Monday, November 25

UWT Mkoa wa Kusini Pemba yakabidhi vifaa hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani.

NA HANIFA SALIM, PEMBA

UMOJA wa wanawake (UWT) Mkoa wa Kusini Pemba umesema, utaendelea kuisadia serikali kuzitatua changamoto ili kuhakikisha inaendeleza shughuli zake za kimaendeleo kama ilivojipangia.

Hayo yameelezwa na Mjumbe wa baraza kuu Taifa (UWT) Mkoa wa Kusini Pemba Maryam Said Khamis, katika hafla ya kukabidhi vifaa kwa hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi CCM.

Alisema, ni katika kazi zao za kawaida kupita kwenye taasisi mbali mbali kuangalia changamoto zinazoihusu jamii, ambapo lengo lake ni kuisaidia serikali katika kutekeleza majukumu yake.

“Matumaini yangu vifaa hivi vitatumika kama inavotakiwa kwa wahitaji ambao tumewakusudia tusifanye mambo ambayo hatukutarajia, tushirikiane katika kutekeleza majukumu yetu ili dhamira ya serikali yetu iweze kufikiwa”, alisema.

Mwenyekiti wa (UWT) Wilaya ya Mkoani Maryam Matora Hussein alisema, ni kawaida yao kupita katika hospitali hiyo mara kwa mara kuangalia changamoto ambazo zinaikabili ili zile ambazo jumuiya wanaziweza huzichukua na kuzifanyia kazi.

“Niwaombe Madaktari mutupokelee hichi kidogo ambacho tumewafikishia ingawa ni vichache lakini (UWT) Wilaya ya Mkoani inakwenda kujipanga tena zaidi, tunaomba mshirikiano yenu ili tufikie malengo”, alisema.

Aidha alisema, (UWT) katika siku yao ya wanawake wamekua na kawaida kupita katika hospitali hiyo kufanya shughuli mbali mbali ikiwemo kuchangia damu, kufanya usafi na kutoa misaada ya vifaa vya aina tofauti.

Katibu wa jumuiya ya wanawake (UWT) Wilaya ya Mkoani Amina Haji Kheir alisema, baada ya jumuiya yao kutembelea hospital hiyo na kubaini uhaba wa vifaa imeona kuna haja ya kuelekeza nguvu zao ili kuisaidia jamii.

Hata hivyo, alisema kutoka na muda waliotembelea katika hospitali hiyo kuwa ni mfupi hawakuweza kujipanga vizuri, hivyo wameahidi watarudi tena kuongeza nguvu zao ili kuhakikisha sekta muhimu ya afya inafikia lengo.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Daktari dhamana wa Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani msaidizi Katibu wa Hospitali hiyo Said Ali Said, aliishukuru (UWT) kwa ujio wao huo, alisema wanathamini mchango wao mkubwa ambao wamekua wakiutoa kwao siku hadi siku.