NA ABDI SULEIMAN.
WAZIRI wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, amewataka wananachi kuwa na tabia ya kupima afya zao mara kwa mara, ikiwemo maambukizi ya Ukimwi, ili kujua wanasumbuliwa na nini kwenye miili yao na waweze kuchukua hatua stahiki.
Alisema ZAPHA+ kwa wao sio mpinzani, bali wanafanya kazi pamoja na wanafanya kwa mashirikiano ya hali ya juu, kwani lengo lao ni moja ni kukinga na kutoa elimu ya afya ili watu waweze kuelewa.
Waziri Mazrui aliyaeleza hayo wakati alipokua akizungumza na wananchi na wanachama wa ZAPHA+, mara baada ya uzinduzi wa Kituo cha Jamii na Watoto ZAPHA+ Pemba Makungeni Shehia ya Wawi, Wilaya ya Chake Chake Pemba.
Aidha alisema wananchi wanapaswa kufika Hospitali mara wanapojiona wana dalili za ugonjwa, hivyo elimu ya afya kwa aliyekuwa hajaathirika anapaswa kupewa ya kutosha ili athiathirike zaidi.
“Yule ambaye ameathirika aweze kupatiwa tiba, ili kufanya kazi zake na kuendeleza maisha yake, lazima tuwe tayari na tushirikiane katika kutoa elimu na kuelimisha wananchi,”alisema.
Aidha amewasisitiza kina mama juu ya umuhimu wa kufika mapema hospitali, kwa ajili ya kupata vipimo na huduma nyenginezo mara wanapojihisi wajawazito, kwani huo ni mkakati wa kuzuaia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati kujifungua.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, akizungumza kwa niaba ta Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massud, alisema uwepo wa kituo hicho kitaongeza utoaji wa huduma na ushauri nasaha kwa vijana na wanachi kwa ujumla.
Alisema kituo hicho kina msaada mkubwa kwa jamii, katika kutoa huduma kwa wananchi mbali mbali, wananchi kufahamu wanapaswa kwenda kupima afya zao na kujua hali zao.
“Majibu watakayoyapata wataweza kuyafanyia kazi kwa kupewa ushauri nasaha, hapa walipo sasa ni pazuri sana kuliko pale kwenye kontena, watu walikuwa wanasita kutokana na mazingira kutokua rafiki,”alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Ukimwi Zanzibar Dr. Ali Salim Ali, alisema ZAPHA+ imepiga hatua kubwa tokea kuanzishwa mwaka 2006, ambapo hali ya unyanyapaa umepungua kidogo ila sehemu nyengine upo.
Alisema kwenye vituo vya afya ambavyo vinawakwaza watu wenye virusi vya ukimwi kushindwa kwenda kupata huduma, kutokana na kunyanyapaliwa.
“Kazi kubwa ya kuondosha unyanyapaa imeondoshwa na ZAPHA+, wanachama wa ZAPHA+ wako tayari kutetea kutokunyanyapaliwa kuliko mtu aliekua sio mwanachama wao,”alisema.
Mwenyekiti wa Zapha+ Hasina Hamad, aliwataka wananchi kuendelea kukitumia kituo hicho kwa kupata ushauri nasaha, Zaidi ya Shilingi milioni 41 zimetumika katika ujenzi wa jengo la Jumuiya ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Zanzibar Zapha+ upande wa Pemba, ambalo litatumika kwa ajili ya Kituo cha Jamii na Watoto.
MWISHO