Monday, November 25

“Serikali bado inahitaji wataalamu wa fani mbali mbali,wanafunzi shuhulikeni na masomo ili kuja kuisaidia serikali”-wWaziri Shamata.

 

NA ABDI SULEIMAN.

WAZIRI wa Kilimo Mifugo Maliasili na Umwagiliaji Zanzibar Shamata Shaame Khamis, amesema serikali bado inahitaji wataalamu wa fani mbali mbali, hivyo wanafunzi ni wakati wao kushuhulikia masomo ili kuja kuisaidia serikali.

Alisema miongoni mwa nafasi hizo za wataalamu ni Afya, Kilimo, Mifugo, Injiniaringi, barabara, maji, hata uchimbaji wa gesi na mafuta, hivyo elimu ndio kitu pekee kwa sasa kitakacho msaidia .

Waziri huyo aliyaeleza hayo wakati alipokua akizungumza na wanafunzi na wahitiumu wa kidato cha nne skuli ya madungu Sekondari, wakati wa mahafali ya 10 ya skuli hiyo.

Alisema wanafunzi wanapaswa kujifunza kwa kuwekeza yale yaliokuwa mema, ili waweze kufikia maendeleo yao waliokusudia kielimu.

“Lazima tuelekeze nguvu zetu na elimu yetu katika suala la elimu, elimu ndio kila kitu kwa sasa katika kufikia maendeleo, watalamu mbali mbali wanahitajika ili kufikia maendeleo,”alisema.

Akizungumzia suala la maendeleo alisema ni lawote na sio la mtu mmoja au chama kimoja, hivyo lazima kuzidisha mikakati ili kuona mafanikio yaliyokusudiwa yanafikiwa tena kwa kivtendo ikiwemo suala la kufuta Divishani II skulini hapo.

“Elimu ndio ufunguo wa maisha mtu aliyepata elimu hayuko sawa na mtu aliyekua hakupata elimu, lazima watapishana katika mambo mbali mbali ikiwemo hata maendeleo pia,”alisema.

Hata hivyo aliwataka wanafunzi wanaohitimu skuli hapo, kuhakikisha wanaendelea kusoma mambo mbali mbali katika kipindi hiki kifupi cha kusubiria matokeo.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Micheweni Zanzibar Fatma Hamad Rajab, aliwataka wazazi na walezi kuongeza mashirikiano na walimu katika suala zima la kufuatilia maendeleo ya elimu kwa watoto wao.

Aidha aliwataka wanafunzi kuhakikisha wanashuhulikia masomo yao ili waweze kutimiza ndoto zao, kwani bado serikali inahitaji wataalamu mbali mbali.

“Wanafunzi wangu someni masomo ya sayansi ili tupate wataalamu, lakini ikiwa sayansi huifahamu basi hata huku arti pia tusome, wataalamu nako wanahitajika pia,”alisema.

Mapema mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Mohamed Shamte Omar, aliwasihi wanafunzi kujitahidi kusaidia taifa kwa kusoma kwa bidii, huku wazazi wakiendelea kushajihisha na kusimamia vijana wao katika suala la elimu.

Akizungumzia suala la changamoto, alisema bado wanahitaji misaada zaidi, ikiwemo walimu wa masomo ya sayansi, pamoja na kuajiriwa kwa basa wa skuli hiyo ili kuwapunguzia mzigo wazazi wa wanafunzi kwani ndio wanaomlipa mshahara hadi sasa.

Akisoma risala ya wanafunzi katika mahafali hayo, mwanafunzi Hunayya Sharif Maalimu, alisema changamoto kubwa inayowakabili wanafunzi ukosefu wa dahalia ya kulala wanafunzi wa kike, kwani mpaka sasa wanafunzi hao wanalala aktika nyumba ya kukodi.

MWISHO