Monday, November 25

Azma ya kuifungua Pemba kiuchumi imeanza : Dk Mwinyi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema azma yake ya kuifungua Pemba kiuchumi na kuifanya kuwa kituo mahsusi cha uwekezaji sasa inakaribia na kueleza kuwa hatua za utekelezaji wake zimeanza rasmi.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye hafla ya kushuhudia utiaji wa saini wa makubalino ya Ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Pemba baina ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na Uongozi wa Kampuni ya Propav kutoka  Brazil pamoja na Kampuni ya Mecco ya Tanzania, hafla iliyofanyika Ikulu, Zanzibar.
Alisema ni lazima Pemba kuifungua kwa kujengwa miundombinu ya kisasa ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa ndege pamoja na kuimarishwa kwa bandari na ujenzi wa barabara.
Kwa upande wa kuimarisha miundombinu ya bandari Dk. Mwinyi alisema tayari kazi za ujenzi wa bandari ya Mkoani imeanza na inaendelea vizuri na ujenzi wa bandari ya Shumba tayari umekabidhiwa kwa mkandarasi wake.
Akizungumzia ujenzi wa barabara kisiwani humo Dk. Mwinyi alieleza mkataba huo pia utajumuisha ujenzi wa barabara kutoka Chake Chake hadi Mkoani.
Aidha, aliitaka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kusimamia kwa karibu utekelezaji wa ujenzi wa miradi hiyo pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara kwenye maeneo ya uwekezaji Micheweni, Pemba.
Naye Balozi wa Uingereza nchini, David Concar alisema anaunga mkono juhudi za maendeleo yanayofanywa na serikali za SMZ na SMT na kwamba Uingereza ni mshiriki wa muda mrefu kwa mataifa mawili hayo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohamed alieleza mkataba wa ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba utajumuisha awamu mbili tofauti ambapo awamu ya kwanza utajumuisha ujenzi wa jengo la abiria lenye ukubwa wa mita za mraba 9170 pamoja na ujenzi wa njia ya kurukia ndege yenye urefu wa  mita 2510 na upana wa mita 25.
Alisema katika hatua za awali za ujenzi huo utakamilisha huduma zote muhimu za kuufanya uwanja huo kuwa na hadhi ya kimataifa kwa mujibu wa maelekezo ya Shirika la kimataifa la huduma za usafiri wa anga duniani (ICAO) sambamba na kuruhusu kutua ndege za kimataifa aina ya 737-800 zenye uwezo wakubeba hadi abiria 189.
Aliongeza kuwa hadi kukamilika kwake uwanja utakua na uwezo wa kuwahudumia abiria 750,000 kwa mwaka kutoka abiria 45,000 waliokua wakihudumiwa awali.
Alieleza katika awamu ya kwanza ya ujenzi huo, utakua na uwezo wa kuchukua abiria 330,000 kwa mwaka ambapo kwasasa unahudunia zaidi ya abiria laki moja kutoka na ufinyu wa uwanya wasasa.
Dk. Khalid alieleza makataba huo pia utajumisha Ujenzi wa kilomita 43 za barabara kutoka Chake Chake – Mkoani, ujenzi wa kilomita 48 za barabara kutoka Fumba – Kisauni na ujenzi wa kilomita 12 za barabara kutoka Tunguu hadi Makunduchi.
Naye mwakilishi wa Kampuni ya Propav ya Brazil, Bw. Leandro Motta alisema kukamilika kwa ujenzi huo kutaifungua Pemba kijamii na maendeleo kutokana na sera yake ya uchumi wa Buluu kutaimarisha maendeleo na utalii.
Hafla ya utiwaji wa saini wa makubalino ya Ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Pemba baina ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na Uongozi wa Kampuni ya Propav kutoka  Brazil pamoja na Kampuni ya Mecco ya Tanzania ulishuhudiwa pia na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiwemo Makamo wa kwanza na Wapili wa Zanzibar, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Waziri wa Fedha na Mipango, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu kiongozi, Wajumbe wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Ardhi, Mawasiliano na Nishati, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Makatibu na manaibu  makatibu wakuu wa serikali ya Zanzibar, Mufti mkuu wa Zanzibar, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wageni wengine.