NA HAJI NASSOR, PEMBA
OFISA Mdhamini Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Thabit Othman Abdalla, amewataka watumishi wa umma kisiwani Pemba, kutoungana na watu wengine, katika kukebehi na kudharau mipangano, sera na mikakati ya serikali, kwani kufanya hivyo ni ukiukwaji wa maadili ya kazi.
Alisema, kila mtumishi wa umma anapofanyakazi katika kitengo na idara yoyote ile, ajue kuwa anamwakilishi kiongozi wa nchi, hivyo lazima asikubali kuwa sehemu ya kuongoza mijadala ya kukibehi mwelekeo wa serikali.
Ofisa Mdhamini huyo aliyasema hayo Januari 15, 2023, ukumbi wa mikutano Baraza la mji wa Chake chake, wakati akiyafunga mafunzo ya siku tatu, kama sehemu ya uthibitishwaji wa kazi, kwa watumishi wapya wa umma, yalioendeshwa na Chuo cha Utawala wa Umma ‘IPA’.
Alisema, wapo baadhi ya watumishi wa umma kwa kule kutokujua nafasi zao, wamekuwa wakiungana au wakati mwengine kuanzisha mijadala ya kudhoofisha mikakati ya serikali.
Alieleza kuwa, kiutumishi hilo ni kosa, kwani kuajiriwa kwake katika kitengo anachofanyakazi, anamwakilishi kiongozi wa nchi, kama muajiri mkuu.
‘’Wapo watumishi wengine kwa mfano, wanakebi suala la kupanda vyakula na sera ya uchumi wa buluu, au kusema serikali haijafanya lolote, haya na mengine yanayofanana na hayo, hayafai kwa mutumishi umma,’’alisema.
Kati hatua nyingine Ofisa Mdhamini huyo, amewataka watumishi hao wakawe watumishi bora wenye kutunza sira za ofisi, matumizi sahihi ya lugha na kufanyakazi, kwa moyo wa kiuzalendo.
Hata hivyo alisema, anaamini kwa elimu walioyoipata kwa siku hizo tatu, watakuwa mfano wa kuigwa na wenzao kwa kule kuzifuata kwa vitendo sheria na kanuni za utumishi wa umma.
Akizungumza kabla ya kufungwa kwa mafunzo hayo, Mkuu wa ‘IPA’ tawi la Pemba Juma Haji Juma, alisema mafunzo hayo yamewafungulia milango watumishi hao.
‘’Moja ya faida kubwa ya mafunzo haya, mtaweza kuthibitishwa kazi, ruhusa za likizo au kwenda masomoni sasa mtakuwa na haki, na hasa baada ya ofisi zenu kuridhishwa na baadhi ya mambo,’’alieleza.
Hata hivyo Mkuu huyo wa ‘IPA’ tawi la Pemba, aliwasisitiza watumishi hao, kama wanataka kufika mbali kiutumishi, waziheshimu na kuyafanyia kazi kwa vitendo mafunzo hayo.
‘’Mafunzo haya mjue kuwa, ni sehemu ya utekelezaji wa sheria na kanuni ya utumishi wa umma ya Zanzibar ya mwaka 2014, hivyo muone thamani yake, katika kazi zenu,’’alieleza.
Mapema akiwasilisha mada ya sheria ya Utumishi wa Umma Zanzibar ya mwaka 2014, mwanasheria Suleiman Omar Makame, alisema sheria hiyo ni nzuri, ikiwa itatekelezwa kama ilivyoandikwa.
‘Kwa mfano, sheria imetoa amri ya likizo kila mwaka, na fedha zake kila baada ya miaka mitatu, lakini hata namna ya upandishwaji madaraja na haki ya matibabu kwa mtumishi wa umma,’’alieleza.
Baadhi ya watumishi hao akiwemo Abass Omar Abass wa wizara ya Habari, alisema sheria ni nzuri, ikiwa muajiri atayatekeza ipasavyo haki za muajiriwa.
Nae Wahida Kombo Khamis kutoka Baraza la mji Chake chake, alipendekeza mafunzo hayo, yashirikishe na maafisa utumishi, ili kupata ufafanuzi zaidi.
Katika mafunzo ya siku tatu, mada 10 zilijadiliwa ikiwa ni Mfuko wa Hifadhi wa Jamii Zanzibar ‘ZSSF’, sheria ya ZAECA, uzalendo na umuhimu wake kwa taifa, sheria ya Utumishi ya umma na kanuni zake pamoja na sheria ya Afya na usalama kazini.
Mwisho