Thursday, January 16

BKN SUPA SULUHISHO LA WAKULIMA WA MPUNGA VISIWANI ZANZIBAR.

NA MCHANGA HAROUB.

Wakulima wa mpunga wa kilimo cha juu Visiwani Zanzibar wameshauriwa kutumia mbegu ya mpunga ya BKN SUPA kwani ndio mbegu bora inayohimili mabadiliko ya Tabia nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mfunzo ya kuripoti habari za utafiti na ubunifu huko ofisi za mtakwimu Mkuu Mazizini Unguja, mtafiti wa mazao ya kilimo kutoka kituo cha utafiti Kizimbani Salum Fakih Hamad amesema mbegu ya mpunga ya BKN SUPA imefanyiwa utafiti wa kina na kuonekana kustawi vizuri katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.

Salum ameendelea kusema mbegu hiyo ina uwezo wa kuzalisha tani elfu tatu kwa kila hekta na inakomaa ndani ya siku tisini na tano tuu kitu ambacho kina mpelekea mkulima kulima na kuvuna mara tatu kwa mwaka.

Mtafiti huyo amesema kwamba kituo cha utafiti wa kilimo kimefanya utafiti wa mbegu takriban sita na kugundua kwamba mbegu ya BKN SUPA ndio yenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi kitu ambacho kimeweza kuwasaidia wakulima wa Zanzibar kupata mazao ya kutosha na kuelekea kulima kibiashara ili Zanzibar iweze kujitegemea kwa chakula.

Takriban 80% ya wakulima wa mpunga  Zanzibar wanategemea mvua ambapo kwa sasa hazinyeshi kama kawaida kutokana na mabadiliko ya Tabia Nchi kitu ambacho kinapelekea kukosekana kwa mazao ya kutosha kwa upande wa kilimo cha mpunga na kusababisha wakulima kukata tamaa, alisema Salum.

Utafiti huo wa mbegu ya mpunga umefanywa katika mabonde ya Kibokwa,Kilombero,Muyuni,Cheju,Kizimbani na Mahonda kwa upande wa Unguja na Chanjaani,Konde,Kiongweni,Mchanga Mdogo na Pujini kwa upande wa kisiwani Pemba,ambapo ulifanywa ndani ya misimu miwili ya mwaka 2016 – 2017 na 2017 – 2018.

Katika hatua nyengine Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Zanzibar Dk Rahma Salum Mahfoudh amewataka waandishi wa habari Visiwani Zanzibar kufanya kazi kwa karibu na watafiti ili kusaidia kutangaza matokeo ya tafiti zinazofanywa kwa maslahi ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Tume ya Mipango Zanzibar kwa kushirikiana na UNICEF pamoja na shirika la ESRF imeandaa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari wa Zanzibar ya kuwajengea uwezo wa kutangaza taarifa za kiutafiti ili ziweze kueleweka na kufanyiwa kazi kama inavyokusudiwa.

MWISHO