Monday, November 25

SMZ Imezitaka Taasisi za Umma Kubadili Mifumo ya Zamani ya Utendaji na Utoaji Huduma kwa Wananchi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar, iliyofanyika leo 13-2-2023 katika viwanja vya Mahkama Kuu Zanzibar Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.

 

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imezitaka taasisi za umma kubadili mifumo ya zamani ya utendaji  na utoaji huduma kwa wananchi kwa kuanzisha mifumo ya kisasa ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha utendaji wao kuenda na kasi ya matumizi ya teknolojia.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyasema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya Sheria, Tunguu  Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema wakati huu wa sayansi na teknolojia mifumo ya uendeshaji taasisi kwa kutumia karatasi na kalamu imepitwa na wakati, hivyo alizitaka taasisi za umma zikiwemo taasisi za sheria na wadau wake kubadili mifumo ya utendaji wao ili kuendana na kasi ya teknolojia.

Alisema matumizi ya TEHAMA hurahisisha utendaji na kuondosha usumbufu pia kusaidia jitihada za Serikali za kukuza uchumi wa nchi na kuimarisha ustawi wa jamii kwa kuokoa fedha nyingi zinazogharamia shughuli zinazotekelezwa kwa mifumo ya zamani na badala yake gharama ya fedha hizo zitaelekezwa kwenye shughuli nyengine za maendeleo.

Akizungumzia haki mtandao Mahakamani, Rais Dk. Mwinyi alisema ni muhimu kwa ujenzi wa taasisi bora za kisheria kwani mfumo unaendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayotokea duniani.

Hata hivyo, aliipongeza Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa mara ya kwanza kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa kusajili mawakili ambao alieleza kwa sasa watafungua mashauri na kufuatilia uendeshaji wa mashauri hayo wakiwa nyumbani, vijijini au Ofisini.

Alisema mfumo huo wa kisasa utasaidia kuokoa muda unaotumika kwenye taasisi za sheria kufanyia kazi nyengine za kuinua vipato vyao, kuimarisha uwazi, uwajibikaji, utawala bora, ukusanyaji mzuri wa mapato na kuimarisha uchumi wa nchi pamoja na kusaidia kukuza imani ya wananchi na wawekezaji wa ndani na nje kwenye vyombo vya sheria.

Akizungumiza faida za matumizi ya TEHAMA kwenye taasisi za Sheria, Dk. Mwinyi alisema usikilizaji wa haraka wa mashauri na kutolewa maamuzi, upatikanaji wa takwimu sahihi, ufuatiliaji bora na usimamizi bora wa mashauri.

“Kwa kupitia haki mtandao, hakutakuwa na ulazima kwa Waheshimiwa Majaji wa Mahkama Kuu kusafirishwa kwenda Pemba kusikiliza mashauri, kwani mashauri hayo yatasikilizwa na kuamuliwa kwa mfumo wa Tehama tuu, Shahidi hatalazimika kufika kwenye jengo la mahakama kutoa ushahidi, inaweza kuandaliwa mifumo ya kutoa ushahidi wake kupitia hata simu yake tu ya mkononi, utaratibu huu mienendo ya kesi itapatikana kwa haraka” alifafanua Dk. Mwinyi.

Rais, Dk. Mwinyi aliahidi kutoa kipaumbele kwa bajeti ya matumizi ya Tehama kwa mahakama kuu Zanzibar ili kuimarisha miundombinu ya taasisi za sheria nchini, na kusema kwamba Serikali itatumia zaidi ya bilioni nne kwa ujenzi wa Majengo manne ya Mahakama kuu na za wilaya kwa Unguja na Pemba ambazo zinaendana na mifumo ya Tehama. Aidha, aliitaka mahakama hiyo kupitia taasisi zake kujipanga na kuwasilisha Serikalini mpangokazi na bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa adhma hiyo.

Pia alitoa wito kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kupitia Ofisi ya Wakala wa Serikali Mtandao kuzisimamia na kuzishauri ipasavyo taasisi zote za sheria katika kufikia lengo hilo la haki mtandao nchini.

Hata hivyo, aliiataka Mahakama kushirikiana na wadau wengine wa haki kwa maboresho yoyote kwenye mhimili wa Mahkama alisema yataleta matokeo chanya yenye ufanisi kwa ushirikiano imara na wadau.

Akizungumzia uanzishwaji wa Mahkama Maalum ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Rais Dk. Mwinyi alisifu jitihada zilizofikiwa na Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa hatua waliyofikia na kueleza kufarajika kwake kusikia tayari wameunda kamati ya wataalamu kwaajili ya kusimamia na kuratibu mchakato wa kuanzishwa Mahakama hiyo.

Alieleza Kuanzishwa kwa mahkama hiyo, kutaisaidia Serikali mapambano dhidi ya vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya Ofisi na rasilimali za umma ambayo huzorotesha uchumi wa nchi na ustawi wa jamii hali aliyoieleza inarejesha nyuma juhudi za Serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma alisema karne ya 21 inazitaka taasisi zote na watendaji wake kuwa na mabadiko ya fikra na kimtazamo yanayoendana na teknolojia iliopo duniani, nakuongeza kuwa mabadiliko ya teknolojia kwenye Mahakama Kuu ya Zanzibar yatasaidia utoaji wa haki na kukuza uchumi wa Zanzibar kwa kuleta mageuzi makubwa ya mabadiliko ya utendaji wao. Hivyo, aliwataka majaji kutumia jitihada za ziada ili kuendana na kasi ya huduma mtandao kwa sasa.

Naye, Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla, alisema maadhimisho ya siku ya sheria ni kuanza mwaka mpya wa mahakama na kueleza miongoni kwa mikakati ya mabadiliko yao kwenye ufanisi wa utendajikazi wao ni kuwafikia wananchi kwa haraka, kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kuwa karibu nao kwaajili ya kuwahudumia pamoja na kutoa mahakama rafiki zenye huduma za haraka.

Madhamisho ya Sheria yaliambatana na wiki ya sheria iliyoanza Febuari 06 mwaka huu kwa kutekelezwa shughuli mbalimbali za kisheria ikiwemo kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya sheria, kutambua mchango wa makaadhi kwa kutunukiwa vyeti vinara bora watoaji haki, kupokea mawakili wapywa, kuzindua mfumo wa kuwasajili mawakili kwa njia ya mtandao pamoja na kuhitimishwa kwa matembezi yaliyoandaliwa na taasisi ya “Zanzibar Maisha bora Foundation” yaliyoongozwa na Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Mama Mariam Mwinyi yakiwa na kauli mbiu “Kupinga vita dhidi ya Udhalilishaji wa kijinsia.”

Aidha, maadhimisho ya Sheria pia yalihudhuriwa na ujumbe kutoka Mahakama kuu ya Tanzania ulioongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Prof. Ibrahim Juma yalikua na kaulimbiu, “Haki mtandao ya kukuza uchumi na Ustawi wa jamii” ni maadhimisho ya 12 tokea kuanzishwa kwake mwaka 2012.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR.