Wednesday, January 15

WADAU wa sheria Kisiwani Pemba watoa elimu kwa wafanyakazi wanaobeba mizigo katika bandari ya Mkoani.

MRATIBU wa Utawala Bora Mohammed Massoud, akizungumza na wabebaji wa mizigo kutoka bandari ya Mkoani Kisiwani Pemba, ikiwa ni shamra shamra ya juma la wiki ya sheria.
MWANASHERIA kutoka Kituo Cha huduma za sheria Pemba Siti Habib, akitoa maelezo kwa wafanyakazi wanaobeba mizigo katika bandari ya Mkoani, ikiwa ni shamra shamra ya juma la wiki ya sheria huko bandarini Mkoani Pemba
MFANYAKAZI ambae anashughuli za kubeba mizigo katika bandari ya Mkoani Pemba Ali Khamis, akizungumza mbele ya wajumbe wa sheria huko bandarini Mkoani Pemba,ikiwa ni shamra shamra ya Maadhimisho ya juma la wiki ya sheria

(PICHA NA SAID ABDULRAHMAN PEMBA)

 

NA SAID ABDULRAHMAN –  PEMBA

WADAU wa sheria Kisiwani Pemba wameitaka Jamii kuacha tabia ya kuchukua sheria mikononi mwao na badala yake kufuata sheria na taratibu zilizopo nchini.

Wakizungumza na wafanyakazi wanaobeba mizigo katika bandari ya Mkoani Pemba, wadau hao wameleeza kuwa Bado jamii haina muamko wa ufuataji wa sheria pale wanapotokezewa na migogoro.
Assistance inspector kutoka jeshi la Polisi Saleh Ame Makame alisema kuwa wananchi walio wengi wamekuwa wakijichukulia sheria mikononi mwao jambo ambalo sio sahihi hata kidogo.
Alieleza kuwa ni vyema Kwa jamii kufuata sheria zilizopo na kuacha tabia ya kujihukumia wenyewe na mwisho wake kujiingiza katika matatizo badala ya kupata haki.
“Tulio wengi tumekuwa tukijichukulia hatua mikononi mwetu na hivyo badala ya kupata haki zetu tunaingia katika matatizo,” alisema Seleh.
“Lakini pia niwaombe ndugu zangu, kuwa karibu sana na jeshi la Polisi na pale ambapo mtapata matatizo katika kazi zenu ni vyema kuripoti katika vituo vya Polisi ili kuweza kupata haki zenu,” alisema Inspector Saleh.
Akijibu hoja zilizotolewa na wafanyakazi hao, Saleh alisema kuwa jeshi la Polisi halikurupuki tu kumkamata mwananchi bila ya kufanya uchunguzi zaidi wa jambo ambalo limetokea.
Alisisitiza kuwa jeshi la Polisi linafuatilia Kwa umakini matendo yote ambayo yanatokea na baadae ndio wanapoamua kuwatia nguvuni wahusika wa vitendo hivyo.
“Sisi jeshi la Polisi hatufanyi kazi ya kukamata mtu moja kwa moja bila ya kupitisha uchunguzi wetu na kujiridhisha kuwa kweli anaekamatwa ndie aliyetenda kosa,” alisema Saleh.
“Jeshi la Polisi kazi yake kubwa ni kulinda raia na Mali zao, hivyo ni vyema Kwa wananchi kuwa karibu sana na jeshi lao pale wanapokuwa na matatizo,” alieleza Saleh.
Nae Mwanasheria kutoka Kituo Cha huduma za sheria Kisiwani Pemba Siti Habibu aliutaka uongozi wa jumuia ya wafanyakazi wa bandarini kukaa pamoja na wanachama wao Ili kuweza kuwaeleza malengo ya jumuia yao.
Aidha Siti aliwasisitiza wafanyakazi hao kuwa, pale ambapo watapata matatizo katika kazi zako ni wajibu kuripoti Kwa viongozi wao kwa ajili ya kusaidia.
Sambamba na hayo Siti aliwataka wafanyakazi hao kutambua wajibu wao na haki zao na pale ambapo patatokea kasoro ni eneo gani ambalo wanatakiwa waende ili kuweza kutatuliwa.
“Sisi tupo hapa bandarini na wateja wetu ni wananchi ambao wanasafiri, jee pale ambapo limetokezea tatizo tunapaswa tuelekee wapi ili tuweze kupata suluhisho hilo? ,” Alisema Siti.
Mapema akitoa maelezo juu mkutano huo, Mratibu wa Idara ya Utawala Bora Mohammed Massoud alieleza kuwa lengo Kuu ni kutoa msaada wa kisheria Bure Kwa jamii  kupitia  makundi mbali mbali.
Aidha Mratibu huyo alifahamisha kuwa Kwa Sasa wako katika wiki ya sheria ambapo wadau wa sheria nikudhihirisha utendaji wao kuliko vipindi vyengine.
“Kilele Cha Maadhimisho hayo itakuwa ni February 13 katika Viwanja vya tennis  Chake Chake,” alisema Mohammed.
Nao wafanyakazi hao wamesema kuwa changamoto kubwa waliyonayo katika shughuli yao hiyo ni kuwa hawana chombo rasmi Cha kuwatetea pale wanapopata matatizo wakati wakiwa kazini.
Aidha wafanyakazi hao walisema kuwa matajiri ambao wanaingiza mizigo yao bandarini hapo hawana Imani nao kutokana na kuwafanyisha kazi kubwa lakini kipato kidogo.
“Hivi sasa polo moja ya mchele ni Tsh, 120000/- lakini sisi hapa bandarini tunateremsha polo hiyo Kwa Tsh 300 ambapo Bei hiyo imeshapitwa na muda,”
Akitoa ufafanuzi wa bei ya ubebaji mzigo katika bandari ya Mkoani,Mkuu wa bandari ya Mkoani Abdalla Kassim Shimeli aliutaka uongozi wa wafanyakazi hao kuandika barua ya malamiko hao na kuifikisha ofisini kwake ili hatua zinazostahiki ziweze kuchukuliwa.