JUKWAA LA PILI LA MSAADA WA KISHERIA ZANZIBAR 2022
Laibua maazimio 16 yenye shabaha ya uimarishaji utoaji msaada wa kisheria
LSF yaahidi makubwa, Mkurugenzi Hanifa aupiga mwingi
NA HAJI NASSOR, PEMBA
DISEMBA 13 na 14 mwaka 2022, ilikuwa ni siku adhimu na adimu, zilizofanyika jukwaa la pili la msaada wa kisheria Zanzibar.
NINI MAANA YA JUKWAA?
Ni mkutano, mjadala, kongamano la wazi linalowakutanisha wadau wa haki jinai, kujadili, kubadilishana uwezo na kukosoana, kwa njia amani.
Maana kupitia jukwaa hilo, linalowakutanisha wadau zaidi ya 200 kutoka Unguja na Pemba, huandaliwa na wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, chini ya Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria.
Jukwaa hilo, liliwakutanisha watoa msaada wa kisheria, wasaidizi wa sheria, mahakimu, waendesha mashtaka, wanufaika wa msaada wa kisheria, Polisi, masheha na wanaasasi za kiraia.
Kwa jicho la kawaida utaona kuwa, jukwaa hilo linamtiki kwa wadau hao kukutana, na kujadili changamoto, mafanikio, mwelekeo na dira ya baadae, ya utaoji wa msaada wa kisheria.
LSF
Tasisi hii, imekuwa ndio mdau mkuu wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria sio tu, kufanikisha majukwaa kama hayo, lakini hata, kuiwezesha Idara, kufikia malengo yake.
Ijapokuwa Idara hiyo ni ya serikali, lakini kupitia sheria yake nambari 13 ya mwaka 2018 ya Msaada wa Kisheria na hata sera yake ya mwaka 2017, hazijakataa kushirikiana na wadau.
Ndio maana, katika jukwaa la mwaka huu, ambalo lilifanyika tena Chuo cha Utalii Maruhubi mjini Unguja, na kufunguliwa na Makamu wa Pili wa rais Hemed Suleiman Abdulla, mwakilishi wa LSF alitoa neno.
‘’Niiombe sana serikli kuhakikisha, sheria ya Msaada wa Kisheria Zanzibar, nambari 13 ya mwaka 2018, ifanyiwe marekebisho,’’anasema Lulu Mwanakilala.
Mwanakilala hapa, kumbe hakulala alichoona ni kufuatia ushauri huo kwa serikali, kutaka kuwepo kifungu kipya, kinachoruhusu uanzishwaji kwa Mfuko wa Msaada wa Kisheria Zanzibar ‘MMSAKIZA’
Hapa akisema, mfuko huo sasa unaweza kuchangiwa na serikali na watu wa asasi za kiraia, au mtu mmoja mmoja, ili sasa kuwasaidia watoa msaada wa kisheria Zanzibar.
Jengine alilolishauri kwenye jukwaa hilo, Lulu anasema wakati umefika kwa wasaidizi wa sheria, ambao hawana mishahara kupewa ofisi chini Idara ya serikali za Mitaa, ili wapunguze gharama za kukodi ofisi.
IDARA YA KATIBA, MSAADA WA KISHERIA ZANZIBAR
Ambapo Mkurugenzi wa Idara hii, Hanifa Ramadhan Said wakati akisoma yataokanayo na jukwaa la mwaka 2021, anasema yapo mengi yaliotekelezwa, baada ya kupendekezwa.
‘’Kwa sasa wasaidizi wa sheria wetu, wanavitumia vyombo vya habari wanapokuwa na shughuli zao za kutoa elimu kwa wananchi,’’anasema.
Hata suala la ushirikiano, kati ya wasaidizi wa sheria na watendaji wa serikali, unatia moyo, jambo ambalo limerahisisha utendaji wa kazi zao.
Mkurugenzi Hanifa hakuacha kuipongeza tasisi ya LSF, kwa kuendelea kuwaunga mkono, katika utekelezaji wa shughili zao hasa za kujengeana uwezo.
Kisha kwenye siku ya pili, kabla ya jukwaa hilo kufunguwa akasoma maazimioa 16 yalioibuliwa na kupitishwa na washiriki wa jukwaa hilo.
Yote ni mazuri na moja wapo ni kwa LSF kuendelea kusadiana kuwajengea uwezo watendaji wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, pamoja na kufunguliwa kwa ofisi za wasaidizi wa sheria katika ofisi ya wilaya.
