Friday, February 28

Waandishi wa habari za online Kisiwani Pemba wapewa mbinu ya kujikinga.

 

 

AMINA AHMED MOH’D-PEMBA.

Waandishi wa Habari Kisiwani Pemba wameaswa kuzidisha umakini katika utumiaji wa mitandao ya kijamii  ikiwa ni pamoja na kuweka ulinzi katika utumaji  wa taarifa zao ili zisiweze  kudukuliwa.

Ushauri huo ulitolewa na  Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari kisiwani Pemba (Pemba Press Club)  Bakar Mussa   Juma  alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja ya  Usalama wa Mitandao (Digital Security) kwa waandishi wa habari wanaotumia zaidi  mitandao ya kijamii   katika kazi zao  yaliofanyika  katika ukumbi wa  Ofisi hizo Misufini Chake Chake.

Alisema   mitandao imekuwa ikipeleka ujumbe  kwa haraka  zaidi  kwa jamii   ukilinganisha na vyombo vyengine vya habari  vilivyopo nchini lakini kumekuwa na changamoto mbali mbali ambazo kama hawakuwa makini wanaweza kujiingiza katika matatizo wasio yategemea kwa vile kunaweza kukatokea wahalifu wakaharibu dhamira zao.

Alieleza kuwa watumiaji wa mitandao wanawajibu wa kujifunza na kuelewa namna ya kujilinda kwenye  mitandao yao ili isiingiliwe na wahalifu   ambapo kunaweza kupelekea kutokuwepo kwa   usalama  kwa  waandishi wa habari   kutokana na baadhi ya wahalifu kutumia  mitandao  hiyo  kudukua taarifa  pamoja  kufanya uhalifu .

“Kudukuliwa  taarifa kwenye mitandao ya kijamii  aidha za mwandishi mwenyewe lakini hata kazi za kihabari zinazofanywa na kutumwa katika mitandao , kunaweza kukajitokeza upotoshaji kwa kupata taarifa nyingi zisizo sahihi ( Fakenews) ambazo hazijafanyiwa uchunguzi wa kina  na hivyo kuwa ni chanzo cha matatizo hata usalama wa nchi “, alisema.

Aidha Mwenyekiti huyo wa Pemba Press Klab aliwataka  waandishi hao  kuyafanyia kazi mafunzo watakayopatiwa  juu  ya  suala hilo la usalama wa mitandao ili kuweza  kujiweka salama  katika utumiaji wao ambao kwa sasa umekuwa ni changamoto kwa waandishi wa habari.

“Kujiepusha na  mitandao ambayo haiko salama  na kutofautisha fake news, kutasaidia kuwaepusha kujiingiza kwenye matatizo musioyatarajia ,ambapo mutafunzwa namna ya kuweza kulinda taarifa zako na mitandao yenu munayofanyia kazi na hapo mutaweza kufanyakazi bila ya wasi wasi wowote”, alisisitiza.

Kwa upande wake  Mratibu  wa Klabu  hiyo ( Pemba Press Club) Mgeni Kombo  Khamis aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kufikisha elimu watakayopatiwa  kwa waandishi wengine ambao wamekosa fursa hiyo  kutokana na sababu mbali mbali.

Alisema kuwa utumiaji wa mitandao umekuwa na kasi kubwa kutokana na uharaka wake, lakini hakuna mafanikio yasiokuwa na changamoto zake hivyo ni lazima wasiwe wachoyo kuyapeleka mafunzo hayo kwa waandishi wengi zaidi.

“ Klabu haina uwezo wa kuwakusanya waandishi nyote munaotumia mitandao ya Kijamii ,lakini kwa umuhimu wake tumeona tuwaite nyinyi muliohudhuria ili muwe mabalozi kwa wengine  hivyo itumieno fursa hii mulioipata”, alisema Mgeni.

Mratibu huyo aliwataka Waandishi wa habari ambao hadi sasa hawajaamuwa kujiunga kuwa wanachama wa Pemba Press Club, kufanya hivyo ili kuweza kupata fursa mbali mbali za mafunzo hususan yanayotolewa na UTPC na Klabu wenyewe.

Akitoa  Elimu ya Usalama wa mtandao   kwa waandishi hao mkufunzi  aliepatiwa  Mafunzo hayo na Umoja wa Klab za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Haji Nassor Muhamed pamoja  na mambo mengine   alisema kuwa usalama wa mtandao ni kujikinga  na hatari zinazoweza kujitokeza kwa watumiaji   sambamba na kujilinda na hatari zilizokusudiwa na wahalifu na zisizokusudiwa kusambazwa.

“Kuna uhalifu katika mitandao ambao umepangwa na ule uliokuwa haukupangwa  yapo mambo  mbali mbali usioyahitaji unaweza ukayakuta katika simu au Komputa yako  , masuala ya kuingilia email ya mtu kumuazima mtu mwengine, afungue, yote hayo ni hatari na ili ujikinge ni lazima ujue usalama na ulinzi wake “alisema.

Aliwataka waandishi hao kujiengeza zaidi katika kujifunza mambo mbali mbali yanayoweza kuwa kinga ya kujilinda na udukuzi wa taarifa zao kwani kumekuwepo na wahalifu wanaotumia mitandao hiyo kwa maslahi yao ama kwa dhamira ya kumchafuwa mwandishi ama mtumiaji wa mtandao fulani.

Haji Nassor ambae pia ni Mwandishi wa habari wa Shirika la Magazeti ya Serikali aliwasisitiza waandishi hao kutumia mitandao yao kwa ajili ya kuihabarisha jamii mambo mbali mbali na sio kwa matumizi ambayo hayana tija kwa jamii na taifa kwa ujumla ikuchukuliwa kuwa wananchi waliowengi wanafuatilia kusoma habari za mitandao kila wakati.

“ Waandishi wenzangu ni wambie sio kila anaemiliki Mtandao ni mjuzi wa matandao hivyo zitumieni simu  ama Komputa zenu kujifunza zaidi mambo ambayo yanaweza kukuweka katika hatari hata ya maisha yako binafsi”, alieleza.

Waandishi hao walipata fursa ya kujifundisha  mambo mbalimbali   ikiwemo ya usalama wa mitandao ikiwa ni pamoja  na  kujikinga dhidi ya hatari  (Safety) kujikinga  binafsi   ili kuweza kuwa salama katika matumizi ya mitandao kwa vyombo vya mitandao (Security) .

Hata hivyo walifunzwa juu ya tathmini ya hali ya hatari pamoja na mbinu za kujua  program  hatarishi na zisizo hatarishi zinazotokana na matumizi mabaya ya Mitandao.

 

MWISHO.