
Michuano ya Kombe la Dunia la Qatar 2022 itaanza tarehe 20 Novemba – ikiwa na maandalizi ya kipekee ya msimu wa baridi ikimaanisha kuwa nyota wengi duniani watashiriki mechi za vilabu vyao hadi wiki moja kabla ya michuano hiyo kuanza.
England tayari ina wasiwasi wao katika safu ya ulinzi na ratiba iliyojaa ndani ya timu hiyo hakika italeta hofu zaidi kwa meneja Gareth Southgate, huku kocha wa Wales Rob Page pia akifuatilia kwa karibu kikosi chake.
Lakini ni nchi gani zingine zina wasiwasi kuhusu hali ya wachezaji nyota wao?
BBC Sport inajaribu kufuatilia….
England
Wachache walidhani kwamba nafasi wa beki wa kulia ingekuwa eneo ambalo lingemtia wasiwasi kocha wa timu hiyo Southgate, hususan kutokana na wingi wa wachezaji aliokuwa nao .hatahivyo hali imebadilika katika wiki za hivi karibuni.
Reece James: Jeraha la goti alilopata dhidi ya AC Milan inamuwacha mchezaji huyo wa Chelsea shaka kuu katika michuano hiyo .
Kyle Walker: Beki huyo wa Manchester City alikuwa amesalia na wiki sita kupona jeraha lake la kinena [lakini anasema kwamba anaamini atahusishwa katika kikosi cha kombe la dunia.
John Stones na Harry Maguire: Stones wa Manchester City na Maguire wa Manchester United wote hawajacheza tangu kupata jeraha la msuli wa paja kwenye mechi ya Ligi ya Mataifa dhidi ya Ujerumani iliosha 3-3 mwezi uliopita.
Kalvin Phillips: Mchezaji huyo wa Manchester City huenda asishiriki baada ya kupata jeraha la bega mnamo mwezi Septemba.
Wales

CHANZO CHA PICHA,REX FEATURES
Gareth Bale anafaa kuwa fiti kuongoza kampeni ya kwanza ya Wales katika Kombe la Dunia baada ya miaka 64 licha ya kukosekana katika klabu ya Ligi Kuu ya Soka ya Los Angeles FC.
Tom Lawrence: The Dragons huenda watamkosa mshambuliaji wa Rangers katika taifa hilo la Ghuba baada ya kutonesha jeraha la goti ambalo linaweza kumweka nje hadi Desemba.
Joe Allen: Kiungo huyo mkongwe hajaichezea Swansea kwa zaidi ya mwezi mmoja baada ya kupata jeraha la msuli wa paja.
Ufaransa
Mabingwa watetezi wa Didier Deschamps bila shaka wana orodha kubwa zaidi ya majeruhi – kutoka kwa kikosi chenye nguvu ya kutisha zaidi ya nchi yoyote ile inayoelekea katika kombe la dunia wiki nne kutoka sasa.
Paul Pogba: Kiungo huyo wa zamani wa Manchester United hajacheza tangu arejee Juventus msimu huu wa joto kufuatia upasuaji wa goti.
N’Golo Kante: Kiungo huyo wa kati wa safu ya ulinzi anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi minne kufuatia upasuaji wa kurekebisha tatizo la misuli ya paja.
Wesley Fofana: Mchezaji mwenza wa Kante Chelsea alichechemea wakati wa ushindi wa 3-0 wa mechi ya Ligi ya Mabingwa nyumbani dhidi ya AC Milan na kuna uwezekano mkubwa wa kutoichezea The Blues kabla ya Kombe la Dunia.
Lucas Hernandez: Mchezaji huyo wa Bayern Munich aliumia paja katika ushindi wa mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona mwezi uliopita, ingawa wakala wake amedai atarejea kabla ya mwisho wa Oktoba.
Boubacar Kamara: Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 alirarua mishipa ya goti baada ya kushiriki mechi nane pekee katika maisha yake ya Aston Villa na atakuwa nje ya uwanja hadi baada ya Kombe la Dunia.
Brazil
Mchezaji mmoja wa Ligi ya Premia anasalia kuwa mashakani kwa timu ya Brazil inayotaka kushinda Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 2002, lakini Richarlison aliyejeruhiwa sasa huenda akashiriki.
Richarlison: Mshambulizi huyo wa Tottenham alionekana akiwa kwenye magongo baada ya kupata jeraha la mguu katika ushindi wa 2-0 wa Spurs dhidi ya Everton mnamo Oktoba 15, lakini mkufunzi wa Tottenham Antonio Conte anasema fowadi huyo wa Brazil anapaswa kuwepo kwa Kombe la Dunia baada ya uchunguzi.
Richarlison aliongeza kwenye Twitter: “Guys, namshukuru Mungu ilikuwa hofu kubwa!! Wiki mbili na nitarudi! Asante kwa ujumbe na upendo.”
Arthur Melo: Kiungo wa kati wa Liverpool anayecheza kwa mkopo Juventus hakuwa na furaha kwenye mitandao ya kijamii, akisema anatarajia jeraha la paja kumfanya akose nafasi ya kupanda ndege kuelekea Qatar.