‘’Kuhakikisha kuandika ripoti za utendaji kazi, kwa kugusia malengo 17 endelevu ya dunia, ili kuonesha muitikio wa jamii pamoja na kuimarisha mifumo, itayohakikisha taifa linakuwa na raia wema,’’alifafanua.
Azimio jengine ni kwa Idara hiyo, kuhakikisha inachukua juhudi za kuratibu na kufanya marekesbisho ya sheria ya Msaada wa Kisheria, ili kuweka mfuko wa taifa wa Msaada wa kisheria.
Mkurugenzi huyo akasema azimio jingine ni kuongeza kasi ya mafunzo ya usuluhishi na utatuzi wa migogoro kwa wasaidizi wa sheria.
Afisa sheria wa Idara hiyo Unguja Ali Haji Hassan, anasema lazima wasaidizi wa sheria, wazidishe kasi ya kuwafikia wananchi kuwapa elimu, ushauri na msaada wa kisheria.
SERIKALI KUU
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah, yeye ndie aliyekuwa mgeni rasmi, katika jukwaa hilo, na kuelezea namna wasaidizi wa sheria, wanavyofanya kazi zao.
Licha ya kuvutiwa huko, amewakumbusha wasaidizi wa sheria na watoa msaada wa kisheria, kuendelea kufanya kazi zao kwa uweledi.
Hapa, akasema hasa nguvu zaidi kwao ni mapambano ya udhalilishaji, rushwa na dawa za kulevya, ambazo zinaendelea kugharimu maisha ya vijana.
Maana anaona kuwa, bado jamii inakabiliwa na changamoto hizo, hivyo ni wajibu wao kuendelea kutumia weledi wao, ili wananchi waishi kwa salama, bila ya kuwa na changamoto hizo.
Lakini hata waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, yeye akasema, serikali, inajua kazi inayofanywa na wasaidizi wa sheria.
Hapa nae akawasisitiza wasaidizi wa sheria wazidishe kasi na juhudi za kuhakikisha, wanaifikisha elimu husika kwa jamii.
Mwalimu Haroun, kama wengi wanavyomuita, akaendelea kutoa darssa kwa wasaidizi hao wa sheria kuwa, serikali itaendelea kuwa karibu mno, na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria.
Lengo anasema kwanza kuwatia moyo watendaji hao wanaoongozwa na Mkurugenzi Hanifa, ili kuona wanafanikisha malengo yao, ya kuifikia jamii.
‘’Muelewe kuwa, kazi hii ya utoaji wa masaada wa kisheria ni kazi ya kujitolea zaidi, na malipo yenu ni kwa Muumba zaidi, hivyo endeleeni kuwasaidia wananchi, ili wapate haki zao kisheria,’’alieleza.
Lakini Makamu wa Pili, alikumbushia ahadi yake kuwa, yuko tayari kuusaidia mfuko wa msaada wa kisheria, mara utakapoanzishwa, ili kuhakikisha unasaidia kusukuma mbele dhana ya utoaji wa msaada wa kisheria.
Jambo hili lilizua shangwe, vifijo, furaha na kushangiliwa na kupigiwa makofi na wasaidizi wa sheria, waliojazana kwenye jukwaa hilo la mwaka 2022.
‘’Mheshimiwa Waziri, mimi naunga mkono uanzishwaji wa mfuko huo, na niko tayari hata mshahara wangu mmoja kuuweka, na naamini na wengine watasaidia,’’aliweka bayana.
Zamu ikafika ya Naibu Katibu Mkuu wizara ya Nchi Afisi ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Omar Haji Gora, amefurahishwa na uamuzi wa waziri Haroun, pale alipoiagiza Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar, ili kuifanyia marekebisho sheria ya msaada wa kisheria, Zanzibar no 13 ya mwaka 2018.
‘’Ushauri wa wenzetu wa tasisi ya LSF, kuwa sasa sheria yetu tuifanyie marekebisho, ili itambuwe uwepo wa mfuko wa maalum wa msaada wa kisheria, kama ilivyo kwa wenzetu wa Tanzani bara,’’anafafanua.
Akafafanua kuwa, jukwaa hilo ni utekelezaji wa sera ya mwaka 2017 na sheria ya msaada wa kisheria no 13 ya mwaka 2018.
Akafurahishwa na tasisi ya LSF kuwa, imekuwa karibu mno na Idara ya Katiba, Msaada wa Kisheria, katika kufanikisha majukumu yake, hasa ya kuhakikisha, wananchi wanapata haki zao na ufumbuzi wa mambo ya kisheria.
