Friday, January 17

Dk Mwinyi aahidi kushirikiana na vijana kuijenga nchi

 

MAKAMO Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaahidi vijana kushirikiana nao katika kufanyana kazi za ujenzi wa maendeleo ya nchi.

Alisema vijna ni nguzo muhimu katika kusukuma mbele maendeleo ya uchumi wa taifa ndio sababu ya serikali za SMZ na SMT  zimeteua vijana wengi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ili kuwapatia uzoefu wa kuongoza nchi yao kwa uwezo na weledi wa kuchapa kazi na kuijenga nchi kiuchumi na maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo huko viwanja vya Mnara wa Kisonge, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi wakati wa shehere za uzinduzi wa matembezi ya vijana ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kilele chake ni Januari 12, mwaka huu.

Dk. Mwinyi alieleza kuwa vijana wana nafasi kubwa ya kutumikia taifa lao na kuliletea maendeleo sambamba na kuwaasa vijana hao kwamba wanapaswa kujitambua kwa kujiweka imara ili kufanikisha malengo ya ukombozi wa kweli kwenye jamii zao.

“Kama nyote mnafahamu kwamba Nchi yetu ilipata uhuru tarehe 12 Januari mwaka 1964, kwa njia ya kufanya Mapinduzi ambayo kwa kiasi kikubwa yaliendeshwa na vijana wakati huo” alithimlia Dk. Mwinyi.

Aidha, aliwaeleza kwamba kazi iliyo mbele yao ni kujenga nchi baada ya kupata uhuru pamoja na kuwakumbusha kwenye suala muhimu la kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamamo katika jamii ambayo ndio chachu ya maendeleo ya nchi ilipofikia

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwashauri vijana hao kushikamana na kusaidiana katika kutafuta na kujitengenezea ajira ili kujitatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kujitafutia maenedeo.

“Tambueni Serikali yenu ya awamu ya nane inaunga  mkono juhudi zenu zinazofanikisha  kuondoa changamoto za ajira nchini na kujiletea maendeleo katika jamii zenu” alitanabahisha Dk. Mwinyi.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuweka mazingira wezeshi kwa makundi yote ya vijana kwa lengo la kuwapatia fursa za ajira vijana kwa namna yoyote iliyobora na sahihi kwa mijibu wa sheria na taratibu za nchi.

Akizungumzia suala la vikundi vya maendeleo ya vijana, Dk. Mwinyi aliwaahidi kwamba serikali itawapatia mikopo kwaaajili ya kuendeleza juhudi zao za maendeleo na kueleza kuwa atazisimamia mamlaka husika ili ziwape vijana kipaumbele kwenye wepesi wa kupata mikopo  ili wanufaike na mipango ya serikali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Alisema serikali zote mbili za  SMZ na SMT zimeweka mifumo mizuri ya kuwawezesha vijana kupata ajira kupitia sekta za umma na binafsi, mifumo aliyoieleza kwamba imewaepusha vijana kuepukana na mambo maovu, kuwajenga vijana kuwa wazalendo raia wema kwa taifa lao na kuwafanya vijana kujiona fahari kufanya kazi za kujitolea katika kujiletea maeneleo ya nchi yao.

“Nyinyi Umoja wa vijana wa CCM mna dhima kubwa ya kuwaongoza na kuwaelekeza vijana wenzenu kuwa na maono hayo” DK. Mwinyi aliwashauri vijana hao.

Dk. Mwinyi aliwataka vijana kutumia mbinu tofauti kwa kuwafundisha vijana wenzao jinsi ya kuwa wazaleo kwa kujiepusha kujiingiza kwenye vitendo viovu ikiwemo matumizi ya dawa za kulenya, udhalilishaji  na vitendo vyote vya uvunjifu wa sheria za nchi.

Akizungmza kwenye hafla hiyo, Mlezi wa Umoja wa Vijana wa CCM, Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Maryam Mwinyi aliwaasa vijana hayo kuzidisha nidhamu kwenye kutumikia chama chao na kuwaomba kuendelea kuisemea vizuri serikali yao na juhudi za maendeleo zinazofanywa na chama chao.

Aidha, akiwaasa kuendelea kuchukua tahadahari kwenye jamii zao kwani bado ugonjwa wa korona upo duniani na Zanzibar ni kisiwa chenye mchanganyiko wa watu kutoka mataifa mengi hiyo aliwaomba vijana hao kushajihisha umuhimu wa chanjo ili kujinusuru sambamba na kuwaasa kuendelea kupiga vita dhidi ya udhalilishaji wa wanawake na watoto ilikujenga jamii iliyo bora.

Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Abdalla Juma Mabodi aliwaasa vijana hao kuhubiri maridhiano ya nchi ili kudumisha jamii yenye umoja na mshikamano katika kujenga taifa lenye maendeleo ya amani na utulivu.

Alisema Chama Cha mapinduzi daima kinaungamkono juhudi za serikali na lazima kifuate maagizo na maono ya viongozi wa nchi.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM taifa, Mjumbe wa Kamati ya Halmashauri kuu taifa, Komredi Muhammed Ali Kawaida, alisema vijana watatumia fursa iliyotolewa na serikali ya kufanya mikutano ya hadhara kwa kuyasemea mazuri yote zanayofanywa na serikali za SMZ na SMT na kwamba chama chao cha CCM kitaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali mbili hizo.

Matembezi hayo ya vijana yataendelea kwa siku saba mfululizo yenye kauli mbiu yake “Uchumi wa buluu kwa maendeleo ya viwanda, vijana tuachangamkie fursa” yanajumuisha shughuli mbambali za ujenzi wa taifa.