(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)
NA ZUHURA JUMA, PEMBA
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya sekta ya elimu, ili kuhakikisha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kinaongezeka nchini.
Aliyasema hayo wakati akifungua skuli ya sekondari Makangale Wilaya ya Micheweni ambayo imejengwa kwa fedha za uviko 19, ikiwa ni katika shamra shamra za kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema kuwa, mwaka 2022 Serikali ilitenga shilingi bilioni 68 kwa lengo la kuimarisha sekta ya elimu ili kuongeza kiwango Cha ufaulu kwa wanafunzi, hivyo wataendeleza juhudi hizo ambapo mwaka 2023 jumla ya shilingi bilioni 100 zitatengwa kwa ajili ya kuimarisha.
“Tulikaa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na kuwataka wanieleze kitu ambacho kitabadilisha kiwango cha elimu, ambapo walisema kuna haja ya kuongezwa madarasa, vifaa pamoja na walimu, yote tumeshaanza kuyatekeleza kwa kiasi kikubwa”, alisema Dk. Mwinyi.
Rais huyo alieleza kuwa, ahadi ya Wizara hiyo kwake baada ya kuimarisha mambo hayo matatu ni kuongeza kiwango cha ufaulu ifikapo mwaka 2025, hivyo aliwaomba waitimize ahadi hiyo kwani Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wanafunzi na walimu.
Alisema kuwa, ujenzi wa skuli hizo utasaidia wanafunzi kuingia wakati mmoja pamoja na kupunguza mrundikano, ambapo lengo lao ni darasa moja kuingia wanafunzi wasiozidi 45.
Aidha Dk. Mwinyi alisema kuwa, wataendelea kutoa ajira za kutosha pamoja na kuboresha maslahi ya walimu, ili waongeze ari ya kufundisha, jambo ambalo litasaidia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.
Dk. Mwinyi aliwapongeza wananchi wa Makangale kwa ushirikiano wao waliouonesha wakati wa ujenzi huo, na kuwataka kuwahamasisha watoto wao kusoma kwa bidii ili wafaulu vizuri katika masomo yao.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Leila Mohamed Mussa alisema, Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Mwinyi inafanya jitihada za makusudi kuhakikisha elimu inaimarika na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.
Alifahamisha kuwa, katika kufanikisha hilo, tayari wameshatekeleza miradi 45 kwa Zanzibar ambapo kwa Mkoa wa Kaskazini Pemba tayari wameshajenga skuli tisa, jambo ambalo litasaidia sana kupunguza msongomano wa wanafunzi madarasani.
“Ili kuona kwamba wanafunzi wanasoma katika mazingira rafiki, Serikali inaendelea kujenga skuli za kisasa, kuongeza madarasa, kufanyiwa ukarabati skuli za zamani na kuweka vifaa, tunaamini kwamba hiyo itawafanya wanafunzi wasome kwa bidii na kufaulu vizuri”, alisema Waziri.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alisema, wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanayatekeleza yale yaliyokusudiwa na Serikali, hivyo wanasimamia miradi yote ili kumalizika kwa wakati na kuwa na kiwango kinachotakiwa.
“Mhe: Rais nakuahidi nitasimamia hili kuhakikisha wanafunzi wanafaulu vizuri katika masomo yao”, alisema Mkuu huyo.
Akiwasilisha taarifa ya kitaalamu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar alisema, skuli hiyo ya Sekondari Makangale ina vyumba 21 vya kusomea, vyoo 20, stoo moja ofisi tatu za walimu na ofisi moja ya mwalimu mkuu.
“Sasa darasa moja litakuwa na wanafunzi si zaidi ya 45, hii ni faraja kwetu kwa sababu hapo awali darasa moja lilikuwa na wastani wa wanafunzi 89 ambapo ilikuwa ni changamoto kubwa inayopunguza ufanisi kwa wanafunzi”, alisema Naibu huyo.
Skuli hiyo ya gorofa imegharimu shilingi 2,529,262,408 ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1890.
MWISHO.