Thursday, January 16

Asasi za kiraia na viongozi wamesema ipo haja ya kuwa na sheria moja maalumu ya kiislam (Muslim Family Law)

Mhadhiri kutoka Chuo kikuu cha Zanzibar University Dkt,Sikujua Omar akiwasilisha ripoti maalumu iliotazama changamoto wanazokutana nazo wanawake wanaoachika.

Picha ya pamoja ya wadau mbali mbali walioshiriki kwenye mkutano huo.

Na Muhammed Khamis,TAMWA-ZNZ 

Wadua mbali mbali kutoka Asasi za kira na viongozi wamesema ipo haja ya kuwa na sheria moja maalumu ya kiislam (Muslim Family Law) itakayosimamia masuala yote yanayohusiana na Familia, hasa katika kipengele cha ugawaji wa mali walizochuma pamoja wanandoa pindi ndoa inapovunjika,  matunzo kwa watoto na matunzo ya mwanamke akiwa katika eda, pamoja na ugawaji wa mirathi.

Wamesema wanaona kuna ulazima wa kuwepo kwa sheria hiyo hivi sasa kutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi ambayo Mahakama ya Kadhi huyatolea maamuzi lakini maamuzi hayo hushindwa kutekelezwa.

Wadau hao waliseama kuwa kuna changamoto kubwa licha ya kuwa Mahakama ya Kadhi inafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria, lakini bado sheria ya Mahakama ya Kadhi haina kifungu cha kumuajibisha mtu aliekataa kutii maamuzi ya Mahakma hiyo  na ndio maana kumekuepo na  idadi kubwa ya walalamikaji ndani ya  jamii wakieleza kunyimwa haki zao na wakati mwengine hata kudhulumiwa.

Wadau wa Asasi hizo wameyasema hayo mjini Unguja katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake  yaliofanyika katika ukumbi wa jengo la ZURA mjini hapa.

Awali akiwasilisha ripoti ya mapungufu yaliyopo katika sheria   za Kiislam inazosimamia masula ya familia ikiwemo mirathi na talaka Dokta Sikujua Hamdan alisema kuwa, lengo la uwasilishaji wa ripoti hiyo ni kupata maoni kutoka kwa wadau ili kuweza kutayarisha mswaada wa  sheria moja ya Kiislam itakayosimamia masuala ya kifamilia na itakayotoa haki na usawa kwa wanawake na Watoto.

Dokta Sikujua alisema Miongoni mwa sheria  ambazo zimepitiwa na kuonekana kuwa zina mapungufu ni Pamoja na Sheria ya Mahakama ya Kadhi Na.9 ya mwaka 2017, Sheria ya Mufti Na 4 ya mwaka 2021, Sheria ya Wakfu na Mali Amana ya mwaka 2007, na Sheria ya Mtoto ya mwaka Na. 6 ya mwaka 2011, ambapo Sheria hizo zinaonekana kuwa na mapungufu yanayopelekea kuwanyima haki  wanawake na watoto hasa katika suala la mgawanyo wa mali, haki ya mwanamke baada ya talaka na matunzo ya watoto baada ya kuachana jambo ambalo hupelekea utelekezwaji na udhalilishwaji kwa  watoto kwa kukosa haki zao za msingi ikiwemo haki ya kulindwa, kupata elimu jambo ambalo hupelekea kuongeza idadi ya watoto wa mitaani kwa kukosa malezi bora ya wazazi.

Wakichangia ripoti hiyo wadau hao walisema kumeonekana kuna umuhimu kwa hivi sasa kuwa na sheria ya Kiislam itakayosimamia masuala yote ya familia, nae Kadhi wa Mahakama ya Wilaya ya kusini Unguja Ali Sharif Maalim alifafanua kuwa anaamini upatikanaji wa sheria Mama ya Kiislam itakayosimamia masuala ya familia kutasaidia kuzipatia ufumbuzi changamoto nyingi za kifamilia na alisisitiza kuwa iwapo sheria hiyo itakapopatikana basi jamii  pia lazima ieleweshwe juu ya sheria ili kwa pamoja iweze kutekelezwa kwa mustakabali wa ustawi wa Wanawake na Watoto.

Awali mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Katibu wa Tume ya kurekebisha sheria Zanzibar Mussa Kombo Bakari alisema wanaungana na wadau wote wenye kutaka mabadiliko ya sheria mbalimbali zenye lengo la kusaidia kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

Aidha katibu huyo wa Tume ya kurekebisha Sheria alisema ipo haja ya kuendelea kufanya tafiti Zaidi kuangali sababu ya uwepo wa matukio ya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto kila kukicha ili kwa pamoja kutafuta mbinu madhubuti za kupambana na vitendo hivi.

Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake  ni kampeni maalumu ya kimataifa kufuatia mauaji ya kinyama ya wanawake  yaliyotokea Jamhuri ya  Dominika mwaka 1960.

Umoja wa Mataifa ulizitenga Siku hizi 16 kendesha kampeni ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake, maadhimisho haya huanza tarehe 25 ya Novemba ya kila mwaka na hufikia kilele chake tarehe 10 Desemba ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Kuadhimisha Tamko Rasmi la Haki za Binadamu, ikiwa ni ishara ya kuhusisha ukatili dhidi ya wanawake na haki za binadamu na pia kuweka msisitizo kwamba ukatili wowote wa kijinsia ni uvunjwaji wa haki za binadamu.