Urusi ilishindwa kuangusha mifumo ya kompyuta ya Ukraine kwa shambulizi kubwa la mtandao ilipovamia mwaka huu, licha ya utabiri wa wachambuzi wengi.
Kazi ya kikosi kisichojulikana sana cha jeshi la Marekani ambacho kinawinda wapinzani mtandaoni inaweza kuwa sababu moja.
BBC ilipata fursa ya kipekee kuwafikia waendeshaji mtandao wanaohusika katika misheni hii ya kimataifa.
Mapema mwezi wa Desemba mwaka jana, timu ndogo ya kijeshi ya Marekani ikiongozwa na meja kijana iliwasili Ukraine kwa safari ya upelelezi kabla ya kikosi kikubwa zaidi.
Lakini meja aliripoti haraka kwamba alihitaji kubaki. “Ndani ya wiki moja tulikuwa na timu nzima huko tayari kwenda kufanya kazi,” mmoja wa timu anakumbuka. Walikuja kugundua Warusi mtandaoni na wenzi wao wa Ukraine waliweka wazi kuwa walihitaji kuanza kazi mara moja. “Aliangalia hali hiyo na kuniambia kuwa timu haitaondoka,” Meja Jenerali William J Hartman, anayeongoza Kikosi cha Misheni cha Kitaifa cha Cyber cha Marekani, aliambia BBC.
“Karibu mara moja tulipata maoni kwamba ‘ni tofauti nchini Ukraine hivi sasa’. Hatukutuma timu tena, tuliimarisha timu.”
Tangu mwaka wa 2014, Ukraine imeshuhudia baadhi ya mashambulizi muhimu zaidi ya mtandao, ikiwa ni pamoja na ya kwanza ambapo kituo cha umeme kilizimwa katika majira ya baridi kali.
Kufikia mwishoni mwa mwaka jana, maafisa wa kijasusi wa nchi za Magharibi walikuwa wakitazama maandalizi ya kijeshi ya Urusi na wakizidi kuwa na wasiwasi kwamba upepo mpya wa mashambulizi ya mtandaoni ungeambatana na uvamizi, uharibifu wa mawasiliano, nguvu, huduma za benki na serikali, ili kufungua njia ya kunyakua mamlaka.
Jeshi la Marekani la Kamandi ya mtadao lilitaka kugundua kama wavamizi wa Kirusi walikuwa tayari wamejipenyeza kwenye mifumo ya Kiukraine, wakijificha ndani kabisa.
Ndani ya wiki mbili, misheni yao ikawa moja ya kazi zake kubwa zaidi na karibu wafanyakazi 40 kutoka kwenye huduma za kijeshi za Marekani.
Mnamo Januari walikuwa na kiti cha mstari wa mbele wakati Urusi ilipoanza kuandaa njia katika anga ya mtandao kwa uvamizi unaokuja ambapo ulinzi wa mtandao wa Ukraine ungejaribiwa sana.

CHANZO CHA PICHA,JOSEF COLE
Kujipenyeza kwa mitandao ya kompyuta kwa miaka mingi kumekuwa kukihusu ujasusi – kuiba siri – lakini hivi karibuni kumekuwa kukishuhudiwa kijeshi na kuhusishwa na shughuli za uharibifu zaidi kama vile hujuma au maandalizi ya vita.
Hii inamaanisha jukumu jipya kwa jeshi la Marekani, ambalo timu zake zinajishughulisha na misheni ya “Hunt Forward”, kuvinjari mitandao ya kompyuta ya nchi washirika kwa ishara za kupenya.
“Ni wawindaji na wanajua tabia ya ‘mawindo’ yao,” anaelezea opereta anayeongoza kazi ya ulinzi dhidi ya Urusi. Jeshi la Marekani liliomba baadhi ya waendeshaji kuhifadhiwa majina yao na wengine kutambuliwa tu kwa majina yao ya kwanza kutokana na wasiwasi wa usalama.
Tangu mwaka 2018, waendeshaji wa jeshi la Marekani wametumwa kwa nchi 20, kawaida washirika wa karibu, huko Ulaya, Mashariki ya Kati na eneo la Indo-Pacific. – ingawa si nchi kama Uingereza, Ujerumani au Ufaransa, ambazo zina utaalamu wao wenyewe na zina uwezekano mdogo wa kuhitaji au kutaka usaidizi kutoka nje.
