,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Afisa Mipango huyo Kassim Ali Omar, alivishauri vyombo vya ulinzi na usalama, kuyasaidia makundi ya watu wenye ulemavu, wanapofika katika tasisi hizo kutafuta haki.
Katibu wa kamati ya kupambana na udhalilishaji wilaya ya Chake chake Rashid Said Nassor, alisema kamati hiyo imekuwa karibu mno na makundi ya watu wenye ulemavu.
‘’Hata katika kamati yetu, yumo mjumbe kutoka Idara ya watu wenye ulemavu wilaya ya Chake chake, lengo ni kuona tunasaidianaje, ili kupunguza matendo hayo kwao,’’alieleza.
Kwa upande wake, Mratibu wa watu wenye ulemavu wilaya ya Chake chake Mwadini Juma Ali, alisema lazima jamii ishirikiane na familia, katika kuimarisha ulinzi wa watu wenye ulemavu.
‘’Kama jamii itaona jukumu la kuwalinda watu wenye ulemavu ni la familia na tasisi za watu wenye ulemavu pekee, kundi hilo linaweza kukosa haki zake mbali mbali,’’alieleza.
Mwakilishi kutoka kituo cha mkono kwa mkono Chake chake Nuru Ali Nassor, alisema kesi nyingi zinazowahusu watu wenye ulemavu, hazina mwisho mzuri.
Akizungumza hivi karibuni, Mratibu wa Jumuia kwa ajili ya watu wenye ulemavu Zanzibar ‘ZAPDD’ Pemba Khalfan Amour Mohamed, alisema makundi yote yanaathirika ingawa wanachama wao ni zaidi.
‘’Zipo kesi kadhaa zimekuwa zikifutwa au kutoendelezwa mahakamani na vituo vya Polisi, ambazo zinawahusu watu wenye ulemavu wa akili, lazima jamii ishirikiane,’’alifafanua.
Afisa mawasiliano wa TAMWA-Pemba Gasper Charles, alisema kama vyombo vya habari vitaweka mkazo wa kukemea matendo hayo, kundi la watu wenye ulemavu linaweza kubakia salama.
Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, ameendelea kuitaka jamii kuhakikisha hakuna sulhu ya aina yoyote kwenye matendo ya ukatili na udhalilishaji.
Mratibu wa Kituo cha Huduma za sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba Safia Saleh Sultan, alisema kama jamii itashirikiana hasa kwenye hatua ya kutoa ushahidi, kesi hizo kwa watu wenye ulemavu zinaweza kukoma.
Mjumbe wa kamati tendaji ya Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu Zanzibar ‘JUWAUZA’ Hidaya Mjaka Ali, alisema bado vyombo vya mahakama na jeshi la Polisi, havijakuwa rafiki na kundi la watu wenye ulemavu.
Mtoto Hadia Mjaka Mosi (17) wa Mwambwe mwenye ulemavu wa viungo, alishauri kuwa, lazima kuwe na adhabu ya ziada kwa washitakiwa watakobainika kuwadhalilisha.
Jumla ya matukio sita ya watu wenye ulemavu yametokezea ikiwa ni pamoja na kubakwa na kulawitiwa, ingawa tayari yameshafikishwa mahakamani.
Mwisho