Thursday, January 16

Soraga azindua mradi wa nishati ya umeme wa jua, visiwa vya Njao na Kokota Wilaya ya Wete.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mudrik Ramadhan Soraga amewataka wananchi kisiwani Pemba kuunga mkono juhudi zinazofanywa  Serikali  ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuwaletea  maendeleo endelevu.

Aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wanachi wa visiwa vya Njao na Kokota Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, katika uzinduzi wa mradi wa nishati ya umeme wa jua, ikiwa ni katika shamra shamra za kuelekea maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar.

Alieleza  kuwa, Serikali ya awamu ya nane inadhamira kubwa ya kutimiza azma yake ya kuwakomboa wananchi na umaskini, hivyo kila mmoja anawajibu wa kuunga mkono juhudi hizo, ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana.

“Serikali inawasogezea wananchi huduma mbali mbali ikiwemo hii ya umeme tuliozindua leo, hii ndio adhma ya Mapinduzi yetu ya Zanzibar kwamba kila mwananchi apate huduma muhimu”, alisema Waziri huyo.

Alifahamisha kuwa, kuwepo kwa huduma ya umeme ni muhimu katika kukuza kipato cha wananchi, hivyo watumie fursa hiyo kuona kwamba uchumi wao unaimarika, jambo ambalo litasaidia kupunguza umasikini.

Aidha Waziri huyo alisema kuwa, Serikali imetumia fedha nyingi kuwafikishia wananchi hao huduma ya umeme na kuwataka wananchi
wasihujumu miundombinu ili kuweza kuwanufaisha zaidi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alisema kuwa, uwekwaji wa umeme katika visiwa hivyo, ni kazi ya kizalendo ya kuimarisha maisha ya wananchi ambayo itasaidia katika kukuza uchumi wa wakaazi wa visiwa hivyo.

“Tunaamini kwamba mumeanza kunufaika na huduma hii na mtaendelea kunufaika, kwa sababu mutaanza kutatua zile changamoto ambazo zilikuwa zikisababishwa na ukosefu wa umeme, ni faraja kubwa kwetu”, alisema Mkuu huyo.

Nae Balozi wa Norway nchini Tanzania ambae wamefadhili mradi huo Elizabeth Jacobsen, aliwataka wananchi hao kuitunza na kuilinda
miundombinu ya nishati ya umeme wa jua, ili itumike kwa muda mrefu.

“Tunalishukuru shirika la ZECCO kwa kufanikisha mradi huu, ni faraja sana kwetu na kwa wananchi hawa, hivyo tutaendelea kushirikiana na Serikali ili kusaidia upatikanaji wa huduma muhimu katika nchii”, alieleza Balozi huyo.

Akisoma yaarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Joseph John Kilangi alisema, kukamilika kwa uwekwaji wa umeme kwa visiwa vya Njao na Kakota vimekalisha idadi ya visiwa vyote kisiwani Pemba kwa upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Alifafanua kuwa, visiwa vya Kokota na Njao vina wananchi 817, ambapo wananchi 156 wameshaomba kuungiwa huku wananchi 139 tayari wameshaungiwa na wanaendelea kutumia huduma hiyo.

Katibu Mkuu huyo aliwataka wananchi hao endapo kutatokezea hitilafunyeyote katika huduma hiyo, wasisite kuwapa taarifa ZECCO na
kuacha tabia ya kuchukua mafunzo wa mitaani, kwani wanaweza kuwasababishi matatizo.

Mradi huo wa nishati ya umeme wa jua katika visiwa vya Kokota na Njao umegharimu dola za kimarekani laki 458,205 ambao umefikishwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana pamoja na Serikali ya Norway.

                                    MWISHO.