Thursday, January 2

BAADHI YA WAFANYA BIASHARA HAWAKO TAYARI KUTUMIA MASHINE ZA UTOAJI RISITI. – RC MATAR

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, akizungumza katika mkutano wa walipakodi, taasisi mbali mbali za Serikali na Binafsi, mkutano uliofanyika katika ofisi za ZRA Gombani Wilaya ya Chake Chake
WATENDAJI kutoka Taasisi mbali mbali za Serikali Pemba, wakifuatilia kwa makini mkutano wa walipakodi na taasisi mbali mbali za serikali na binafsi, mkutano uliofanyika katika ofisi za ZRA Gombani Chake Chake
BAADHI ya Wafanyabiashara Mkoa wa Kusini Pemba, wakifuatilia kwa makini aMkutano wa walipakodi ulioandaliwa na kamishna Mkuu wa ZRA na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba na kufanyika katika ofisi za ZRA Gombani Chake Chake
MKUU wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, akizungumza na kuwakaribisha walipakodi katika mkutano maalumu wa walipakodi, taasisi mbali mbali za Serikali na Bianfsi, mkutano ulioafanyika katika ofisi za ZRA Gombani Chake Chake
KAMISHNA Mkuu wa ZRA Zanzibar Yussuph Juma Mwenda akibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa ZRA Pemba Jamal Hassan Jamali, wakati walipokua katika mkutano wa walipakodi, Taasisi mbali mbali za Serikali na Binafsi, mkutano uliofanyika katika ofisi za ZRA Gombani Chake Chake
KAMISHNA Mkuu wa ZRA Zanzibar Yusuph Juma Mwenda, akijibu hoja na maswali mbali mbali ya wafanyabiashara mbali mbali Mkoa wa Kusini Pemba, katika mkutano wa walipakodi, taasisi mbali mbali za serikali na binafsi mkutano uliofanyika katika ofisi za ZRA Gombani Chake Chake.
MMOJA ya walipakodi wa ZRA Tahia Maohamed Sultani, akichangia katika mkutano wa walipakodi, Taasisi mbali mbali uliandaliwa na kamishna Mkuu wa ZRA Zanzibar na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba na kufanyika katika ofisi za ZRA Gombani Chake Chake.

 

(PICHA NA:ABDI SULEIMAN,PEMBA)

BAKAR MUSSA –PEMBA.

MKUU wa mkoa wa Kusini Pemba , Matar Zahor Massoud amesema kuwa pamoja na juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya  uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa kutumia mashine maalumu za kutolea risiti za Elektronik , lakini bado kuna baadhi ya wafanyabiashara hawajakuwa tayari kuendana na mfumo huo.

Alisema ni wajibu wa kisheria kwa kila Mfanyabiashara kuwa na mashine ya kutolea risiti za Elektronik na kuitumia ili Serikali iweze kupata mapato yake inayostahili na kwa ukamilifu wake.

Matar aliyaeleza hayo huko katika ukumbi wa Mamlaka ya mapato Zanzibar (ZRA) Gombani Pemba wakati alipokuwa akizungumza na Wafanyabiashara wa mkoa wa Kusini kisiwani humo ikiwa ni uendelezo wa mikutano yake ya kusikiliza kero mbali mbali kupitia makundi tafauti.

Alifahamishwa kuwa kila mmoja anawajibu wa kutambuwa kuwa hakuna Serikali yoyote inayokwenda bila ya kuwa na kodi kwani ndio inayoiwezesha kupanga mipango ya maendeleo ya sekta mbali mbali kwa wananchi wake.

“ Wafanyabiashara nawaomba muelewe kuwa kodi munazolipa ndio zinazoisaidia Serikali kupanga mipango yake ya maendeleo na nchi yoyote Duniani inafanya ustawi wa wananchi wake kupitia kodi zinazolipwa kupitia vianzio mbali mbali vilivyowekwa”, alisema RC.

Alisema kuwa Serikali ya Mkoa huo haitomuonea haya na wala haitomvumilia Mfanyabiashara yoyote ambae hatokwenda kwa majinu wa sheria za nchi wakati akifanya shuhuli zake za biashara kwani nchi inakwenda kwa mujibu wa sheria.

“ Ni wahakikishie wafanyabiashara wa mkoa wa Kusini Pemba , Serikali haiko tayari kumuonea mtu yoyote pale anapofanya shuhuli zake kwa mujibu wa sheria lakini haitovumilia kwa mtu ambae ataonekana anapindisha sheria na pale penye dosari yoyote wanayofursa ya kuzungumza na wahusika , watasikilizwa na zitapatiwa ufumbuzi kero zao”, alieleza.

Alieleza kuwa amelazimika kuitisha mkutano huo kwa Wafanyabiashara wa mkoa wake ili kusikiliza kero mbali mbali zinazowakwaza jambo ambalo limepelekea kuongezeka kwa bei ya Bidhaa hususan Mchele ambao ndio chakula kikuu kwa  wananchi wa Zanzibar jambo ambalo limetowa taharuki kubwa.

Mkuu wa mkoa huyo alisema kumekuwa na visingizio vingi kutoka kwa Wafanyabiashara ambayo wanadai kupandisha bei ya bidhaa hiyo jambo ambalo vyengine havina ukweli hivyo amewaita na viongozi wa taasisi mbali mbali zinahusiana na hilo ili kupata uhakika wa jambo hilo.