WADAU WA SHERIA
Kwenye jukwaa hilo, wapo waliopata nafasi ya kusema jambo, akiwemo mwakilishi kutoka Umoja wa watu wenye Ulemavu Zanzibar ‘UWZ’ Shaibu Abdalla Mohamed, akasema kuna ahuweni kwa watu wenye ulemavu, juu upatikanaji wa msaada wa kisheria.
‘’Jukwaa hili la pili na sisi kushirikishwa kikamilifu hadi kutoa mada ni hatua moja, maana kwa jukwaa la kwanza hatukushirikishwa kikamilifu,’’anasema.
Kwenye hili, mwakilishi kutoka LSF Said Chitung, akasema kundi la watu wenye ulemavu, lazima liangaliwe kwa macho manne, katika kuwafikia kielimu.
Akichangia kwenye jukwa hilo, Said Rashid Hassan wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ tawi la Pemba, akasema lazima suala la utoaji wa msaada wa kisheria, liendelee kwa kasi.
Akitoa mada ya saikolojia ya jamii na upatikanaji wa msaada wa kisheria kwa wahanga na waathirika wa udhalilishaji katika mfumo wa haki jinai, wakili wa serikali Ali Rajab, anasema ni jambo la kuzingatiwa mno.
‘’Hata matumizi ya maneno wakati wa kumuuliza, kumtaka akuelezea nini alichofanyiwa, usipokuwa makini unaweza kumzidishia maumivu,’’anafafanua.
Anasema saikolojia kwa jamii wakati mwengine, mfano mdhalilishaji haonekani kama ni mtenda kosa kubwa kama kisheria, hivyo lazima kwa watoa msaada wa kisheria walijue hilo.
‘’Ndio maana wapo wanaodhalilishwa, wamekuwa wakikataa kutoa ushahidi makahamani, kwani saikolojia yao kwao hilo sio kosa kubwa,’’alifafanua.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ Harusi Miraji Mpatani, yeye akavishauri vyama vya wanasheria, lazima viongeze nguvu, ili jamii ipate msaada wa kisheria.
Hoja yake ni kuwa, msaada wa kisheria umewalenga wale watu maskini zaidi, hivyo lazima viongozi wa vyama na wale wanasheria, wawasaidie wananchi.
‘’Hapa mawakili wa kujitegemea, lazima sasa tujitolee kuzisimamia kesi bila ya kujali malipo ‘probono cases’ na huo ndio mchango wetu kwa jamii,’’alishauri.
WASAIDIZI/WADAU SHERIA WANASEMAJE
Mkurugenzi wa Jumuia ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, anasema kazi inayofanywa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria ni nzuri.
‘’Hata sisi jumuia za wasaidizi wa sheria, inafaa kwa kila aliyepata mafunzo kuwapa wenzake, maana wakati mwengine inakuwa ngumu wasaidizi wote kufikiwa,’’anasema.
Mkuugezi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Kaskazini ‘A’ Asiya Fadhil Makame, anasema moja ya changamoto wanayokumbana nayoni kukosa elimu ya saikolojia.
‘’Elimu ya mapambano dhidi ya ukatili na udhalilishaji, tunayo ingawa sasa elimu ya saikolojia ndio shida, na wakati mwengine tunawakosa kuongozana na waathirika kwenye mahojiano,’’alisema.
Lakini hata Mkurugenzi wa wasaidizi wa sheria wa sheria wilaya ya Mkoani Nassor Hakim, anasema kupitia jukwaa hilo, linawapa mwanga kwa kule kubadilishana uzoefu na wengine.
Kumbe hili la uwepo wa jukwaa, hata profesa Mohamed Makame kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar ‘SUZA’ anasema, suala la usaidizi wa sheria, linafaa kuungwa mkono na jamii.
‘’Chimbuko la msaada wa kisheria ni la kujitolea zaidi, kwa ajili ya kuwafikishia huduma za msaada wa kisheria, tena bila ya malipo,’’anasema.
Jukwaa hilo lilifungwa Disemba 14, 2022 na Waziri Haroun, ambae aliwataka wasaidizi wa sheria, kuyafanyiakazi, yale waliyoyapata kwenye jukwaa hilo.
Ambapo ujumbe wa mwaka huu ni ’Uimarishaji wa Huduma Bora na endelevu za utoaji wa msaada wa kisheria Zanzibar ‘’.
Mwisho