Monday, November 25

MDHAMINI ELIMU PEMBA, AWAONESHA NJIA WAALIMU KUFIKA MBALI

NA HAJI NASSOR, PEMBA

WAALIMU wa skuli za msingi na sekondari kisiwani Pemba, wametakiwa kuongeza uadilifu, uaminifu, heshima na uzalendo wanapokuwa kazini, ili ufanisi na tija ipatikane.

 

Kauli hiyo imetolewa leo Disemba 19, 2022 na Afisa Mdhamini wizara ya elimu na mafunzo ya amali kisiwani humo Mohamed Nassor Salim, wakati alipokuwa akiyafungua mafunzo ya siku mbili, kwa waalimu hao, yenye lengo la kuthibitishwa kazi.

Alisema, kazi wanayofanya ni kubwa, na inakuwa na tija kwa taifa, na hasa ikiwa wataongeza kasi ya ufundishaji, uadilifu na kuweka mbele uzalendo kwa taifa.

Alieleza kuwa, kila jambo mtu analolifanya lazima afikirie namna ya kuweka uzalendo mbele, na akitia na uadilifu anaweza kufanikisha malengo yake.

‘’Leo (jana) mafunzo haya ni ishara kua, nyinyi ndio chaguo la jamii, kuwatumia katika fani ya ualimu, sasa lazima muongeza uaminifu, ujasiri, uadilifu na uzalendo, ili wanafunzi wakifie lengo husika,’’alieleza.

 

Katika hatua nyingine Afisa Mdhamini huyo, aliwataka waalimu hao kuongeza elimu na kundoka walipo, ili wewe na uweledi wa kulitumikia taifa lao.

‘’Taifa linahitaji waalimu wenye weledi, ili wafundishe wanafunzi kwa ufanisi zaidi, sasa ili kufikia hilo, lazima kila mmoja, aongeze elimu na kufikia ya juu zaidi,’’alieleza.

Hata hivyo, alisema mpango huo wa mafunzo ya uthibitishaji kazini, utakuwa endelevu kwa wafanyakazi wote wa wizara ya elimu na mafunzo ya amali.

Akiwasilisha mada ya uzalendo, muwezeshaji kutoka Chuo cha Utawala wa Umma ‘IPA’ kisiwani Pemba Khamis Nassor, alisema uzalendo, ni vyema ukaanzia ngazi ya familia.

Alisema, kisha upande kwenye ngazi ya kijiji, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla, kufanya shuhguli mbali mbali za kitaifa, kwa lengo la kuendeleza mbele taifa.

Alifahamisha kuwa, sifa moja ya mzalendo ni kutii sheria za nchi bila ya shuruti, kuogopa rushwa, kuwa na lugha nzuri kwa viongozi, heshima na nidhamu kwa kila mmoja.

Muwezeshaji huyo alieleza kuwa, eneo jengine la kuendeleza uzalendo, ni jamii kutekeleza maagizo ya viongozi, mfano suala la kudai risiti za kielektroniki, baada ya kununua.

 

‘’Waalimu, uzalendo hata mnapokuwa kwenye shughuli zenu za ufundishaji upo, mfano unapotumia vifaa vya skuli vibaya mfano chaki au mabuku utakuwa hamna uzalendo,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine, muwezeshaji huyo, aliwataka waalimu hao, elimu waliyoipata kuhakikisha wanawafikishia na wengine, ili wajae uzalendo.

 

Nae Kaimu Mratibu wa Idara ya Uendeshaji na Utumishi ‘MIUU’ wa wizara ya elimu na mafunzo ya amali Pemba, Harith Bakar Waziri, alisema katika zoezi hilo watumushi 1,417 watafikiwa na elimu hiyo.

‘’Mafunzo haya yenye lengo la uthibitishaji wa kazini kwa watumishi wa wizara wakiwemo waalimu, tutahakikisha hakuna atakayebakia,’’alisema.

Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Mafunzo kutoka ‘IPA’ Pemba Abubakar Nuhu, alisema utekelezaji wa program ya mageuzi ya utumishi wa umma, yanawalenga watumishi wote.

Alieleza kuwa, program hiyo, inakusudia kuona kila mtumishi anatekeleza wajibu wake kwa ufanisi, ili wananchi wanapofuata huduma iwe rahisi kwao.

‘’Mpango huu unataka kuona mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya utoaji huduma kwa watumishi mkiwemo nyinyi waalimu, pamoja na kufikiria uimarishaji wa miundo ya kazi,’’alifafanua.

Katika mafunzo hayo, ya siku mbili mada saba zitajadiliwa ikiwa ni pamoja na sheria ya utumishi wa umma nambari 2 ya mwaka 2011, kanuni ya utumishi wa umma ya mwaa 2014, mafunzo ya afya na usalama kazini pamoja na mamlaka ya kuzuia rusha na uhujumu wa uchumi.

                          Mwisho