Monday, November 25

Mabadiliko ya tabianchi yawapeleka wakulima wa mwani kina kirefu cha maji

Mabadiliko tabianchi yawapeleka wanawake kulima mwani kina kirefu.

Licha changamoto zinazowakubwa, Wapo walionufaika kwa kujenga nyumba.

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

UHIFADHI wa mazingira ni muhimu, na linamgusa kila mtu kwa nafasi yake na sehemu yake alipo.

Siku za hivi karibuni uharibifu wa mazingira umekua mkubwa, katika maeneo mbali mbali ya Tanzania hata visiwani.

Uharibifu huo umepelekea kutokea ukame wa muda mrefu, miongo ya mvua kubadilika, baadhi ya mazao kulimwa maeneo ya mbali, ikiwemo kilimo cha mwani.

Sensa ya wakulima wa mwani, iliyofanywa na Idara ya mazao ya baharini Pemba 2011 hadi 2014, ina Jumala ya wakulima 15,010 wanawake wakiwa 11,049 na wanaume 3,961.

Wilaya ya Wete inawakulima 888, wanawake 778 na wanaume 110, wakati Wilaya ya Mkoani ni 2,531 wanawake 1,622 na wanaume 909, huku wilaya ya Micheweni ikiwa na wakulima 11,591 wanawake 8,649 na 2,942, ikiongoza kwa 75%.

Kilimo hicho kimekua kikilimwa kina kikubwa cha maji, tafauti na miaka iliyopita kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri dunia.

                WAKULIMA WA MWANI WANASEMAJE

Fatma Hamad Omar mkaazi wa Kinowe Tumbe, anasema kwa sasa wameamua kwenda kulima maji makubwa, ili kukumbia athari za mabadiliko ya tabianchi, ambayo yamekua yakiathiri kilimo hicho.

Anasema maji madogo mwani haukubali na msimu (bamvua) unaweza usipate kitu, mwani wote ukaharibika zaidi ya kupoteza muda na kurudi na machofu.

“Mwani mwingi unaharibika kwa kukatikakatika mwengine unaoza kabisa, maji madogo joto linakua kali yote haya yanatokana na mabadiliko ya tabianchi,”amesema.

WAANDISHI wa Habari kutoka chama cha waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET), wakizungumza na Fatma Hamad Omar ambae ni mkulima wa mwani katika shamba la Tangini Tumbe, kujua kwa nini wamelazimika kulima maji marefu kilimo hicho, ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa tuhifadhi maliasili Tanzania unaofadhiliwa na USAID.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)

Maryam Said Sharif mkaazi wa Tumbe magharibi, anasema wamelazimika kulima maji makubwa kutokana na maji madogo mwani unakuwa mchafu, kuanatope na majani na mwani kuharibika.

Hali hiyo imekua katika miaka hii minne, mwanzo hakuweza kuamini mpaka hali ilipokua kubwa, ndipo wataalamu kutoka serikalini kuanza kuwawahamasisha kuhamia maji marefu.

“Hakuna uchafu wala tope au takataka, mwani unakuwa safi tumeepukana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika maji madogo,”amesema.

Khadija Jafar Said mkaazi wa Tumbe mashariki, anasema vipindi vitatu amelima maji madogo hakuweza kupata hata wa mbegu, kutokana na kuungua kwa joto, kuharibiwa na majani.

Kombo Subira Kombo, amefahamisha kwamba wakulima wengi wamelazimika kulima maji marefu, licha ya kukosa vyombo vya kuwafikisha huko.

“Maji madogo unaweza kufika miezi 6 hujavuna, wakati mwengine kuingia majini, tafauti na maji makubwa ukivuna na kuweka katika chombo kupeleka kuanika,”amesema

HATUA GANI WAMEZICHUKUWA KUKABILIANA NA HALI HIYO

Nyezume Haji Nyezume, amesema waliwasiliana na wataalamu wa Idara uvuvi na kupatia elimu juu ya kulima kina kirefu cha maji.

“Pamoja na elimu ya kulima mwani kwenye kina kirefu, lakini pia wameshatufundisha namna ya uogoleaji pale tunapotwa na dharura baharini,”ameeleza.

