Monday, November 25

Waandishi wa habari za Uhifadhi wa wanyamapori na Bioanuwai Tanzania, waelimishe jamii juu ya umuhimu wa shoroba.

NA ABDI SULEIMAN – BAGAMOYO.

WAANDISHI wa Habari za Uhifadhi wa wanyamapori na Bioanuwai Tanzania, wamesema wanadhima kubwa ya kuelimisha jamii, juu ya umuhimu wa kulinda na kuhifadhi shoroba za wanyamapori nchini.

Wamesema shoroba zina mchango mkubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla, kwani wanyama hupita kwenda kufuata mahitaji yao na binaadamu hutumia kwa ajili ya shuhuli zao za kijamii.

Hayo yameelewa na Mwandishi wa habari kutoka TBC na Mwanachama wa Chama cha Waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET) Swalehe Makoye, alipokua akizungumza na Zanzibarleo baada ya kumalizika kwa mafunzo ya siku mbili, yaliyoandaliwa na JET Tanzania kwa ufadhili wa shirika la USAID kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.

Alisema iwapo waandishi wa wataelimisha jamii juu ya umuhimu wa shoroba, wataweza kuona athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaathiri shuhuli za binaadamu na maisha ya wanyamapori.

“Natamani kuona Tanzania inapiga hatua katika suala la uhifadhi wa wanyamapori, waandishi wa habari tunanafasi kubwa kutumia kalamu na sauti zetu kwa kuifikisha elimu kwa jamii iliyokuwa sahihi,”alisema.

Naye Mwandishi kutoka Hope Chanel Tanzania Nyamiti Kayora, alisema mafunzo yamemjengea uwezo kwa kuelewa suala la uhifadhi, jinsi migogoro ya wanyamapori na binaadamu inavoweza kuepukika.

Alisema bado suala la mabadiliko ya tabianchi linaendelea kuathiri binaadamu na wanyamapori, kwani kila mmoja ana mahitaji yake katika ulimwengu.

“Binaadamu anahitaji maji, chakula na kuni hivi vyote vimekua vikiathiriwa na mabadiliko haya, wanyama wanao wanahitaji malisho na maji na yote yanapotea hapo ndio migogoro inapoanza sababu mabadiliko ta tbianchi,”alisema.

Aidha alisema wakati umefika wa kuandika habari zitakazoleta tija kwa jamii na serikali, kwani ulizi na uhifadhi wanyama na binaadamu zinakwenda sambamba katika dunia.

Kwa upande wake mwandishi mkongwe kwenye masuala ya uhifadhi wa wanyamapori na bionuwai Tanzania, Salome Kitomari alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa sasa, dunia inapozungumzia mabadiliko ya tabianchi, kwani Tanzania nayo ni sehemu ya nchi ambayo imeathiriwa na mabadiliko hayo.

“Tunapozungumzia mabadiliko tunazungumzia ukame na vipindi virefu mvua ambazo hazitabiriki, hata zikinyesha zinaleta madhara, upatikanaji wa maji nayo ni shida, lazima waandishi wa habari tuwe na uwelewa katika suala la mazingira ili kuelimisha jamii,”alisema Salome.

Alisema iwapo uwelewa utakuwepo wa hali ya juu, basi habari za mazingira hifadhi, mapori ya akiba, mapori tengefu, WMA zitaandikwa kwa wingi na jamii kuweza kufahamu umuhimu wake.

Aidha alisema wataalamu wa mazingira, wanasema maji ni vita vikubwa vinavyokuja, niwakati kwa waandishi kujiuliza na kuona wanaelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutunza na kulinda vyanzo vya maji, licha ya shuhuli za kilimo kuendelea kufwanya katika vyanzo hivyo.

Hata hivyo aliwashauri waandishi wa habari, wanapaswa kuelekeza nguvu katika uwandishi wa habari za uhifadhi, ili kutunza mazingira kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kinachokujwa.

Katika hatua nyengine Salome alisema, kunachangamoto za kisera na kisheria, kwa baadhi ya sheria hivyo taasisi zinazohusika na wanyamapori, maji na utalii, vizuri nyaraka hizo kusimamiwa na taasisi moja.

mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru, alisema mafunzo yamegusa kila mtu, ikiwemo uchumi wa buluu kwenye Bioanuwai, udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi yote hayo yanahusika pamoja na ushiriki wa binaadamu katika maisha na wanyamapori na viumbe hai vyote.

Hata hivyo alitaka wananchi kuelimishwa umuhimu wa uhifadhi kwa faida yake ya kiuchumi, kiutamaduni na vizazi vya sasa na vijavyo, pamoja na sera kuboreshwa ili kusaidia uhifadhi na kuhifadhi vyanzo vya maji kwa ajili ya maisha ya mwanaadamu na wanyamapori.

MWISHO