Monday, November 25

Madereva watakiwa kuwa makini wanapokua barabarani

NA ABDI SULEIMAN.

Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kusini Pemba ACP Khamis Rashid Said, amewataka madereva wa Gari za abiria Pemba, kuwa makini wanapokua barabarani, kwani ajali nyingi zimekua zikitokea na kupelekea watu kupoteza maisha na wengine wakiwa walemavu.

Alisema ajali hizo husababishwa nan ambo mbali mbali ikiwemo uzembe wa madereva hao, kwa kutokua makini na kujisahau kama wanapokua barabarani wanapaswa kushuhulia gari na sio mambo mengine.

ACP Khamis aliyaeleza hayo, kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, wakati akifungua mkutano mkuu wa Jumuiya ya wenye magari na madereva, wafanyakazi wa magari ya biashara Mkoa wa Kusini Pemba (PESTA), mkutano uliofanyika Mjini Chake Chake.

Alisema lazima madereva kuzijua barabara wanazotumia na kujua barabarani watakutana na vitu gani na gani, sambamba na kusikiliza maoni ya abiria wanayokua wanayatoa na sio kuwadharau.

“Naipongeza PESTA kwa akuamua kuunda taasisi yenu inayowakutanisha wadau mbali mbali, ili kuona mafanikio yanafikiwa na madereva kufuata sheria,”alisema.

Akitoa taarifa ya hali ya usafiri wa barabarani Mkoa wa Kusini Pemba, Katibu wa PESTA Hafidhi Mbarak Salim, alisema wamekuwa wakishuhudia ongezeko kubwa la kasi kwa vyombo vya usafiri wa barabarani, imetokana na matokeo ya kasi ya mabadiliko ya sera za kiuchumi zilizowekwa zimepelekea kukua sekta ya uchumi na kuongezeka kwa kipato cha watu.

Alisema ajali za barabarani zimekua zikisababisha kupoteza maisha ya watu, ulemavu na uharibifu wa mali na kupoteza nguvu kazi ya nchi.

“Tafiti mbali mbali zinaonyesha kuwa wastani wa asilimia 76 ya ajali zote zinatokea barabarani zinasababishwa na makosa ya binaadamu, asilimia 16 husababishwa na ubovu wa gari,”alisema.

Naye Mwenyekiti wa PESTA Amini Othman Sharif,

Kwa Upande wake Mwanasheria wa kujitegemea Halfan Amour, aliwataka madereva na makondakta wa gari za abiria, kubadilika katika utendaji wao wa kazi kwa kuijali kazi yao ipasavyo.

“Tunapokua katika kazi zetu lazima kila mtu aijali kazi yake, madereva wengi bado hawako sahihi katika kazi kwani wamekuwa wakisahau majukumu ya kazi zao,”alisema.

Naye dereva wa gari ya abiria Suleiman Mohamed Said, alisema mtu kazi yake yoyote anatakiw akuithamini kwani kuna gari aina ya Nohora 20 hadi 25 zinazokwenda mkoani zinatokana alfajiri sana na kuchukua abiria kinyume na taratibu.

Aidha aliitaka Serikali kupitia Jeshi la Polisi na Mawasiliano, kuhakikisha wanazitia mikononi gari zote aina ya Noha zinazofanya kazi za kupakia abiria na kupeleka mkoani muda wa alfajiri.

Naye afisa kutoka Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Mussa Amour Mussa, aliwataka madereva kuacha tabia ya kuzilalamikia bajaji na bodaboda, badala yake wanapaswa kuzipa mashirikianao kwani serikali imekuja na nia njema na vijana wa vyombo hivyo.

Kwa upande wake Afisa Leseni Pemba Saumu Khamis Massoud, aliwashauri madereva kufuata taratibu za barabarani ikiwemo, uvaaji wa beji na sare muda wote wanapokua barabarani.

MWISHO