Kwa sasa wakulima wengi wameelimikana wanalima kina kirefu, kama sio hizo athari za mabadiliko ya Tabianchi wangeendelea kulima maji kidogo.

“Mimi napelekwa na watoto wangu kwenye kilimo cha mwani kina kirefu, na nikimaliza wananirudisha nyumbani,”amesema Nyezume Haji.

Fatma Omar Kombo amesema baada ya athari hizo kujitokeza, serikali iliwataka kulima kina kirefu cha maji na kupatiwa mafunzo yakuogolea na mbinu za kujiokoa.

“Taasisi mbali mbali zimeweza kutupatia mafunzo ya kuogolea ikiwemo Milele Zanzibar Foundation, RIPOA, kwa kiasi fulani tunaweza kujipapatua,”amesema.

MAFANIKIO GANI WAMEYAPATA KUPITIA KILIMO HICHO

Mariyam Othman Kombo mkaazi wa Chimba, amesema licha ya kilimo hicho kuwa na bei ndogo, tayari ameshatia huduma ya umeme nyumbani mwake, kusomesha watoto skuli na kupata fedha za kikundi cha kuweka na kukopa.

“Kazi tunayofanya ni kubwa kipato chetu kidogo, serikali iongeza bei ya mwani kutoka shilingi 600 ya sasa hadi kufikia 2,000 kwa kilo moja cha mwani mkavu ili kupunguza athari ya machofu kilimo hicho, athari za mabadiliko ya tabianchi yametuathiri na tunalima maji makubwa,”ameongeza.

Asha Mohamed Omar anasema licha ya mabadiliko ya Tabianchi kuathiri kilimo hicho, mwani umeweza kuboresha maisha yake.

“Tayari nimeshajenga nyumba yangu ya makaazi, nasomesha watoto wangu na kwa sasa nasomesha watoto wangu wawili ngazi ya chuo ambapo fedha za ada na matumizi mengine yanatokana na kilimo cha mwani,”amesema.

Faudhia Ali Hamad amesema mwani umemnufaisha ikiwa ni pamoja na kununua charahani, mifugo hata vyombo vya baharini.

“Mimi ninacharahani tatu na zote zinatumiwa na watoto wangu, kwa kushonea nguo mbali mbali na sihaba wanapata kiasi fulani cha fedha,”amesema

CHANGAMOTO GANI ZINAWAKABILIA KULIMA MAJI MAREFU

Fatma Hamad Omar (55) anasema kutokujuwa kuogolewa ni tatizo kwao na wanakolima ni mbali, hawana vifaa vya zarura vya kuokoa maisha kama vile ‘life jacket’ na viatu.

“Tunahitaji hata vyombo vya kufikia maji makubwa, tulivyonavyo havina hata mashine tupewe vya kisasa, ila bado mafunzo zaidi ya kuogelea yanahitajika kwa baadhi yetu,”amesema.

Mkulima wa mwani Kombo Subira Kombo amesema tayari ilishatokea chombo kuzama baada ya kupigwa na upepo, mvua kubwa na vyombo sio rafiki kwao.

Amesema Changamoto bei ndogo ya mwani, kilo shilingi 600 au 800, ingepanda kufikia angalau 1500 hadi 2000 kidogo na kupata unafuu.

ASASI ZA KIRAIA ZINASEMAJE JUU

Mkurugenzi taasisi ya ‘HUDEFO’ Tanzania Sarah Pima, anasema kila mtu ana paswa kuchukua juhudi kuhakikisha mazingira yanalindwa na bioanuai kwa kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Anasema kwa sasa athari hizo zimekua zikiathiri hata wavuvi, kilimo cha mwani kupandwa sehemu za mbali tafauti na maji madogo.

“Sasa maji madogo yamekua na joto kali, hakuna kinachoweza kupatikana kwa wakulima, tujitahidi kupanda miti na kupunguza uchafuzi wa hewa angani,”amesema.

Naye Mwakilishi kutoka taasisi ya ‘Elico Foundation Tanzania’ Sisty Basil, anasema ni wakati sasa taasisi za serikali na binafsi kuanza kushirikiana, katika suala la uhifadhi wa mazingira kwa kuhakikisha, wanapunza matumizi ya vitu vinavyochafua hewa.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET) Dk.Elen Outaru, amesema JET imekua mstari wa mbele katika kushajihisha wananchi kutunza, kuhifadhi na kulinda mazingira.

