Friday, January 31

UVIKO 19, changamoto katika mifumo ya chakula na uzalishaji katika nchi nyingi.

NA ABDI SULEIMAN.

IMEELEZWA kuwa janga la UVIKO 19, limeonyesha uhitaji mkubwa wa mikakati ya jinsi ya kukabiliana na majanga na kupelekea ugumu kwa wakulima, ambao bado wanakabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi katika uuzaji wa mazao.

Hayo yameelezwa na mwakilishi kutoka Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN Family) Stella Kiamba, kutoka shirika la kilimo cha Chakula (FAO), wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya habari Pemba.

Alisema janga la UVIKO 19 limezidi kuonyesha nyufa katika mifumo ya chakula na uzalishaji katika nchi nyingi zikiwemo nchi tajiri ambapo uhaba wa chakula umejitokeza.

Alifahamisha kwamba thelusi moja ya hewa ya kijani kibichi inatokana na mimea na wakati huo huo mimea huathiriwa na mabadiliko ya Tabianchi, hivyo mataifa yanatakiwa kuwa na mfumo endelevu wa uzalishaji wa chakula wenye uewezo wa kulisha watu bilioni 10 kufikia 2025.

“kumaliza tatizo la njaa ni zaidi ya upatikanaji wa chakula, tunapozungumza chakula kingi kinazalishwa cha kutosha idadi ya watu wote tunaoishi katika sayari hii ya dunia,”alisema.

Aidha Stella alisema njia ya kukifikia au kufikiwa na chakula imezongwa na madhila mengi ikiwemo janga la UVIKO 19, migogoro isiyokwisha, masuala ya mabadiliko ya tabianchi na mazingira.

Madhila mengine ni kutokuwepo kwa uwiano katika bei na mivutano ya kimataifa, ambapo kila mtu katika dunia kwa sasa anapata madhara ya matokeo ya changamoto hizo.

Alifahamisha katika nyakati ngumu za dunia ni suluhisho la pamoja ndio njia pekee ya kupatia ufumbuzi wa ujumla ikiwa ni pamoja na kukuza uchumi jumuishi, kushughulikia masuala ya usawa na kujenga ustahamilivu.

Hata hivyo alisema mamilioni ya watu duniani bado hawawezi kukidhi mlo wenye ubora jambo ambalo linalo waweka katika hatari ya kuweza kupata athari zinazotokana na upungufu wa chakula na kutapa utapiamlo.

Naye Afisa Biashara kutoka shirika la Heifer Interanion Wema Chuwa, aliwataka wafugaji kuhakikisha wanajitahidi kufuga kisasa ili kupata maziwa mengi yatakayokidhi soko la kisasa.

Alisema hivi sasa kumekua na mwamko mdogo katika suala la unywaji wa maziwa nchini, hivyo wananchi wanapswa kujikita katika unyaji huo ambao umekua na faida kubwa kwa watoto.

MWISHO