Matar alifahamisha haoni vizuri wala hafurahii kuona Wananchi wanapata shida ya chakula kwani hata kama yeye ni Mkuu wa mkoa lakini anapata mahitaji kupitia kwa Wafanyabiashara na maduka hayo hayo , hivyo anauelewa mkubwa wa changamoto inayowakumba wananchi kipindi hichi.

“Pamoja na kuwa mimi ni Mkuu wa mkoa lakini pia ni mwananchi napata mahitaji kama wananchi wengine kwenye maduka yenu na siachi kufanya hivyo kwani cheo ni dhamana ya muda kesho nitakuwa pamoja na nyinyi hebu muelekeeni  Mwenyeezi Mungu musiweke matamanio mbele mukawaumiza wananchi wakati munaelewa hali zao za kipato”, alieleza.

Kwa upande wake Kamishna mkuu wa Mamlaka ya mapato   (ZRA) Zanzibar , Yusuph Juma Mwenda alisema Zanzibar ndio nchi pekee kwa nchi za Afrika Mashariki ambayo inatoza kodi ndogo  kwa Wafanyabiashara wake na imewafanya wafanyabiashara wakubwa  wanaoingiza bidhaa Zanzibar kutolipa ushuru wa VAT wala Stamp.

Alieleza kuwa Serikali imekuwa ikitowa mchango wa kupunguza ushuru ili wananchi waweze kufaidika na mahitaji yao mbali mbali ya chakula kutokana na hali zao kimaisha na pale kunapokuwa na changamoto milango ya ofisi zao ikowazi wafanyabiashara waende kuzieleza.

Alisema ZRA sio maaduwi kwa wafanyabiashara na wala isijengeke dhana hiyo ,ispokuwa kila anaestahiki kulipakodi alipe kodi yake hata kama ni kidogo lakini kama mtu yoyote anaekwepa kodi ataona anaonewa pale wakusanyaji mapato wanapokwenda kufanya kazi zao inangawaje mlipa kodi mzuri ataona anatetewa.

“ Nawashauri mfanyabiashara yoyote ambae anastahili kuwa na mashine ya kutolea risiti lazima awe nayo na muitumie ipasavyo ili kuondowa malalamiko na mivutano baina yenu na wakusanya mapato”, alisisitiza.

Kamishna Mwenda akijibu kero za Wafanyabiashara wa mkoa huo kuhusiana na watendaji wa ZRA alisema lengo la Mamlaka hiyo ni kujenga utowaji huduma bora kwa walipa kodi na itaendelea kuwaelimisha watendaji wao juu ya lugha nzuri kwa walipa kodi pale wanapokwenda kutekeleza majukumu yao.

Alieleza ZRA haitokuwa tayari kuona mfanyakazi wake anafanyakazi kinyume na maadili ya kazi yake na pindipo wakibaini hilo wanaweza kumchulia hatuwa ikiwemo kumpangia nafasi nyengine ili kuwe na utendaji uliotukuka .

“ Nitahakikisha kila Mtendaji wa ZRA anakuwa na lugha nzuri kwa watua anaowapatia huduma nakama kutakuwa na mtendaji wangu atakauwa anawapa shida walipakodi tuelezeni tutamchulia hatuwa kwani bila nyinyi hatuwezi kufanya kazi zetu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa tume ya ushindani wa biashara Zanzibar Moh’d Sijaamini Moh’d , aliwaomba Wafanayabiashara kuwa wakweli na kuteremsha bei ya bidhaa hiyo walioipandisha na kutowa taharuki kwa Wananchi kwani hailipishwi kodi kwa maana hiyo wasiwadanganye wananchi.

Aliwataka wafuate maagizo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi  ya kuteremsha bei ya mchele kwani huko mitaani hali za wananchi ni mbaya kutokana na kuongezeka bei kubwa ya bidhaa hiyo.

“ Wafanyabiashara kuweni wakweli musiwadayanye wananchi, wafanyabiashara wakubwa walieleza kuwa wanawauzia Mchele wafanyabiashara wadogo kwa bei ya shilingi 82,000/= mpaka 82,600/= kwa paket moja lakushangaza sasa hivi mlaji anauziwa paketi hiyo ya kilo 50 kwa bei ya 125,000/= jee huo sio uaduwi, sijahadhithiwa nimepita baadhi ya maduka nimeona”,alisema.

Alifahamisha kuwa taasisi yake itapita kwenye maduka kuangalia hali ya bei iliopo lakini  Serikali haitomuonea huruma wala haitomuonea Mfanyabiashara anaeuza mchele kwa kilo shilingi 3000/= ama zaidi ya 2000/= ama kipolo shilingi 100,000/= kwa muda huu lakini lengo ni kufikia bei ya nyuma iliokuwepo ya 1,700/= kwa kilo.

“ Tutamchukulia hatuwa Mfanyabiashara yoyote ambae tutabaini anaikuka maagizo yaliotolewa na Serikali ikiwemo kuongeza bei ama kuficha bidhaa kwa ajili ya kusubiri bei “, alisema.

Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara waliomba kuweko usawa wa ulipaji kodi kutoka kwa wenzao wa Unguja na Pemba ikiwemo ya asilimia 2 na 15, sambamba na kutafutwa vyanzo vyengine vya mapato na kufanyiwa uharaka wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Pemba na uboreshaji wa Bandari za Pemba jambo ambalo litaimarisha mapato.

MWISHO.