Wednesday, January 15

MWAKILISHI apiga jeki Tawi la CCM Mkoroshini

NA ABDI SULEIMAN.

MWAKILISHI wa Jimbo la Wawi Bakar Hamad Bakar, amekabidhi mlango wa geti wa duka, kwa Tawi la CCM Mkoroshini ili tawi hilo liweza kuanzisha kitega uchumi ambacho kitawasaidia katika harakati zao ndogo ndogo.

Alisema atahakikisha geti hilo linawekwa na mlango huo unaanza kufanya kazi baada ya kukamilika kwa matengenezo ya ndani ikiwemo uwekaji wa silingi bodi, umeme na sakafu.

Hayo aliyaeleza wakati alipokua akizungumza na vijana wa tawi hilo, juu ya mikakati ya kutaka matawi ya jimbo hilo kuanzisha vitega uchumi vyao.

Alisema Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi, anahitaji sasa chama kiweze kujitegemea kiuchumi, na ili kiweze kujitegemea lazima waanze kwenye matawi ili kufikia huko.

“Sisi katika jimbo letu, matawi yetu yanayohi sehemu za kuekeza vitega uchumi, ikiwemo tawi la Mkoroshoni na leo tupo katika kukabidhi mlango huu wa geti,”alisema.

Alisema vijana wenyewe wataweza kufungua duka au kukodisha au kuuza vitu wanavyotaka, mwisho wa siku tawi linapata faida na fedha zinawasaidia katika shuhuli nyingen ikiwemo kulipia umeme.

Alisema athakikisha changamoto ya umeme iliyopo ndani ya mlango huo wa duka, atahakikisha anaikamilisha kwa wakati na matokeo yakiwa mazuri kuna uwezekano wakujengwa kwa duka jengine wakati kiwanja kipo.

“Sehemu hii hapa ikiwa mafanikio yamepatikana na tunaona tija yake, basi tutajenge mlango mwengine wa kitega uchumi na chama kiweze kunufaika nacho,”alisema.

Hata hivyo aliwataka wanachama wa tawi hilo la CCM Mkoroshoni, kuhakikisha wanatimiza malengo yao katika chama pamoja na kulinda msaada huo.

Mwenyekiti wa tawi la ccm Mkoroshoni Salim Juma Ali, alimshukuru mwakilishi huyo kwa kuwapatia msaada huo wa mlango, ambao utawafanya waweze kuwa na kitega uchumi katika tawi lao la CCM.

Alisema vijana wataweza kujiendeleza wao kiuchumi, pamoja na kukiendeleza chama kwa kukipatia wanachama na kukisaidia chama na sio kukiangusha chama.

Naye mlezi wa Tawi hilo la CCM Mkoroshoni, Khamis Iddi Songoro alimpongeza mwakilishi huyo kwa kuendelea kuwasaidia vijana wenzake, kwa kuhakikisha anaimarisha matawi ya ccm yaliyomo ndani ya jimbo hilo.

Alisema vijana ndio nguzo muhimu kwenye CCM hivyo hawana budi wazee kuwa karibu na vijana na kuwafahamisha malengo mahususi na dhamira nzima ya ccm katika kuleta umoja na mshikamano.

MWISHO