Friday, February 28

SMZ na SMT zimejipanga vizuri kuhakikisha changamoto zilizopo katika sekta ya afya zinapatiwa ufumbuzi- DK Mpango

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Isdor Mpango, akikunjua kitambaa kuashiria ufunguzi wa hospitali ya Kendwa shehia ya Kendwa jimbo la Kiwani, akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera Uratibu na baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma, wakiwa na watendaji wengine ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar.
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Isdor Mapango, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa hospital;li ya Kendwa shehia ya kendwa jimbo la Kiwani, akiwa na viongozi mbali mbali wa serikali na Chama cha Mapinduzi, wakiwa na watendaji wengine ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Isdor Mpango, akipata maelezo ya chumba cha kujifunguliwa wazazi katika hospitali ya Kendwa shenhia ya Kendwa jimbo la Kiwani, kutoka kwa Mganga mkuu wa Wilaya ya Mkoani Dk.Ali Omar, wakiwa na watendaji wengine ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Isdor Mpango, akicheza wimbo maalumu uliokuwa ukiimbwa na wanafunzi wa skuli ya Msingi Kendwa jimbo la Kiwani, katika hafla ya ufunguzi wa Hospitali ya Kendwa Shehia ya Kendwa, wakiwa na watendaji wengine ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar
MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzanzibar (TASAF) Ledslaus Mwamanga , akisoma taarifa ya ujenzi wa hospitali ya Kendwa kupitia mfuko huo wa kaya masikini shehia ya Kendwa,katika hafla ya ufunguzi wakiwa na watendaji wengine ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Isdor Mpango, akizungumza na wananchi na watoa huduma za afya katika Hospitali ya Kendwa shehia ya Kendwa Jimbo la Kiwani, mara baada ya kuifungua kwa Hospitali hiyo wakiwa na watendaji wengine ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Isdor Mpango, akiwasalimia wananchi wa shehia ya Kendwa jimbo la Kiwani, mara baada ya kufungua Hospitali ya Kendwa iliyojengwa kupitia TASAF, wakiwa na watendaji wengine ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar

(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

NA HANIFA SALIM, PEMBA

MAKAMO wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk, Philip Isdor Mpango, amewahakikishia wananchi kwamba Serikali zote mbili zimejipanga vizuri kuhakikisha changamoto zilizopo katika sekta ya afya zinapatiwa ufumbuzi.

Alisema, licha ya mafanikio makubwa ambayo Serikali imepiga hatua lakini inaeleweka kwamba sekta ya afya bado inakabiliwa changamoto mbali mbali ikiwemo upungufu wa vifaa tiba, uhaba wa wafanyakazi pamoja na miondombinu.

Dk, Mpango alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo katika hatua za mwisho kuhakikisha wananchi wanapata huduma kupitia mfuko wa huduma za afya, vile vile kuna mpango mahususi wa kuongeza wafanyakazi katika vituo na kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa wakati.

Aliyasema hayo katika ufunguzi wa kituo cha Afya Daraja la II Kendwa Jimbo la Kiwani, Wilaya ya Mkoani Kisiwani Pemba kilichojengwa kupitia fedha za Mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania TASAF ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema, kabla ya Mapinduzi huduma za Afya zilikua zikitolewa kwa matabaka na watu maalumu ambapo watu wengi waliachwa na kukosa huduma jambo ambalo lilisababisha madhara makubwa na hata kupelekea vifo kwa wananchi wanyonge.

Alifahamisha, kabla ya Mapinduzi Zanzibar kulikua na vituo 44, lakini baada ya Mapinduzi hadi kufika mwaka 2021 vituo vya afya vya serikali vimeongezeka na kufikia 1710,000 ambapo, kwa upande wa Unguja vikiwa 99 na Pemba 72.

Dk, Mpango alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuweka juhudi kubwa katika kuimarisha huduma za kijamii kwa wananchi wake ikiwemo sekta ya afya, kwani licha mafanikio ambayo yapo lakini sekta hiyo inafahamika kwamba inakabiliwa na changamoto nyengine mbali mbali.

“Kituo hichi kitawapunguzia sana wananchi na hasa akina mama kutembea masafa marefu kufuata huduma za afya, ni dhahiri kituo hichi kitakua ni mkombozi wa shehia ya Kendwa, kiwani, Mtangani na nyengine jirani”, alisema.

Aidha aliwasihi wale ambao watapata fursa za kuishi katika nyumba za madaktari kuzitunza vizuri ili kuepusha gharama za matengenezo yasiokua ya lazima, pamoja na kuwataka madaktari na wananchi kupanda miti na kutunza mazingira yaliyozunguka kituo hicho ili kiweze kudumu kwa muda mrefu.

Waziri wa Nchi OMPRSUBLW Zanzibar Hamza Hassan Juma alisema, miongoni mwa faida ambayo Wazanzibari wanaipata sasahivi kutokana na muungano uliopo ni kupata fedha ambayo imekuja kwenye Serikali ya Mapinduzi ambayo imetekeleza miradi mingi ikiwemo barabara, viwanja vya ndege nahospitali.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh alisema, malengo yao wizara ni kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi, kwani tayari wameshaeka baadhi ya vifaa katika hospitali hiyo na karibuni wataondosha changamoto ya upungufu wa dawa na vipimo ndani ya hospitali zote.

Akitoa salamu za Mkoa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa kuendelea kuboresha huduma mbali mbali za kijamii ndani ya Mkoa huo ambazo wananchi wanazihitajia.

Akisoma taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu OMPRSUBLW Zanzibar Dk, Islam Seif Salim alisema, mradi huo wa kituo cha Afya Daraja la II Kendwa umegharimu zaidi ya shilingi Milioni 500, ambao umefadhiliwa na mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania TASAF.

Akitoa salamu za Makao Makuu ya TASAF Tanzania Mkurugenzi Mtendaji Ladislaus Mwamanga alisema, TASAF ni chombo cha muungano ambacho kinatekeleza shughuli zake vijiji, mitaa na shehia zote za Tanzania.

                            MWISHO.