Amesema kwa sasa wanatekeleza mradi wamiaka mitano, “Tuhifadhi Maliasili Tanzania”, miti imekua ikipungua hewa chafu zinaongezeka, yote ni kutokana na vyombo tunavyoagiza viwango vyake vimeshapungua,”amasema.

Ali Rashid kutoka Milele Zanzibar Foundation, anasema mwani unaolimwa maji madogo unakua chini ya sentimita 20 maji yakitoka, joto la maji linakua kubwa na mwani huathirika, wadudu kuzaliana zaidi na kuushambulia mwani.

“Maji hata yanapojaa mwani unakuwa tayari umeshaharibika kwa jua kali pale maji yapotoka, hii imepelekea wakulima kuchukua muda wa miezi sita kua na mavuno hafifu,”amesema.

Amesema faida ya kulima maji makubwa mwani, joto lake halibadiliki kwa haraka wala haushambuliwi sana na wadudu kama ilivyo maji madogo.

              IDARA YA MAENDELEO YA UVUVI INASEMAJE

Afisa mkuu wa Mwani Pemba, kutoka Idara ya maendeleo ya Uvuvi Pemba Asha Khamis Sultani, amesema serikali kupitia shirika la ZSTC inanuanua mwani aina ya “Cottonii” kwa kilo moja shilingi 1,800 na mwani aina ya “Spinosum” shilingi 700 kwa kilo moja.

Amesema Idara itaendelea kutoka mafunzo kwa wakulima wa mwani katika kulima kina kirefu, pamoja na kutoa vifaa vya kufikia huko.

amesema micheweni ndio inayozalisha mwani asilimia 50% hadi 75% kwa Pemba, wakulima wengi na wanashiriki katika kuhifadhi mazingira kwa kuachana na matumizi ya chupa.

“Unapolima mwani maji madogo ya kitoka mwani unapata jua, maji yakirudi mwani unakua unaathirika, kina kikubwa wakulima wengi wameelekeza huko,”amesema.

Anasema wanawake wamekwamuka kimaisha kupitia kilimo cha mwani, kutokana na mipango na kuacha kutengemea waume zao, wapo wanaomiliki nyumba na kutia umeme, vyarahani na vikundi vya ushirika.

Naye mkuu wa Idara ya Hifadhi ya Bahari ya Mkondo wa Pemba (PECCA) Omar Juma Suleiman, amesema lengo lao ni kuhifadhi rasilimali ambazo zinapungua kwa ajili ya vizazi vinavyokuja, kutokana na mabadiliko ya Tabianchi.

Rasilimali hizo ni Samaki, matumbawe, miti ya mikandaa (mikoko) na kilimo cha mwani, hali inayotishia bahari kutokuwa na maufaa ya kutosha.

Mabadiliko ya tabianchi yamekua ni changamoto kubwa kwa wakulima wa mwani, hali iliyopelekea wakulima kulima kina kikubwa cha maji, kwani kina kidogo imekua ni changamoto kwao.

Kilimo cha mwani kimethirika na joto katika miaka ya hivi karibuni, wakulima wanalima maji madogo na joto kuwa kali kupitia kiasi, sasa wakulima wanapanda kina kirefu na mwani unakua mzuri.

KAMPUNI YA UNUNIZI WA MWANI ZINAMCHANGO GANI

Msimamizi wa mashamba ya Mwani kituo cha Tumbe, kutoka kampuni ya Sea Wed Cooperation LTd Bosco Huruma Kimambo, amesema suala la bei bado ni changamoto kubwa kwa wakulima, kwani walaji wakuba wa zao hilo liko nje ya Tanzania.

Amesema siku bei ikipanda mkulima atapata mavuno mengi, suala la bei ni kero ya muda mrefu, kwani wapo watu wananunua mwani kilo shilingi 700 lakini hamsaidii mkulima kitu chochote.

Amesema kwa sasa bado wako katika mikakati ya kuhakikisha wanaongeza bei ya zao hilo, ili wakulima nao waweze kunufaika kwani wapo wanaopendekeza 1000 na wengine wanataka 1500.

