NA ABDI SULEIMAN.
WASHIRIKI wa Kongamano la wadau wa Amani Kisiwani Pemba, wameiyomba Serikali kuongeza nguvu katika udhibiti wa mitandao ya kijamii, kwani imekua ikitumiwa vibaya na vijana waliowengi.
Walisema vijana wamekuwa wakitumia mitandao hiyo na kupakua, video zinazotoa mafunzo yasioendana na mila silka na utamaduni wa kitanzania na mwisho wake kuingia katika uvunjifu wa amani.
Walisema baadhi ya mitandao hiyo ni kama vile Fecbook, Twitter, Istragram na mitandao mengine, hutumwa video za kivita, wizi, ujambazi, mambo ambayo vijana wengi huvutiwa nayo na mwisho kupelekea kutokufahamiana.
Wadau hao waliyaeleza hayo wakati wa kongamano la wadau wa amani Pemba, liliandaliwa na Kituo cha Majadiliano kwa Vijana Zanzibar CYD, kupitia mradi wa AMANI VISIWANI unaotekelezwa na CYD kwa ufadhili wa shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeloe Duniani (UNDP).
Bakari Makame Khamis alisema kutoka na hali hiyo ni vizuri kwa serikali kushirikiana na TCRA na kuhakikisha video ambazo zinazoweza kupelekea uvunjifu wa amani kutokuruhusiwa kuonekana Tanzania.
“Hebu angalia maeneo ambayo mitandao ipo WIFE utaona vijana kila mmoja yuko bize na simu, sio kama wanasoma wanapakua video ambazo hazifai na kuzitumia,”alisema.
Aidha aliitaka CYD kuwepo na ufuatiliaji na uwendelezaji kwa vijana baada ya kupatiwa mafunzo au mitaji ili kujua matumizi ya mafunzo wanayopatiwa.
Naye Abdulkarim Yussuf Mussa, alisema suala la dini na kiroho linapaswa kupewa kipaombele katika mitaala ya elimu, kwani vijana wataweza kujifunza umuhimu wa amani tokea wakiwa skuli.
“leo utamuona mwanafunzi anamaliza skuli hajuwi chochote masuala ya amani, zaidi ya kupatiwa semina tu kama ingetumika tokea maskulini basi amani ingewajaa akilini mwao,”alisema.
Hata hivyo alitaka kudhibitiwa kwa mifumo ya mitandao ili kuwalinda vijana, kwani nafasi nyingi za kwenda nje ya nchi kwa vijana zinaanzia katika mitandao hiyo.
Kwa upande wake Ali Ramadhan, aliwataka vijana kuzitumia fursa zinazotolewa za uchumi wa buluu, katika suala la kujiajiri na sio kukimbilia nje ya nchi ambako hakuna faida kwao.
Mshiriki mwengine Hadija Mwadini , alisema vitendo vya udhalilishaji vinaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani, kwa jamii husika na kupelekea migogoro ya familia kwa familia au jirani.
“Baada ya kufanyiwa tukio mtoto wako, jirani yako ukampeleka mahakamani jamii iliyokuzunguka itakuona wewe mbaya, mwisho wake hata kukutenga ndio mgogoro unapokua,”aliongeza.
Hata hivyo aliwataka washiriki wenzake kuwa mabalozi kwa vijana, ili viashiria vya uvunjifu wa amani visiwepo na vikitokea kuanza kuvizima mapema.
Mkurugenzi wa Taasisi ya KUKHAWA Pemba, Hafidhi Abdi Saidi alisema suala la amani sio la mtu mmoja au taasisi, bali linagusa kila mtu kwenye jamii, kwani kumekua na migogoro mingi ya mirathi na ardhi, hali inayoweza kupelekea uvunjifu wa amani.
Afisa Vijana Wilaya ya Chake Chake Stara Khamis Ali, alisema lengo la baraza la vijana ni kuwaweka pamoja vijana na kuwahimiza juu ya umuhimu wa utunzaji wa amani.
Mhadhiri kutoka SUZA Dkt.Said Mohd Khamis, alisema bado vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi, tayari serikali na wadau wa maendeleo wamekuwa mstari wa mbele katika kuzitatua hatua kwa hatua.
Mratibu wa CYD Ali Shabani, alisema CYD itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha vijana wanapatiwa elimu mbali mbali.
Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Pemba Ali Mussa Bakar, alisema suala la amani linamgusa kila mtu, hivyo vijana wanapasw akuwa mabalozi wazuri katika utunzaji wa amani hiyo na kutokua chanzo cha uvunjifu wa amani.
MWISHO