Friday, February 28

Urusi na Iran: Uhusiano mgumu kati ya wapinzani wawili wa kihistoria ambao wanaungana kukabiliana na Magharibi

Rais Rais wa Iran na Vladmir PUtin wa Urusi

Urusi imesalia kuwa kisiwa baada ya kutengwa na mataifa mengi duniani baada ya uvamizi wake wa Ukraine, Hali ambayo ilifanya taifa hilo kutafuta miungano ya mataifa mengine ambayo katika nyakati zale bora zaidi isingezingatia: moja wapo ni uhusiano wake mgumu na Irani.

Ni mataifa yaliyogawanyika kwa masuala kadhaa, kuanzia kihistoria, kutokana na dhuluma ambayo Wairani wengi wanakumbuka kuwa waliteseka kutoka kwa Dola ya Urusi na Umoja wa Kisovieti, hadi kiuchumi, kwa vile wao ni wapinzani katika masuala ya nishati.

Lakini uadui wao na nchi za Magharibi mara nyingi huwaleta pamoja

Tangu aanzishe uvamizi wake nchini Ukraine, Rais wa Urusi Vladimir Putin amefanya safari tano nje ya nchi, zote zikipakana na mataifa ya zamani ya “stan” ya Soviet, isipokuwa safari yake ya Tehran Julai iliyopita.

Cha kushangaza, katika ziara hiyo, Putin alitoa wito wa utatuzi wa kidiplomasia wa mzozo wa Syria “madhubuti” kwa kuzingatia “kanuni za msingi za kuheshimu mamlaka, uhuru, umoja na uadilifu wa eneo.”

Safari ya Iran ilitumiwa na Putin kujaribu kuonyesha kwamba, licha ya majaribio ya kuitenga Urusi, bado ina washirika na ina umuhimu fulani katika jukwaa la kimataifa.

Lakini kwa kweli, ilionekana na wengi kama ushahidi zaidi wa ubaguzi wa kisiasa na kidiplomasia wa Urusi.

“Inaonyesha kiwango ambacho Bw. Putin na Urusi wanazidi kutengwa. Sasa wanapaswa kugeukia Iran kwa usaidizi,” alisema John Kirby, msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la White House.

.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Urusi imekuwa ikifanya mashambulizi ya anga ya ndege zisizo na rubani za Iran kwenye mji mkuu wa Ukraine Kyiv.

Hivi majuzi, Urusi ilipata msaada wa kijeshi nchini Iran.

Katika shambulio dhidi ya mji mkuu wa Ukraine Kyiv siku ya Jumatatu, vikosi vya Urusi vilitumia ndege zisizo na rubani za Shahed-136 zilizotengenezwa na Iran ambazo zina uwezo wa kusafiri zaidi ya kilomita 2,000 na zinaweza kuruka zikijiendesha.

Ingawa Tehran imekataa rasmi kusambaza vifaa hivyo kwa Urusi, maafisa wa Marekani wanasema usafirishaji wa kwanza ulifanywa mnamo Agosti.

Ripoti ya hivi majuzi ya Taasisi ya Utafiti wa Vita, taasisi yenye makao yake makuu mjini Washington, inaonyesha kwamba kundi la Wairani huenda walisafiri katika maeneo yanayokaliwa na Urusi nchini Ukraine kufundisha vikosi vya Urusi jinsi ya kutumia ndege zisizo na rubani.

Marafiki” na wapinzani

Putin na Ebrahim Raisi, rais wa Iran, wanaongoza mataifa yaliyowekewa vikwazo zaidi duniani, yakifuatiwa na Syria, Belarus na Venezuela, ambazo pia zina tawala zinazotiliwa shaka na kukosolewa na nchi za Magharibi.

Lakini uhusiano wa Urusi na Irani ni mgumu zaidi kuliko Putin angependa

 Hamidreza Azizi, mtaalamu wa uhusiano wa Iran na Urusi katika Taasisi ya Kimataifa na Usalama wa Ujerumani, anasema Moscow na Tehran zina uhusiano ambao unaweza kufafanuliwa kuwa ni mchanganyiko unaobadilika-badilika wa urafiki na ushindani.

“Viongozi wa sasa wa nchi zote mbili wanapenda kusisitiza kwamba wana uhusiano wa kimkakati na kwamba wao ni washirika,” aliambia BBC Mundo.

“Lakini kwa upande mwingine, ikiwa tunaona jinsi wanavyofanya kazi nchini Syria na ikiwa tutazingatia masuala ya nishati, tunaona kwamba wao pia wana ushindani,” anaongeza.

Ingawa Urusi na Iran zinakubaliana kwamba Bashar al-Assad abaki katika amri ya Syria, Moscow na Tehran zimeonyesha maslahi yanayoingiliana.

Wanadumisha mapambano fulani kwa ajili ya udhibiti wa maeneo fulani na wana maono tofauti sana ya jinsi Syria inapaswa kuonekana baada ya vita.

Historia ya uhusiano mgumu

Lakini ushindani wa Russia na Iran ni wa kihistoria.

.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979 yalijumuisha kukabiliana na ushawishi wa Marekani na uingiliaji wa Soviet nchini humo.

