Monday, November 25

Micheweni imenufaika na mradi wa AMANI MIPAKANI

NA ABDI SULEIMAN.

MKUU wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, amesema kupitia mradi wa AMANI MIPAKANI wilaya hiyo imefaidika sana, kwani wamekuwa wakipata taarifa mbali mbali kutoka kwa makundi yaliyopatiwa mafunzo CYD.

Alisema tayari ameona mafanikio makubwa ambayo Wilaya ya yake imeyapata katika kipindi hiki cha utekelezaji wa maradi huo, tokea ulipoanza mwaka 2022 hadi 2023.

“Makundi yale ya mwanzo yameweza kufanyakazi vizuri sana na yanendelea na ufanyaji wao wa kazi, Wilaya sasa imekuwa ikipata taarifa mara kwa mara za wageni wanaoingia na tunafuatlia na kuwafikisha uhamiaji,”alisema.

Mkuu huyo aliyaeleza hayo huko Micheweni, wakati akifungua mafunzo kwa Masheha, viongozi wa dini, wakuu wa mdiko, watu mashuhuri, maafisa ustawi, viongozi wa Bodaboda, Tax na wakuu wa madiko, kupitia maradi wa AMANI MIPAKANI unaotekelezwa na CYD, kwa ufadhili wa Ubalozi wa Canada Tanzania kutipia Mfuko wa Maendeleo ya Kijamii (CFLI).

Alisema amani ndio kitu muhimu katika nchi yoyote ile, kwani ndio jambo ambalo linaleta maendeleo na linakuza uchumi wa nchi yoyote, wilaya imenufaika na mradi huo kuja ndani.

“Sote ni mashahidi kwa sasa katika nchi ya Ukreni na Urusi ambazo zinapigana na muda mrefu kwa sasa, kila nchi inapiga kelele juu ya kutetereka kwa uchumi wao,”alisema.

Alifahamisha kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa wananchi wa micheweni, kwani ndio Wilaya ambayo inabandari bubu nyingi ambazo zinaruhusu watu kuingia na kutoka bila viongozi kujua.

Aidha alisema miongoni mwa taarifa wanazozipata zinatokana na watu hao, wakiwemo waendesha bodaboda, tax, madereva wa gari za abiria na wakuu wa madiko.

mapema Mkurugenzi wa kituo cha Majadiliano kwa Vijana Zanzibar (CYD) Hashim Pondeza, alisema lengo ni kuwafahamisha viashiria mbali mbali vya uhalifu ambavyo vinaweza kutokea, uhalifu wa wizi, watu kuingia nchini bila ya kufuata taratibu zinazostahiki.

Alisema wanapozungumza suala la ulinzi husuzungumza upande mmoja, aliupongeza uongozi wa Wilaya na timu yake kwa kutoa mashirikiano kipindi chote cha utekelezaji wa mradi.

Hata hivyo aliwataka viongozi wa Wilaya na washiriki wa mkutano huo, kuhakikisha wanayafanyia kazi mafunzo yote waliopatiwa juu ya suala zima la AMANI MIPAKANI, ili kuona nchi inakua katika zingira bora nay amani.

Naye Afisa Vijana Wilaya ya Micheweni Yunus Mbarouk Kombo, alisema suala la amani ni muhimu sana katika maisha ya mwanadamu, kwani bila ya amani hakuna kitu chochote kinacho weza kufanyika.

“Sisi tusingekuwepo kama nchi isingekua na amani, huu mradi wa amani mipakani umekuja kwa wakati muwafaka, sisi huku micheweni tumekua na bandari bubu nyingi na hatujuwi nani anaingia na muda gani, vizuri tukawa makini katika mafunzo haya muda wote,”alisema.

Hata hivyo aliwataka wadhiriki hao, kuhakikisha wanakua mabalozi kwa waumini wao, kuhakikisha wanawafikishia ujumbe huo ili nchi iendelee kubakia salama.

MWISHO