Monday, November 25

MWALIMU SKULI YA MADUNGU ANAYEDAIWA KUMBAKA MWANAFUNZI WAKE AREJESHWA RUMANDE

NA HAJI NASSOR, PEMBA.

MWALIMU wa skuli ya Madungu msingi Ali Makame Khatib miaka 25, anayetuhumiwa kumbaka mwanafunzi wake, amerejeshwa tena rumande na mahakama maalum ya makosa ya udhalilishaji, baada ya upande wa mashtaka kutopokea shahidi mpelelezi.

Baada ya kufika mahakamani hapo akitokea rumande, Mwendesha mashataka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Ali Amour Makame, alidai kuwa, shauri hilo lipo hatua ya kusikiliza ushahidi.

Alidai kuwa, walitarajia kumpokea shahidi ambaye ni Askari mpelelezi, ingawa hakutokeza mahakamani hapo, na wala upande wao, hawana taarifa za dharura yake.

‘’Ni kweli mheshimiwa hakimu, shauri hili la mwalimu wa skuli ya Madungu, tulitarajia kumsikiliza shahidi wetu wa mwisho ambae ni askari mpelelezi, ingawa hakufika mahakamani hapa,’’alidai.

Hivyo wakili huyo, aliiomba mahkama hiyo, kuliahirisha shauri hilo na kulipangia siku nyingine, ili kuendelea na utaratibu mwengine mahkamani hapo.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu wa mahkama hiyo maalum ya makosa ya udhalilishaji, Muumini Ali Juma, alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka, na kuliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 11, mwaka huu.

‘’Wakili wa upande wa utetezi una hoja yoyote, baada ya maelezo ya wakili wa upande wa mashataka, na kama huna basi mtuhumiwa arudi tena rumande, hadi siku hiyo na shahidi aliyebakia aitwe,’’alisema Hakimu.

Wakili wa upande wa utetezi Suleiman Omar, alikubaliana na ushauri wa upande wa mashataka, na kuiomba mahakama hiyo kulipanga shauri hilo tarehe fupi.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mtuhumiwa huyo Ali Makame Khatib, mkaazi wa Matuleni wilaya ya Chake chake, alidaiwa kumbaka mtoto wa miaka 11.

Aambapo kufanya hivyo ni kinyume na kifungu 108 (1), (2) (e) na kifungu cha 109 (1) cha sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.

Tuhma ya pili alilitenda August 12, mwaka huu majira ya saa 11:30 akiwa skuli ya Msingi Madungu wilaya ya Chake chake, ambapo alidaiwa kumbaka mtoto huyo.

                Mwisho