Ureno
Meneja Fernando Santos anaweza kukosa huduma za wachezaji wanne muhimu kwa kampeni yao ya Kundi H dhidi ya Ghana, Korea Kusini na Uruguay.
Diogo Jota: Mshambuliaji wa Liverpool atakosa Kombe la Dunia baada ya kutolewa nje kwa machela akiwa na jeraha la paja katika muda wa nyongeza wa ushindi wao wa 1-0 wa Ligi Kuu ya Uingereza dhidi ya Manchester City mnamo Oktoba 18.
Pedro Neto: Wolves walisema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22 atakosa Kombe la Dunia baada ya jeraha la kifundo cha mguu alilopata dhidi ya West Ham mnamo Oktoba 1 na kumfanya ahitaji kufanyiwa upasuaji.
Pepe na Nuno Mendes: Porto wanatarajia Pepe mwenye umri wa miaka 39 atakosa michezo kadhaa kutokana na kuteguka goti, huku mlinzi mwenzake Mendes atakuwa nje kwa wiki chache kutokana na tatizo la misuli.
Ujerumani
Wasiwasi mkuu wa Ujerumani Unamzunguka nyota wa Die Mannschaft aliyecheza mechi 48 na kufunga mabao 15 ya kimataifa na mshambuliaji wa Bayern Munich .
Marco Reus: Nahodha huyo wa Borussia Dortmund, 33, alijeruhiwa kano za kifundo cha mguu mwezi Septemba. Jeraha la kifundo cha mguu pia lilimfanya akose ushindi wa Ujerumani wa Kombe la Dunia huko Brazil mnamo 2014.
Leroy Sane: Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alirarua msuli wa paja lake la kushoto wakati Bayern Munich iliposhinda 5-0 dhidi ya Freiburg siku ya Jumapili. Klabu haijatoa muda wa kupona kwa Sane, ikisema tu kwamba watamkosa fowadi huyo “kwa sasa.”
Uholanzi
Uholanzi, ambayo ni mpinzani mkuu wa timu ya taifa ya England au Wales, katika kufuzu kwa raundi ya 16 bora, pia itamkosa mchezaji hmuhimu wa kimataifa.
Georginio Wijnaldum: Kiungo wa kati wa zamani wa Liverpool mwenye umri wa miaka 31, aliyecheza mechi 86, alijeruhiwa kwenye mguu wake wa kulia baada ya kucheza mchezo mmoja tu kwa mkopo akiwa Roma.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Argentina
Argentina walioshikilia nafasi ya pili 2014 pia watalazimika kuvumilia bila mchezaji muhimu wa klabu ya Roma.
Paulo Dybala: Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 atakosa mashindano hayo baada ya kupata jeraha la paja wakati alipokuwa akipiga penalti mapema mwezi Oktoba.
Angel Di Maria: Winga huyo wa zamani wa Manchester United pia alipata jeraha la paja akiwa kwenye majukumu ya Ligi ya Mabingwa akiichezea Juventus wiki iliyopita na atakuwa nje kwa wiki tatu, hivyo kumuacha katika kinyang’anyiro dhidi ya muda kuwa fiti.
Marekani
Marekani, wapinzani wa Kundi B wa England na Wales, wana majeraha mawili muhimu .
Daryl Dike: Mshambulizi wa West Bromwich Albion amekuwa nje kwa tatizo la paja tangu Agosti na bado haijajulikana kama atarejea kabla ya mapumziko ya Novemba.
Miles Robinson: Jeraha la kupasuka kwa tendon ya Achilles kumemuondoa beki wa kati wa Atlanta United kushiriki katika michuano hiyo ya dunia.
Mexico
Mkufunzi Gerardo Martino ana wasiwasi mkubwa juu ya nyota wake wawili wakuu, lakini anasema atawapatia wote wawili hadi dakika ya mwisho kuthibitisha utimamu wao.
Raul Jimenez: Fowadi huyo wa Wolves hajacheza tangu Agosti 31 kutokana na jeraha la paja na ni shaka kubwa kwa michuano hiyo.
Jesus Corona: Winga huyo wa Sevilla alivunjika mguu mwezi Agosti lakini anaendelea kupata nafuu kabla ya muda uliopangwa.
Croatia
Marcelo Brozovic: Kiungo wa kati wa Inter Milan hajacheza kwa takriban mwezi mmoja baada ya kutoka na jeraha la paja wakati wa ushindi wa Croatia wa Ligi ya Mataifa dhidi ya Austria mnamo Septemba.
Uruguay
Ronald Araujo: Barcelona ilisema mwezi Septemba beki huyo huenda akakosa michuano hiyo kutokana na kufanyiwa upasuaji wa nyama ya paja iliyochanika na kumuweka nje kwa miezi miwili hadi mitatu.
Poland
Jakub Moder: Kiungo wa kati wa Brighton hatachezea Poles nchini Qatar baada ya kupasuka kwenye ligament yake ya ndani mwezi Aprili.
Canada
Atiba Hutchinson: Nahodha huyo wa Canada, 39, hajacheza kabisa msimu huu katika klabu yake ya Uturuki, Besiktas, baada ya kupata mchubuko wa mfupa katika maandalizi ya msimu mpya.
CHANZO CHA HABARI BBC NEWS SWAHILI.