Monday, November 25

SMZ kujenga madarasa zaidi ya kusomea Unguja na Pemba, ili wanafunzi waweze kwenda skuli mkondo mmoja.

 

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Mohamed Mussa Akizungumza na walimu, wazazi na wananchi wa shehia wa Mjini Wingwi Wilaya ya Micheweni mara baada ya kuifungua rasmi skuli ya Maandalizi Chupwe, iliyojengwa kwa nguvu za wananchi na Taasisi ya Ifraj Zanzibar Foundation
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Mohamed Mussa, akikagua vifaa vya eneo la baharini vilivyomo ndani ya skuli ya Maandalizi Chupwe shehia ya Mjini Wingi, mara baada ya kuifungua rasmi skuli hiyo, iliyojengwa kwa nguvu za wananchi na Taasisi ya Ifraj Zanzibar Foundation.
BAADHI ya wanafunzi wa skuli ya Maandalizi Chupwe shehia ya Mjini Wingi, wakifuatilia ufunguzi wa skuli yao iliyojengwa kwa nguvu za wananchi na Taasisi ya Ifraj Zanzibar Foundation

(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

 

NA ABDI SULEIMAN.

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Mohamed Mussa, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kujenga madarasa zaidi ya kusomea wanafunzi Unguja na Pemba, ili wanafunzi waweze kwenda skuli mkondo mmoja baada ya miwili iliyopo sasa.

Alisema adhma ya serikali ya ujenzi wa madarasa mapya unatarajia kuanza ndani ya Mwaka huu, ili kuondosha kabisa changamoto ya kuingia mikondo miwili kwa wanafunzi.

Waziri Lela aliyaeleza hayo mara baada ya kufungua skuli ya Maandalizi CHUPWE shehia ya Mjini Wingi Wilaya ya Micheweni iliyojengwa kwa nguvu za Wananchi wa Vijiji vya Chupwe, Sebudawa na Taasisi ya Ifraji Zanzibar Foundation.

Alisema dhamira ya serikali kwa wananchi wake bado iko pale pale ya kuwapelekea maendeleo, ikiwemo sekta ya elimu ambayo tayari Wilaya ya Micheweni kupitia fedha za COVID 19 imejengewa madarasa 103 jambo ambalo la kupigiwa mfano.

“Sote ni mashahadi sekta ya elimu micheweni imepiga hatua kubwa, kila mtu ameona mabadiliko yaliyopo bado tunapaswa kuendelea kumuunga mkono Rais Wete Dk.Hussein ili kufikia malengo aliyokusudia,”alisema.

Aidha waziri Lela aliwahidi wananchi wa vijiji hivyo kuwajengea skuli ya msingi, ili wanafunzi wanaomaliza maandalizi kuendelea kusoma hapo hapo na sio kwenda mbali jambo ambalo ni hatari kwao.

Aliwasihi walimu wa Tutu kubadilika na kujua wajibu wao, kwani sasa wamekua wafanyakazi wa serikali kama ilivyo wengine, hivyo wanafunzi ndio tegemeo lao kubwa katika kuwafundisha mambo mema na kufikia ndoto zao.

Hata hivyo aliwataka wazazi kuhakikisha wanafuatilia maendeleo ya watoto wao, kwani bila ya mashirikiano ya walimu na wazazi wanafunzi hawatofikia popote.

“Lazima watoto wanaporudi majumbani kujua wameandika nini au wamesoma nini, hapa tutakua tumejenga jamii iliyobora, vijana wanahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wazazi,”alisema.

Naye Mkuuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahay, aliishukuru taasisi ya Ifraj Zanzibar Foundation, kwa misaada mbali mbali inayoitoa katika wilaya ya micheweni kupitia sekta mbali mbali ikiwemo Elimu na watoto mayatima.

Alisema awali watoto walikua wakisoma katika mazingira mgumu, kwani Wilaya ya Micheweni kila mtu ni muumini wa Maendeleo hali iliyopelekea wananchi wa vijiji hivyo kuwatafuta wafadhili Milele na kuwajengea skuli hiyo.

“Sisi sote ni waumini wa maendeleo katika wilaya yetu, baada ya kuona tatizo lipo wananchi wametafuta wafadhili wenye na sote leo tumeona haya maendeleo,”alisema.

Hata hivyo aliwataka wananchi kuthamini juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na Rais Dk.Hussein Mwinyi, katika kupeleka maendeleo bora.

Kwa upande wake Naibu Ktaibu Mkuu Wizara ya ELimu Zanzibar Dkt.Mwanakhamis Adam Ameir, aliishukuru Taasisi ya Ifraj Zanzibar Foundation kwa kusaidia sekta ya Elimu Zanzibar, kwani bila ya elimu hakuna maeneo yoyote yatakayofikiwa.

Aidha aliwataka walimu kujielewa, kujitambua na kujua thamani yao kwa taifa, kwani vijana wengi wanawategemea wanapokua skuli katika kuwafundisha mambo mema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Ifraj Zanzibar Faoundation Abdalla Said Abdalla, alisema ujenzi wa shuku hiyo umegharimu Zaidi ya shilingi Milioni 48.5 hadi kukamilika kwake, ikiwemo nguvu za wananchi kwenye hatua ya msingi (foundation).

Alisema taasisi hiyo itaendelea kusaidia sekta mbali mbali muhimu nchini, kwani tayari imeshajenga skuli maeneo mbali mbali ya Pemba na vituo vya afya kwa lengo la kuunga mkono juhudi mbali mbali za Serikali.

Mapema akisoma risala ya skuli hiyo mwalimu Rehema Khamis Massoud, alisema jenge hilo la vyumba viwili vya kusomea linatumika kwa wanafunzi 170 walioandikishwa huku kukiwa na watoto 110 bado hawajaandikishwa skulini hapo.

Hata hivyo aliyomba serikali kuwapatia jengo jengine la skuli ya msingi, ili kuwasaidia watoto watakaomaliza skuli mwakini kuwa raihisi kujiunga na skuli mpya na sio kufuata huduma maeneo ya mbali.

MWISHO