“Wairani wanaishuku sana Urusi, kwa sababu Warusi wana historia ndefu ya kuingilia masuala ya nchi yao,” Azizi anaeleza.

Wakati wa karne ya 19 na sehemu ya karne ya 20, Iran ilibidi ijifunze kuishi na majaribio ya mara kwa mara na yenye mafanikio ya Warusi ya kudhibiti eneo lake na kuathiri siasa zake.

Mojawapo ya malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979, kwa mfano, ilikuwa ni kuukabili Umoja wa Kisovieti.

Hata hivyo. uhusiano huo umeendelea tangu safari ya Putin nchini Iran mwaka 2007, ikiwa ni ziara ya kwanza ya kiongozi wa Urusi mjini Tehran tangu Joseph Stalin mwaka 1943.

Ingawa Azizi anasema bado haoni Urusi na Iran kama washirika, anakubali kwamba hatua kwa hatua zimeanzisha uhusiano wa kimkakati unaozidi kuongezeka tangu wakati huo.

“Nchini Syria, licha ya ushindani kutoka kwa pande zote mbili, kuna ushirikiano mkubwa,” anaelezea.

“Pia tunaona ndege zisizo na rubani za Irani sasa zinatumiwa na Urusi, ambayo haijawahi kutokea.”

“Urusi inataka kuiingiza Iran katika mzozo”

.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Mwanamke katika maandamano huko Poland, Oktoba 17, 2022. Mamia kadhaa ya watu walikusanyika mbele ya ubalozi wa Iran kupinga usambazaji wa ndege zisizo na rubani kwa Urusi.

Msako mkali wa Urusi wa kutafuta washirika kote ulimwenguni ili kukabiliana na ushawishi wa Marekani, hasa baada ya nchi za Magharibi kuiwekea vikwazo vya kutwaa eneo la Crimea mwaka 2014, umeifanya Iran kuwa “mshirika wa urahisi”

Haya yamesemwa na Alam Saleh, mtaalamu katika Kituo cha Mafunzo ya Kiarabu na Kiislamu cha Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia, ambaye anaongeza kuwa Moscow na Tehran zina malengo tofauti na uhusiano huu.

“Urusi inataka kuiingiza Iran katika mzozo na Ukraine na kuhakikisha kuwa Tehran inakosolewa na nchi za Magharibi na kuiweka mbali zaidi na kuitenga na nchi za Magharibi,” anaiambia BBC Mundo.

“Urusi haihitaji silaha za Iran, inataka tu kuungwa mkono wakati wa imetengwa,” anasisitiza.

Kwa upande wa Tehran, hitaji la kushirikiana na Urusi lilikuja baada ya Rais wa zamani Donald Trump kuamua kuiondoa Marekani kutoka kwa makubaliano ya nyuklia ya Iran mnamo 2018.

“Serikali ya Iran ilikuwa katika hali ya kukata tamaa na ililazimika kupitia uhusiano wake mpya na Urusi na kutafuta ushirikiano wa karibu na nchi hiyo,” anasema Azizi wa Taasisi ya Kijerumani ya Masuala ya Kimataifa na Usalama.

Alam Saleh kwa upande wake anaeleza kuwa, Iran inataka na inahitaji uungwaji mkono wa Urusi katika Umoja wa Mataifa na katika wimbi la maandamano ambayo hivi sasa serikali ya Iran inataabika, mbali na kuungwa mkono kiuchumi na kijeshi.

Katika ziara yake nchini Iran, Putin aliahidi kupanua ushirikiano wa kiuchumi na kutia saini mkataba wa kuwekeza katika maeneo ya mafuta na gesi ya Iran.

Nchi mbili ambazo hazipendani

Lakini wengi wana shaka kwamba Urusi itakuwa na msaada mkubwa, angalau kiuchumi.

Kufuatia mfululizo wa vifurushi vya vikwazo vya Magharibi, uchumi wa Urusi unatarajiwa kushuka kwa 3.5% mwaka huu na 2.3% mwaka ujao, kulingana na Shirika la Fedha la Kimataifa.

Hamidreza Azizi anaeleza kuwa uchumi haujawahi kuwa sehemu muhimu ya uhusiano wa Urusi na Iran hata hivyo.

“Kiuchumi, Urusi na Iran ni wapinzani. Mataifa yote mawili yanategemea mapato kutokana na mauzo ya hidrokaboni na nishati.”

Na uchumi wote wa mataifa hayo mawili umeendelea kwa njia ambayo inafanya ushirikiano wa maana kuwa mgumu.

“Ni vigumu kwa Iran kuwa soko la bidhaa za kiteknolojia ambazo Urusi inahitaji na kinyume chake. Ili kukidhi mahitaji yao, nchi zote mbili zinapaswa kuelekea Magharibi au China, kama zimekuwa zikifanya hivi karibuni,” anasema Hamidreza Azizi.

Mustakabali wa uhusiano wa pande mbili utategemea mambo ya ndani ya Iran, Azizi anaonya.

Ikiwa maandamano ya sasa yanayoitikisa Iran yatasababisha mabadiliko ya kimsingi katika mfumo wa kisiasa, “ushirikiano wa kimkakati” na Moscow unaweza kumalizika.

CHANZO CHA HABARI BBC NEWS SWAHILI.