Thursday, November 14

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Dk.Charlotte Hawkins, Ikulu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Dkt.Charlotte Hawkins, Daktari bingwa wa Upasuaji kutoka nchini Uingereza,alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika leo 29-9-2022, katika ukumbi wa Ikulu.(Picha na Ikulu)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Dkt.Charlotte Hawkins,Daktari bingwa wa Upasuaji kutoka nchini Uingereza, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 29-9-2022.(Picha na Ikulu)                                                                   

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema  Serikali itaendelea kuunga mono juhudi za wahisani katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazoikabili jamii.

Dk. Mwinyi ameeleza hayo alipozungumza na Dk. Charlotte Hawkins, aliefika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kusalimiana.

Alisema Zanzibar inahitaji wataalamu wengi zaidi kutoka nje kuja nchini na  kusaidiana na wataalamu wazalendo ili kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii kupitia sekta mbali mbali, ikiwemo za Afya na Elimu.

Alisema ujio wa Daktari Hawkins hapa nchini na kujikita katika kukabiliana na changamoto inayowakabili  watoto wanaozaliwa na hitilafu katika miguu  imewawezesha watoto wengi kunufaika na huduma zilizotolewa.

Alimpongeza Daktari huyo kwa kazi kubwa na nzuri aliyofanya katika kipindi chote akiwa nchini, na kubainisha azma ya Serikali  ya kuvutia wahisani na wataalamu   kwa kuzingatia kuwa haiwezi kuwafikia watoto wote  wenye mahitaji.

Alieleza kuwa pamoja na Daktari huyo kupitia changamoto mbali mbali katika utekelezaji wa shughuli zake, amechangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa maisha ya watoto. ambapo baadhi ya nyakati Serikali hulazimika kuwasafirisha nje kwa matibabu.

Dk. Mwinyi alimuomba Daktari huyo kuendelea na juhudi za kusaidia jamii katika kukabiliana na changamoto hiyo ,huku akiahidi Serikali itahakikisha inampa kila aina ya ushirikiano kufanikisha malengo yake.

Nae, Dk. Charlotte Hawkins, Daktari bingwa wa Upasuaji kutoka nchini Uingereza, pamoja na mambo mengine aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya zanzibar kwa mabadiliko makubwa yanayofanyika katika kuimarisha  sekta ya Afya hapa nchini.

Alitumia fursa ahiyo kupongeza mashirikiano makubwa aliyopata kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zazibar kupitia Wizara ya Afya pamoja na watendaji wa Wizara hiyo, hatua iliomuwezesha kufanikisha vyema majukumu yake.

Mapema, Waziri wa Afya Ahmeid Nassor Mazrui alisema Dk. Charlotte Hawkins amekuwa nchini kwa kipindi cha miaka 13 sasa, akisaidia juhudi za Serikali katika kukabiliana na changamoto zinazowakbili  watoto wachanga wanaozaliwa wakiwa na  miguu yenye hitilafu.

Alisema katika kipindi hicho amefanya kazi kubwa na nzuri ya kutoa huduma katika Hospitali ya Abdalla Mzee Kisiwani Pemba kwa kuboresha  miguu bandia pamoja na kutengeneza viatu vya ngozi, ikiwa ni hatua ya kwanza ya kuondoa hitilafu ya miguu kwa watoto.

Alisema pia amesaidia kwa kiasi kikubwa kujenga uwezo na  kurekebisha miundo mbinu katika skuli mbali mbali ambapo watoto wenye hitilafu ya miguu wanasoma.

Waziri Mazrui alimpongeza Daktari huyo kwa kubeba dhima ya kuwashajiisha wahisani kutoka nje kutoa michango yao ya hali na mali pamoja na  wataalamu wengine kuja nchini kusaidia upatikanaji wa huduma za afya.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.