Friday, January 31

ZECO tawi la Pemba lakusanya Shilingi 84,578,500 maonyesho ya siku ya Chakula duniani.

NA ABDI SULEIMAN.

 

JUMLA ya Shilingi 84,578,500 zimekusanywa na shirika la umeme Zanzibar (ZECO) tawi la Pemba, ndani ya maonyesho ya siku ya Chakula duniani huko Chamanangwe.

 

Fedha hizo zimekusanywa kufuatia wateja 408 kupatiwa huduma mbali mbali, ikiwemo usajili wa wateja wapya kwa ajili ya kuungiwa huduma ya umeme, pamoja na malipo mengine ya huduma.

 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Afisa Uhusiano wa ZECO Pemba Haji Khatib, alisema wateja 328 hawahitaji nguzo, wateja 80 wanahitaji nguzo huku wastani wa nguzo 240 zikitarajiwa kutumika kuwafikishia wananchi hao huduma hiyo.

 

Alisema mwamko ulikuwa ni mkubwa sana, kwani wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya kisiwa cha Pemba walifika kufuata huduma hiyo ndani ya maonyesho hayo.

 

Alifahamisha kuwa, wateja watakao ungiwa huduma za harakahara ni wanaoishi karibu maeneo ya Chamanangwe, baada ya kupimiwa na kupewa hesabu zao siku hiyo hiyo.

 

Aidha afisa huyo, alisema maonyesho hayo yamewasaidia sana wananchi kupata uwelewa juu ya suala la Uviko 19, kwani zipo nguzo zinzotolewa bure na ZECO kupitia mradi huo.

 

“Wananchi wengi walikuwa hawajuwi kama kuna  kwenye Uviko 19, sisi tumebahatika kupata nguzo na tutazisambaza bure kwa wananchi wanaohitaji huduma ya umeme,”alisema.

 

Alisema wateja 80 wanaohitaji Nguzo karibu 240, hii idadi ilidhani nguzo zinalipiwa kumbe kwa sasa kupitia mradi wa Uviko 19 nguzo ni bure kupatiwa wateja.

 

Aliwataka wananchi kufahamu kuwa ZECO ipo kwa ajili ya watu wote, na inafanya kazi masaa 24 kwa huduma za zarura ni kupiga simu na kuhudumiwa.

Hata hivyo aliwasihi wananchi kutokukubali kuungiwa umeme na kutakiwa kulipa fedha za nguzo, kwani sasa shirika hilo linatoa huduma ya nguzo bure, lengo ni kuhakikisha Zanzibar nzima inangara kwa umeme.

Naye Mohamed Haji Mkaazi wa kinyikani, alisema watendaji wa ZECO wanapaswa kuweka kambi katika maeneo yenye mchangiko wa watu ili kutoa huduma kama ilivyokuwa Chamanangwe, na sio wananchi kuwafuata ofisini kwao.

Alisema baadhi yao wanakua ngumu kufika mjini kutokana na gharama za nauli, wakati fedha ya kuingizwa huduma ameichanga changa muda mrefu.

Naye Hamad Omar Halfan mkaazi wa Junguni, aliwataka watendaji wa ZECO kuhakikisha wanawapatia huduma ya umeme na sio kuchukua muda mrefu, kwani huduma hiyo wamekuwa wakiisubiria kwa muda mrefu.

Alisema kwa sasa wananchi watahamasika kufuta huduma hiyo, kufuatia kutangazwa kuwa nguzo za umeme ni bure kwa kila mwananchi anayehitaji.

MWISHO