Wednesday, January 15

Upatikanaji Uhuru wa Habari hainufaishi vyombo vya Habari tu, ni kwa manufaa ya Taifa

WADAU wa habari Zanzibar wamesema ipo haja ya kufanyia marekebisho sheria ambazo zinakinzana na upatikanaji wa habari na uhuru wa vyombo vya habari ili kuchochea uwajibikaji na upatikanaji wa taarifa kwa lengo la kuleta maendeleo katika jamii.
Wameeleza kwamba suala la upatikanaji wa uhuru wa habari sio suala linalolenga kuwanufaisha waandishi na vyombo vya habari pekee bali ni suala mtambuka lenye manufaa ya kujenga uwajibikaji kwa viongozi na jamii kwa ujumla katika upatikanaji wa huduma.
Hayo yamebainishwa wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari Zanzibar ya kuwajengea uwezo kutambua mapungufu yaliyopo katika sheria za habari na kujadili mkakati wa kufanya uchechemzi wa mabadiliko ya sheria hizo ili kuweka mazingira rafiki ya vyombo vya habari Zanzibar.
Walisema kukiwa na sheria zinazotoa fursa kwa vyombo vya habari kutekeleza wajibu wake kwa uhuru bila vikwazo vya kisheria kunatoa nafasi kwa waandishi wa habari kusaidia jamii na mamlaka kuibua changamoto zilizopo katika maeneo mbalimbali na kutatuliwa kwa wakati.
Wakizungumza katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Shirika la Internews Tanzania walisema sheria zinazosimamia vyombo vya habari Zanzibar zinahitaji kufanyiwa marekebisho kutokana na baadhi ya vifungu vya sheria hizo kukandamiza uhuru wa habari.
Walitaja miongoni mwa sheria ambazo zimebainika kuwa na mapungufu yanayohitaji kufanyiwa marekebisho ni sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria Na.8 ya mwaka 1997, sheria ya Tume ya Utangazaji ya Zanzibar Na. 7 ya mwaka 1997 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010 pamoja na sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015.
Nyingine ni sheria ya kufuta sheria ya Baraza la Wawakilishi (kinga, uwezo na fursa) namba. 4 ya 2007 na kutunga sheria mpya ya Baraza la Wawakilishi (kinga, uwezo na fursa) katika kutekeleza kazi na mambo mengine yanayohusiana na hayo Na. 6 ya 2022, Sheria ya kufuta Sheria ya Uchaguzi namba. 11 ya 1984 na kutunga sheria ya uchaguzi ya mwaka 2017 na masuala mengine yanayohusiana nayo pamoja na sheria ya kufuta sheria ya adhabu Na. 6 ya 2004 na kutunga sheria mpya ya adhabu, kuweka masharti bora zaidi pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Akiwasilisha mapitio ya sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Na. 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria Na. 8 ya mwaka 1997, Imane Duwe, mkufunzi wa habari alisema Kifungu cha 3 cha sheria hiyo kimempa Waziri mamlaka ya kuteua Msajili wa Vitabu na Magazeti lakini iko kimya juu ya sifa na uzoefu wa msajili huyo.
Alieleza, “nafasi ya msajili inatakiwa itangazwe na achaguliwe kwa mujibu wa sifa, mfano awe mwanasheria au mtu mwenye taaluma ya habari na mawasiliano ya umma na sifa za msajili zinapaswa kuainishwa katika sheria.”
Aidha alibainisha kuhusu upatikanaji wa taarifa hakuna kifungu kinachozungumzia haki ya muandishi wa habari kupata taarifa kutoka kwa mamlaka mbalimbali.
“Sheria hii hajaweka na kuzingatia uhitaji wa sasa kulingana na dhana ya kidemokrasia au kuwa ni haki ya msingi kutengeneza mazingira ambayo mwandishi ataweza kupatiwa taarifa na habari pale inapohitajika hivyo tunapendekeza kiwepo kifungu maalum kitakachozungumzia upatikanaji wa taarifa na habari na kuanisha hatua zitakazo chukuliwa kwa aliyepewa dhamana ya kutoa taarifa hizo pale asipotekeleza haki hiyo,” alifahamisha mkufunzi huyo.
Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa aliwataka waandishi wa habari kuendelea kufanya ushawishi wa mabadiliko ya sheria zenye mapungufu ili kutoa fursa ya upatikanaji wa sheria zinazoweka mazingira bora kwa vyombo vya habari Zanzibar kutekeleza majukumu yake.
Alibainisha mkurugenzi huyo, “haki haiji mezani, ni lazima tukazane, tusiogope sheria na wala tusikate tamaa, tuendelee kuandika kwani sheria zipo kwaajili yetu ilimradi tunachokifanya ni kitu sahihi hatuvunji sheria. Twende tukaandike zaidi kwani tunafanya uchechemuzi ili wananchi wapate taarifa zinazowaletea maendeleo.”
Nae Salim Said Salim, mwandishi wa habari mwandamizi Zanzibar aliwahimiza waandishi wa habari kuzungumzia kifungu baada ya kifungu badala ya kuangalia mapungufu ya sheria kwa ujumla ili kusaidia kufanikisha lengo la uchechemzi wa mabadiliko ya sheria hizo.
“Sisi waandishi wa habari tunao wajibu mkubwa wa kuwafahamisha viongozi na wananchi wote kwamba tunapozungumzia uhuru wa habari si kwa manufaa ya waandishi na vyombo vya habari tu bali ni kwa manufaa ya jamii nzima kupata huduma zao muhimu,” Salim Said Salim, mwandishi wa habari mwandamizi Zanzibar.
Akichangia wakati wa mafuzo hayo Berema Suleiman Nassor, mwandishi wa habari kutoka Zenji FM alisema sheria kutoweka haki ya mwandishi wa habari kupata taarifa kutoka kwa mamlaka mbalimbali kunayima haki waandishi wa habari kupata baadhi ya taarifa pale zinapohitajika.
Alichangia, “unaweza kwenda kwenye ofisi kutaka taarifa fulani lakini kiongozi akakuzungusha na kukunyima kabisa taarifa kwasababu anajua hakuna sheria inayomlazimisha kutoa tarifa kwa mwandishi, tunaomba hiki kifungu kiwekwe kwenye sheria kwani tunakumbana na changamoto pale tunapokuwa tunahitaji kupata taarifa kutoka sehemu Fulani.”
TAMWA Zanzibar, shirika la Internews Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine wa habari Zanzibar wanaendelea kuangalia mapungufu yaliyopo katika sheria zinazosimamia sekta ya habari Zanzibar ili ziweze kufanyiwa marekibisho kwa lengo la kuweka mazingira rafiki ya vyombo vya habari Zanzibar kutekeleza majukumu yake kwa uhuru.
*Imeandaliwa na kitengo cha Mawasiliano*
*TAMWA ZANZIBAR*