VIONGOZI WA SERIKALI WANASEMAJE WAO

Afisa misitu mkuu na kiungo wa Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania DK.Freddy Manyika, anasema mabadiliko ya Tabianchi yameathiri mambo mengi, ikiwemo sekta ya uhifadhi, upatikanaji wa nishati, ukame katika vyanzo vya maji na bionuai za baharini.

Amesema joto la bahari limepanda, baadhi ya viumbe baharini vimeanza kupotea, wakulima wa mwani na wavuvi wa samaki wameanza kwenda maji makubwa kufanya shuhuli zao kufuatia atharini za mabadiliko ya tabianchi.

Afisa Mdhamini Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Pemba Dk.Salum Mohamed Hamza, amesema serikali imeamua kuongeza thamani zao la mwani, ikiwemo kupanda kwa bei ya shilingi 1,800 mwani aina ya “Cottoni) na shilingi 700 mwani aina ya “Spinosum” tafauti na miaka iliyopita.

Amesema tayari serikali imeshawapatia boti 337 wakulima wa mwani Wilaya ya Micheweni, imezingatia kuwa Wilaya inachukua asilimia 80 ya kilimo hicho kwa unguja na Pemba.

“Tumewapa boti hizi zikiwa na mashine zake, ili kuweza kufikia maji makubwa katika shughuli zao za kilimo cha mwani, kwani sasa mwani unalimwa kina kirefu ili kuhimili mabadiliko ya tabianchi,”amesema.

Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali imepanga kutoa boti 500 kwa Zanzibar kwajili ya kusafirishia zao la mwani, ili kuwapunguzia mzigo wanapokwenda na kurudi katika shuhuli zao.

Amesema kwa sasa wakulima wanalima kina kikubwa cha maji kutokana na kina kidogo kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, ambapo kina hicho unakua maradufu zaidi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, akimkabidhi vifaa vya kulimia mwani mmoja ya wakulima wa Mwani Tumbe, wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo kwa Wilaya ya Micheweni.(PICHA NA ABDI SULEIMAN,PEMBA)

BAJETI YA WIZARA YA UCHUMI WA BULUU INASEMAJENA 2022/2023

Kwamujibu wa bajeti ya wizara ya uchumi wa buluu na uvuvi kwa mwaka 2022/2023, iliyowasilishwa baraza la wawakilishi waziri wa wizara hiyo Suleiman Massoud Makame, amesema usafirishaji wa mwani nje ya nchi umeongezeka kutoka tani 11,383 mwaka 2020 hadi tani 12,124 mwaka 2021.

Amesema kuendeleza kilimo cha mwani na kuongeza uzalishaji kutoka tani 9,000 hadi zaidi ya 12,000 kwa kuwapatia wakulima mafunzo bora ya uzalishaji wa mwani na kuwapa nyenzo zitakazosaidia kufanya usarifu wa mwani.

Aidha amesema vikundi 150 vya wakulima wa mwani Unguja na Pemba vimepatiwa mafunzo kuhusu njia bora za kisasa za upandaji mwani yenye uwezo wa kuongeza uzalishaji wa mwani mara tatu hadi nne.

NINI KIFANYIKE

Fatma Hamad Omar (55) amesema serikali kuwapatia vyombo madhubuti kwa wingi vitakavyoweza kuwafikisha kina kirefu cha maji, ili waweze kuendelea na shughuli zao za ukulima wa mwani.

Afisa misitu mkuu na kiungo wa Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania Dr.Freddy Manyika, amesema ni wakati sasa Tanzania kuanza kutumia nishati mbadala katika matumizi yake, ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mkurugenzi wa (JET) Jonh Chikomo amesema ni wakati sasa kwa wadau mbali mbali kuelelekeza nguvu zao katika kuhimili mabadiliko ya tabianchi, ambayo athari zake zimeanza kuelekea katika masuala ya uchumi wa buluu.

Afisa Mdhamini Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Pemba Dk.Salum Mohamed Hamza, amewataka wakulima kuongeza bidii katika kilimo hicho, kwani kiwanda kitakapoanza kiweze waweze kukidhi mahitaji ya kiwanda hicho kwa kuzalisha tani zaidi ya elfu 30000 kwa mwaka.

MWISHO