Monday, November 25

Shughuli za kibinaadamu chanzo cha kupotea Shoroba

 

NA ABDI SULEIMAN- BAGAMOYO.

MENEJA ushirikishwaji wa sekta binafsi wa USAID Tuhifadhi Maliasili Dr.Eliakana Kalumanga, amesema maeneo yaliyohifadhiwa ambayo hutumiwa na wanyamapori (Shoroba), yanapaswa kuendelea kulindwa kwani hata binaadamu maeneo hayo yanawasaidia.

Alisema maeneo ya shoroba wanyama huyatumia kwa shuhuli zao za kimaisha, kwa kujipatia chakula na mambo mengine ambapo binaadamu nae hunufaika kwa asilimia kubwa.

Aliyaeleza hayo wakati alipokua akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari za Mazingira Tanzania, kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, unaotekelezwa na JET Tanzania kwa ufadhili wa shirika la misaada la watu wa Marekani (USAID) huko Bagamoyo.

Alisema shoroba zinawasaidia wanyama kupata mahitaji ya maji, malisho na hifadhi, binaadamu hupata kuni na madawa, huku akitolea mfano wananchi jamii ya wahazabi.

Aidha alifahamisha uzuri wa baadhi ya maeneo ya misitu yanavutia watalii, na yanafaida kiuchumi ikiwemo uwekezaji wa mahoteli ya kiutalii, mfano shoroba ya kwakuchinja inaunganisha hifadhi ya Burunge, Tarangire na Ziwa manyara, wananchi wanauza bidhaa za kitalii.

Hata hivyo alisema kwa sasa shoroba zinakabiliwa na changamoto kubwa, ikiwemo shuhuli za binaadamu ambazo ni endelevu hali inayofanya shoroba nyingi kuanza kupotea.

“Kwa sasa hali za shoroba zetu mbalimbali nchini si nzuri, kwa mujibu wa takwimu za serikali zipo baadhi zimepotea kabisa, kutokana na shughuli hizo za wananchi zinazofanywa kila siku, kuna haja ya kuendelea kuwaelimisha wananchi,” alisema.

Naye Meneja ufuatiliaji na Tathmini USAID Tuhifadhi Maliasi John Steven Noronha, aliwataka waandishi wa habari za Mazingira Tanzania, kuwa mstari wa mbele kuibua na kuelimisha jamii juu ya athari zitokanazo na shughuli za kibinadamu zinazofanywa ndani ya shoroba.

Alisema iwapo shoroba zitatoweka zote basi watalii hawatokuja tena Tanzania, kwani wamanyama watakosa maeneo yao ya malisho na mahitaji yao.

Hata hivyo alisema iwapo koridoo zitatoweka kutakua na athari kubwa zitapatikana, hifadhi zitakuwa kama visiwa na wanyama hawatotoka kwenye mbuga moja kwenda nyengine na kutakua na wanyama dhaifu, na ugonjwa ukiingia wanyama watatoweka.

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo alisema kumekuwa na ongezeko la wanyamapori katika baadhi ya hifadhi, jambo ambalo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na uhifadhi wa wanyamapori.

“Hata ongezeko la watalii wanaoingia nchini ni mafanikio yanayotokana na elimu ya uhifadhi wa mazingira na wanyamapori inayotolewa mara kwa mara kwa waandishi wa habari hapa nchini,” alisema.

Naye mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru alisema ni wakati sasa kwa vyombo vya habari kujikitaka katika habari za uhifadhi na utunzaji wa mazingira, ili wananchi waweze kuona umuhimu wa utunzaji wa shoroba kwa maslahi ya taifa.

Chama cha waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET) kinatekeleza mradi wa miaka mitano, USAID Tuhifadhi Maliasili kwa ufadhili wa shirika la misaada la watu wa Marekani (USAID).

MWISHO