Monday, November 25

SMZ itaendelea kujenga Hospital mbali mbali ili huduma zote za afya zipatikane visiwani Zanzibar-Dk Mwinyi.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kujenga hospitali mbali mbali, ili huduma zote za afya zipatikane visiwani Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya kuzindua hospitali ya Wilaya Micheweni ikiwa ni katika shamra shamra za kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Mwinyi alisema hospitali hiyo ya Wilaya ina huduma zote muhimu ambazo wanazihitaji.
Alisema kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za kiafya na ndio maana wameamua kujenga hospitali za Wilaya na vituo vya afya, ili kuimarisha huduma hizo kwa wananchi.
“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora, hivyo tumeshajenga hospitali za Wilaya na itakapofika mwaka 2025 matarajio yetu ni kwamba tutakuwa tumeshakamilisha hospitali za Mkoa pamoja na hospitali ya Taifa itakayojengwa Binguni Unguja, hii itasaidia sana huduma zote kupatikana ndani ya Zanzibar”, alisema Dk. Mwinyi.
Dk. Mwinyi alieleza kuwa, hakuna mtu yeyote ambae atakwenda katika hospitali hiyo na akakosa huduma, kwani tayari kuna vifaa vya kutosha na vya kisasa vinavyotumika kwa huduma mbali mbali.
“Tumeanza na kuruhusu sekta binafsi kutoa huduma, hivyo maabara tuliyonayo hapa itaendeshwa na sekta binafsi, hivyo hakutakuwa na sababu ya kukokosekana kwa huduma katika hospitali hii, haya ndio matunda ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar, tunajvunia sana”, alifafanua.
Aidha aliwataka madaktari, wauguzi na watoa huduma wengine wa afya kutoa huduma ya hali ya juu sambamba na kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa, hali ambayo itawapa faraja wananchi watakaofika katika hospitali hiyo.
“Serikali tayari imeshaimarisha maslahi yenu, hivyo mutoe huduma ipasavyo, pia mnapohudumia wagonjwa muwe na lugha nzuri, hii humfanya ajisikie unafuu wakati anapofika pale”, alisema Rais Mwinyi.
Dk. Mwinyi aliwapongeza wananchi kwa ushirikiano wao wanaouonesha katika kuijenga nchi na kuwataka kuendelea kudumisha amani kwani ndio msingi wa Maendeleo nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui alisema, hospitali hizo za Wilaya zilizojengwa zitaleta manufaa makubwa kwa jamii, kwani zitawasaidia watu kupata matibabu mbali mbali
“Rais wetu alituambia kuwa anataka aone mabadiliko katika sekta ya Afya, hivyo kwa jitihada zake hizo Wizara imeshajenga hospitali za Wilaya na tutaendelea kujenga za Mkoa, lengo ni kuhakikisha huduma zinaimarika”, alisema Waziri huyo.
Alisema kuwa, kazi kubwa imeshafanyika katika kujenga hospitali hiyo na kwa sasa wanaangalia namna bora ya kutoa huduma na kuhakikisha zinamfikia kila mtu bila ya ubaguzi.
Akisoma taarifa ya kitaalamu Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dk. Amour Mohamed Suleiman alifafanua kuwa, jengo hilo limegharimu shilingi bilioni 6,835,878,878, ambapo kwa sasa ina uwezo wa kulaza wagonjwa 160 ikilingalinshwa na hospitali ya zamani ambayo walikuwa wanalaza wagonjwa 60 tu.
Alisema kuwa, kuna huduma mpya ambazo zimeongezeka ikiwa ni pomoja na ICU, huduma ya dharura na huduma ya ICT ambazo zitasaidia katika kuimarisha huduma za afya.
Nae Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alisema, watasimamia kwa vitendo ili kuhakikisha usafi unaimarishwa pamoja na kutoa huduma bora.
Aliwataka watendaji hao kutekeleza wajibu wao, ili wananchi wapate huduma bora, kwani afya ni muhimu katika maisha ya binadamu.
Hospitali hiyo ni moja kati ya hospitali kumi za Wilaya zilizojengwa Zanzibar, ambapo lengo ni kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.
           MWISHO.