Kazi zao nyingi zimekuwa zikipambana na wadukuzi wa serikali kutoka China na Korea Kaskazini lakini Urusi imekuwa adui wao wa kudumu. Baadhi ya nchi zimeona watu wengi wakitumwa, ikiwa ni pamoja na Ukraine, ambapo kwa mara ya kwanza mashambulizi ya mtandao yalijumuishwa na vita kamili.
Kualika jeshi la Marekani katika nchi yako kunaweza kuwa nyeti na hata kuleta utata ndani ya nchi, kwa hivyo washirika wengi hutaka uwepo wa Marekani ubaki kuwa siri.
Mnamo Mei, Lithuania ilithibitisha kupelekwa kwa miezi mitatu ilikuwa imemaliza kufanya kazi kwenye mitandao yake ya ulinzi na mambo ya nje, iliyopewa kipaumbele kwa sababu ya wasiwasi juu ya vitisho kutoka kwa Urusi kutokana na uvamizi wa Ukraine.
Croatia ilikuwa mwenyeji pia hivi karibuni. “Uwindaji huo ulikuwa wa kina na wa mafanikio, na tuligundua na kuzuia mashambulizi mabaya kwenye miundombinu ya jimbo la Croatia,” Daniel Markić, mkuu wa shirika la usalama na kijasusi la nchi hiyo, anasema.

CHANZO CHA PICHA,JOSEF COLE
Lakini taarifa za umma hufunika ukweli kwamba misheni hii mara nyingi huanza bila raha. Hata nchi zinazoshirikiana na Marekani zinaweza kuwa na wasiwasi kuhusu kuruhusu Marekani kujikita ndani ya mitandao nyeti ya serikali.
Kwa kweli, ufichuzi kutoka kwa mkandarasi wa zamani wa ujasusi Edward Snowden miaka 10 iliyopita ulisema kuwa Marekani ilipeleleza marafiki na maadui.
Tuhuma hiyo ina maana kwamba vijana wa kiume na wa kike wanaowasili kwenye misheni mara nyingi wanakabiliwa na mtihani mkali wa ujuzi wao wa kidiplomasia.
Wanajitokeza kwenye uwanja wa ndege wakibeba masanduku mengi ya vifaa vya kiufundi visivyoeleweka na wanahitaji kujenga uaminifu haraka ili kupata ruhusa ya kufanya jambo nyeti – kusakinisha vifaa hivyo kwenye mitandao ya kompyuta ya serikali ya nchi mwenyeji ili kutafuta vitisho.
“Hilo ni suala la kutisha sana ikiwa wewe ni taifa mwenyeji,” anaelezea Jenerali Hartman. “Una wasiwasi mara moja kwamba tutaenda kufanya kitu kibaya au ni aina fulani ya siri ya operesheni.” Kwa ufupi, Wamarekani wanahitaji kuwashawishi wenyeji wao kuwa wapo kuwasaidia – na sio kuwapeleleza.
Washirika wa ndani wakati mwingine huketi na timu za Marekani karibu na vyumba vya mikutano wakifuatilia kwa karibu ili kuhakikisha kuwa hakuna chochote kibaya kinachoendelea.
“Lazima tuhakikishe tunaonesha uaminifu huo,” anasema Eric, mkongwe wa miaka 20 wa shughuli za mtandao. “Kuwa na watu kukaa kando na sisi ni jambo kubwa katika kuendeleza hilo.” Na ingawa tuhuma haziwezi kuondolewa kabisa, adui wa kawaida huwaunganisha pamoja. “Jambo moja ambalo washirika hawa wanataka ni Warusi kutoka kwa mitandao yao,” Jenerali Hartman anakumbuka mmoja wa timu yake akimwambia.

CHANZO CHA PICHA,SPC. CRAIG JENSEN
Timu za Marekani zinasema zinashiriki kile wanachopata ili kuruhusu mshirika wa ndani kuwaondoa Warusi (au wavamizi wengine dhidi ya serikali) badala ya kufanya hivyo wao wenyewe.
Pia hutumia zana za kibiashara ili washirika wa ndani waweze kuendelea baada ya misheni kukamilika.
