Monday, November 25

MABADILIKO ya Tabianchi yanapelekea upungufu wa maji maeneo ya hifadhi na kusababisha migogoro baina ya wanyama na binaadamu.

NA ABDI SULEIMAN – BAGAMOYO.

MABADILIKO ya Tabianchi yanayoendelea kutokea katika maeneo mengi nchini Tanzania, yanapelekea upungufu wa maji maeneo ya hifadhi za wanyamapori na kupelekea migogoro baina ya wanyama na binaadamu.

Wanayama hufuata maji nje ya hifadhi zao na kuingia katika makazi ya binaadamu, hupelekea kusababisha migogoro na wakati mwengine kutokea madhara.

Akiwasilisha mada mabadiliko ya Tabinachi na bionuai Joseph Olila kutoka USAID Tuhifadhi Maliasili, kwa waandishi wa habari za Mazingira Tanzania, kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, unaotekelezwa na JET Tanzania kwa ufadhili wa shirika la misaada la watu wa Marekani (USAID).

“Changamoto zipo tatu, moja mabadiliko ya tabia nchi yanapelekea upungufu wa maji, katika maeneo wanyama wanayotegemea na kupelekea kuingia katika maeneo ya binaadamu na kusababisha migogoro baadae,”alisema.

Alisema changamoto nyengine, binaadamu wanapoteza mazao ambayo ndio tegemeo kwao, kutokana na wanyama kusogelea kupata malisho na maji, hali inayopelekea jamii kuendelea kubakia maskini kufuatia mazao yao kuharibiwa na wanyama.

Akizungumzia changamoto ya kupotea kwa bionuai, mkufunzi huyo alifahamisha kwamba, baadhi ya bionuai za viumbe vidogo vidogo kama chura na kinyonga vipo hatarini kupotea kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoikubwa tanzania.

“Viumbe hivi haviwezi kusafiri masafa marefu kutafuta mahitaji yao, mabadiliko yanapozidi baadhi ya viumbe vinaweza kupotea kwa kushindwa kuhimili mabadiliko hayo,”alisema.

Hata hivyo alisema kupotea kwa bionuai hizo, zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa taifa, kwani hivi sasa sekta ya utalii imekua na mchango mkubwa katika kuchangia pato la taifa kupotea kwake ni hasara kwa nchi,”alisema.

Katika hatua nyengine mkufunzi huyo, alishauri kuwepo kwa mipango mizuri ya matumizi ya ardhi kwa kuruhusu kuwa na maeneo  yatayoruhusu wanyama kupita kutoka eneo moja kwenda jengine. Aidha alisema kwenye mfumo wa kiekolojia kila mnyama anaumuhimu, mfano nyuki akipotea kuna madhara makubwa yanatokea hata mimea haitoweza kuzalishwa, lazima kuwaangalia wanyama hawao wasipotee.

Kwa upande wake mwandishi wa habari kutoka Tanzania Daima Janeth Jovin, alisema waandishi bado wanakazi kubwa ya kufanya ili kuwe na usimamizi mzuri wa sheria na kufanya ufuatiliaji wa hali.

“masuala yote ya uhifadhi yanapaswa kusimamiwa na taasisi moja na kuwa na sauti moja, sio kila taasisi inajihusisha na mambo ya uhifadhi hapo usawa hautokuwepo,”alisema.

Naye Mwandishi Exuperius Kachenje, alisema waandishi wanamchango mkubwa wakuelimisha jamii juu ya umuhimu wa koridoo, ili kujuwa umuhimu wa uhifadhi na kulinda hifadhi hizo.

MWISHO