Mabadiliko ya hali ya hewa: Hakutakuwa na barafu Mlima Kilimanjaro ifikapo 2050
Barafu kote ulimwenguni – ikiwa ni pamoja na zile za mwisho barani Afrika – bila kuepukika zitapotea kabisa ifikapo mwaka 2050 kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, UN inasema katika ripoti.
Theluthi moja ya barafu katika maeneo ya Urithi wa Dunia wa Umoja wa Mataifa itayeyuka ndani ya miongo mitatu, ripoti ya UNESCO iligundua.
Barafu za mwisho za Mlima Kilimanjaro zitatoweka kama vile barafu katika Milima ya Alps na Hifadhi ya Kitaifa ya Yosemite nchini Marekani.
Zitayeyuka bila kujali hatua za ulimwengu za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, waandishi wanasema.
Ripoti hiyo, ambayo hufanya makadirio kwa kuzingatia data za satelaiti, inakuja wakati viongozi wa dunia wakijiandaa kukutana nchini Misri kwa ajili ya mkutano wa wiki ijayo wa mabadiliko ya tabia nchi COP27.
Takriban barafu 18,600 zimetambuliwa katika maeneo 50 ya Urithi wa Dunia wa Umoja wa Mataifa.
Zinawakilisha karibu 10% ya eneo lenye barafu la Dunia na ni pamoja na maeneo mashuhuri ya watalii na maeneo matakatifu kwa wakaazi wa eneo hilo.
Kupungua ba kutoweka kabisa kwa barafu ilikuwa “miongoni mwa ushahidi wa kushangaza kwamba hali ya hewa ya Dunia inaongezeka joto”, ripoti hiyo ilisema.
“Tunatumai tunaweza kuwa tumekosea, lakini hii ndiyo sayansi ngumu,” alisema afisa mradi wa UNESCO Tales Carvalho Resende, mmoja wa waandishi.
“Miamba ya barafu ni mojawapo ya viashirio muhimu vya mabadiliko ya hali ya hewa, kwa sababu yanaonekana. Hili ni jambo ambalo tunaweza kuona likifanyika.”
Theluthi mbili iliyobaki ya barafu katika maeneo ya Urithi wa Dunia wa Umoja wa Mataifa inaweza kuokolewa, lakini ikiwa tu dunia itapunguza ongezeko la joto duniani hadi 1.5C, waandishi wanasema.
Ripoti nyingine ya Umoja wa Mataifa wiki iliyopita iligundua kuwa dunia kwa sasa “haina njia ya kuaminika” kufikia hilo.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Makadirio hayo yanatokana na ripoti ya awali ambayo ilitumia modeli kukokotoa jinsi barafu za tovuti ya Urithi wa Dunia zingebadilika kadiri muda unavyopita.
“Jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa katika rekodi ya kihistoria ni jinsi hii inavyotokea haraka,” alisema Beata Csatho, mtaalamu wa mtaalamu wa barafu kutoka Chuo Kikuu cha Buffalo, ambaye hakuhusika katika utafiti huo.
“Katikati ya miaka ya 1900, barafu zilikuwa thabiti,” alisema.
“Kisha kuna hii kuanza kuyeyuka haraka sana.”
Maeneo ya Urithi wa Dunia yaliyoorodheshwa kuwa barafu yake itatoweka ifikapo 2050 ni:
- Misitu ya Hyrcanian (Iran)
- Mbuga ya Kitaifa ya Durmitor (Montenegro)
- Mbuga ya Kitaifa ya Virunga (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo)
- Eneo la kivutio cha utalii na Kihistoria la Huanlong (Uchina)
- Mbuga ya Kitaifa ya Yellowstone (Marekani)
- Mbuga ya Kitaifa ya Mlima Kenya/Msitu wa Asili (Kenya)
- Eneo la Pyrenees Mont Perdu (Ufaransa, Uhispania)
- Mbuga ya Kitaifa ya Milima ya Rwenzori (Uganda)
- Putorana Plateau (Russia)
- Swiss Tectonic Arena Sardona (Uswizi)
- Hifadhi ya Kitaifa ya Nahanni (Canada)
- Hifadhi ya Kitaifa ya Lorentz (Indonesia)
- Mfumo Asilia wa Hifadhi ya Kisiwa cha Wrangel (Urusi)
- Hifadhi ya Kitaifa ya Kilimanjaro (Tanzania)
- Hifadhi ya Kitaifa ya Yosemite (Marekani ya Amerika)
- Misitu ya Virgin Komi (Urusi)

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Ripoti hiyo ilisema kuwa kupotea kwa barafu katika maeneo ya Urithi wa Dunia huenda umesababisha hadi 4.5% ya ongezeko la kina cha bahari duniani kote kati ya 2000 na 2020.
Barafu hizi hupoteza tani bilioni 58 za barafu kila mwaka – sawa na jumla ya kiasi cha kila mwaka cha maji yanayotumika Ufaransa na Uhispania zimewekwa pamoja.
Watu wengi pia wanategemea barafu kama chanzo chao cha maji kwa matumizi ya nyumbani na kilimo, na hasara yao inaweza kusababisha uhaba wa maji safi wakati wa kiangazi, alisema Prof Duncan Quincey, mtaalamu wa barafu katika Chuo Kikuu cha Leeds ambaye hakuhusika katika utafiti.
“Hiyo inasababisha masuala ya usalama wa chakula kwa sababu walikuwa wakitumia maji hayo kumwagilia mazao yao,” alisema Quincey.
Jamii za wenyeji na watu wa asili watabeba msalaba mkubwa wa mafuriko yaliyosababishwa na kupotea kwa barafu, wasema waandishi wa ripoti hiyo, wakihimiza kwamba mifumo ya maafa ya kuonya mapema na kupunguza hatari kuwekwa.
Hata hivyo jambo la wazi zaidi tunalohitaji kufanya ni kupunguza ongezeko la joto duniani.
“Kuna ujumbe wa matumaini hapa,” Carvalho Resende alisema.
“Ikiwa tunaweza kudhibiti kupunguza kwa kiasi kikubwa hewa chafu, tutaweza kuokoa sehemu kubwa ya barafu hizi.”
“Kwa kweli huu ni wito wa kuchukua hatua katika kila ngazi – sio tu katika ngazi ya kisiasa, lakini katika ngazi yetu kama wanadamu.”
CHANZO CHA HABARI BBC NEWS SWAHILI.