Uhusiano mzuri unaweza kutoa faida. Mwishoni mwa misheni moja, waendeshaji wa Marekani wanasema kwamba washirika wa ndani waliwapa zawadi ya kuwaaga – diski ya kompyuta iliyo na programu hasidi, kutoka kwa mtandao mwingine ambao timu haikuwa ndani.
Kila misheni ni tofauti na kuna baadhi ambapo adui amepatikana katika siku ya kwanza ya kutazamwa, anaelezea Shannon ambaye ameongoza misheni mbili huko Ulaya. Lakini mara nyingi huchukua wiki moja au mbili kuibua wadukuzi wa hali ya juu zaidi ambao wamejiimarisha zaidi. Mchezo wa paka na panya mara nyingi huchezwa na wadukuzi kutoka mashirika ya kijasusi ya Urusi ambao ni mahiri katika kubadilisha mbinu.
Mnamo 2021, iliibuka kuwa Warusi walikuwa wametumia programu kutoka kwa kampuni inayoitwa SolarWinds kupenyeza mitandao ya wateja walioinunua. Waendeshaji wa Marekani walianza kutafuta athari za uwepo wao.
Sajenti wa teknolojia katika Kamandi ya Mtandao ambaye alipenda mafumbo aliona jinsi Warusi walivyokuwa wakificha namba zao za siri katika nchi moja ya Ulaya, Jenerali Hartman anasema.
Kwa kuifungua, aliweza kubaini kuwa Warusi walikuwa wamejificha kwenye mtandao. Sampuli nane tofauti za programu hasidi, zote zikihusishwa na ujasusi wa Urusi, ziliwekwa wazi ili kuruhusu uboreshaji wa ulinzi.
Mara nyingi Marekani imekuwa na shida kutambua na kuondoa udhaifu ndani ya nchi, iwe katika sekta au serikali, kwa sababu ya mwingiliano wa majukumu kati ya mashirika tofauti hata inapotuma waendeshaji wake nje ya nchi.
Misheni za Hunt Forward zimeorodheshwa kama za “kujilinda” lakini Jenerali Paul Nakasone, anayeongoza Kamandi ya Jeshi la Wanajeshi na Wakala wa Usalama wa Kitaifa alithibitisha misheni ya kukera pia imefanywa dhidi ya Urusi kufuatia uvamizi wa Ukraine. Lakini yeye na wengine walikataa kutoa maelezo zaidi.
Wengi walitabiri huu ungekuwa mwanzo wa wimbi la mashambulizi ya kuangusha maeneo muhimu kama reli. Lakini hilo halikutokea. “Moja ya sababu ambazo Warusi huenda hawakufanikiwa sana ni kwamba Waukraine walikuwa wamejiandaa vyema,” anasema Jenerali Hartman. “Kuna fahari kubwa kwa jinsi walivyoweza kulinda. Walimwengu wengi walidhani wangeshindwa tu.
Na hawakuwa,” anasema Al, mchambuzi mkuu wa kiufundi ambaye alikuwa sehemu ya timu ya kupelekwa ya Ukraine. . “Walipinga.” Ukraine imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya mtandaoni ambayo yakifanikiwa yangeathiri miundombinu.
Lakini nchi imeendelea kujilinda kuliko wengi walivyotarajia. Maafisa wa Ukraine wamesema kuwa hii imekuwa kwa kiasi kutokana na usaidizi kutoka kwa washirika, ikiwa ni pamoja na Kamandi ya Mtandao ya Marekani na sekta binafsi pamoja na uzoefu wao wenyewe unaokua.
Sasa, Marekani na washirika wengine wanageukia Waukraine kujifunza kutoka kwao. “Tunaendelea kushiriki habari na Waukraine, wanaendelea kushiriki nasi habari,” anaelezea Jenerali Hartman.
“Hilo ndilo wazo zima la ushirikiano huo wa kudumu.” Huku maafisa wa ujasusi wa Ukraine na nchi za Magharibi wakielezea wasiwasi wao kwamba huenda Moscow ikajibu vikwazo vya hivi karibuni vya kijeshi kwa kuzidisha mashambulizi yake ya mtandaoni, ni ushirikiano ambao huenda ukakabiliwa na majaribio zaidi.
CHANZO CHA HABARI BBC NEWS SWAHILI.