Friday, January 17

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi Azindua Michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa Mchezo wa Netiboli Gymkhana

NA MWAJUMA JUMA

MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi amewataka wanamichezo kutoridhika na viwango walivyofikia, waongeze bidii ili kuwa na viwango vya umahiri.
Mama Mariam aliyaeleza hayo wakati wa uzinduzi wa michuano ya kombe la mapinduzi kwa mpira wa netiboli huko Gymkhana Mjini Zanzibar.
Ă€lisema anajua kwamba Michezo ni afya, burudani, urafiki, nidhamu lakini Katika dunia wanayoishi Sasa michezo ni ajira yenye malipo na ujira mkubwa.
“Sote ni mashahidi, tunasoma, tunasikia, tunajionea namna wanamichezo mbali mbali waliofikia viwango vikubwa wanavyolipwa mamilioni ya fedha na wachezaji mahiri Leo hii duniani ni matajiri wakubwa na mabilionea kutokana na ujira mkubwa wanaolipwa”, alisema .
Hivyo alisema ni vyema wakajiuliza wao kama wanamichezo wanakwama wapi kufikia viwango hivyo na kusema kwamba ni kuwa baadhi yao hawajawa na dhamira ya kweli ya kutambuwa kuwa michezo ni ajira.
Hata hivyo alisema ni wajibu wa jamii ya wanamichezo wote nchini kutafakari kuweka malengo na kuamuwa kwenda kwenye viwango vya juu zaidi vya kimataifa .
“Tufikie pahali nchi yetu iwe na wanamichezo wanaowika katika majukwaa ya kimataifa kwa fani zote, tujiulize wale waliofikia huko wana nini na kwa namna gani, kinachohitajika hapa, ni nia, malengo na jitihada na ninaamini kabisa uwezo munao”, alisema.
Sambamba na hayo alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa umuhimu mkubwa katika sekta ya michezo nchini na kwa kutihibitisha Hilo imeunda Wizara ya kushughulikia michezo ili kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta hiyo .
Alisema Serikali yao inafanya mengi katika kuboresha michezo nchini ikiwa ni pamoja na kujenga na kuboresha miundombinu ya viwanja mbali mbali vya michezo na ipo tayari kutoa ushirukiano wa wanamichezo mbali mbali ili kuhakikisha wanafanya vizuri ndani na nje ya Zanzibar.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab amesema lengo la mashindano hayo pamoja na kuwa wanaibuwa vipaji lakini pia wanaunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha na kukuza michezo nchini.
Aidha alisema mashindano hayo yameandaliwa kuungana na wananchi wote kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ambayo kilele chake ni Januari 12.
Mapema Katibu Mkuu wa Chama Cha Netiboli Zanzibar (CHANEZA), Said Ali Mansab alisema mashindano hayo ni kiunganishi baina ya wachezaji na viongozi katika kupeleka mbele gurudumu la michezo Zanzibar .
Hata hivyo alisema mashindano hayo ni moja ya mshindano ambayo husaidia kupata timu ya Taifa ya Zanzibar na yenye ushindani.
Jumla ya timu saba zinashiriki michuano hiyo zote za wanawake ambazo ni KVZ, Mafunzo, Zimamoto, Warriors, The Talent, Bandari na Afya .