Sunday, January 26

VIFUNGU VYA SHERIA YA TUME YA UTANGAAZAJI ZANZIBAR, VYATAJWA KUWA MWIBA MKALI KWA UHURU WA HABARI

NA HAJI NASSOR, PEMBA.

SASA ni miaka 26 tokea kuasisiwa kwa sheria ya Tume ya Utangaazaji Zanzibar nambari 7 ya mwaka 1997, licha ya kujumuisha na marekebisho yake.

Sheria hii, imekuja kusimamia, kuangalia mwenendo wa vyombo vya habari Zanzibar hasa redio, televisheni na vile vya kisasa vyenye kurusha maudhui yao mtandaoni.

Sheria hii yenye vifungu 30, vilivyobebwa na sehemu sita kuu, inavyovifungu kwa hakika sio rafiki, kuelekea uhuru kamili wa habari hapa Zanzibar.

SHERIA KWA UJUMLA

Kama ilivyo sheria nyingine zote, kwenye sehemu ya kwanza imeundwa na vifungu vitatu, maana kile cha nne, kimefutwa na kati ya hivyo kimoja kinatoa jina la sheria na maana ya maneno.

Kwa mfano, mtangaazaji ni mtu ambaye amepewa leseni chini ya sheria hii ya kutoa huduma za utangaazaji katika vyombo vya habari.

Kwenye sehemu ya pili ya sheria hii, yenyewe imeundwa na vifungu kuanzia cha tano (5) hadi cha 10, na kubwa zaidi lililopo ni pamoja na uanzishwaji wa Tume ya Utangaazaji Zanzibar.

Jengine ni kinga kwa wajumbe wa Tume, majukumu ya maafisa wa tume, muundo wake pamoja na saifa za Katibu Mtendaji.

Sehemu ya tatu ya sheria, imejitegemea kwa vifungu vinne (4) kuanzia kile cha 11 hadi cha 14, ni eneo lililotajwa uwepo wa zuio la utangaazaji, usiokuwa na leseni, masharti ya kuomba, utoaji wake na kiwango cha matumizi na kuongeza muda wake.

Sehemu ya nne (4), inaangalia zaidi uratibu na usimamizi wa utangaazaji, huku sehemu ya tano, ikundwa na vifungu saba (7) na ikiangalia zaidi amsuala fedha.

Sehemu ya sita ya sheria hii ya Utangaazaji Zanzibar nambari 7 ya mwaka 1997, imeundwa na vifungu vitano (5) kuanzia kile cha 26 hadi 30, ambacho kinaelezea kufutwa kwa sheria nambari 25 ya mwaka 1961.

VIFUNGU HASIDI KWA UHURU WA HABARI ZANZIBAR

Vipo vifungu kadhaa, lakini kimoja wapo, kinachotishia na kuutia doa uhuru wa habari hapa Zanzibar ni kile cha 13 (5).

‘’Mtu yeyote asiyeridhika na uamuzi wa Tume kutoa au kataka maombi, anaweza kukata rufaa kwa Waziri kwa namna ya njia itakavyoelezwa na kanuni,’’kinaeleza kifungu hicho.

Ambapo hapa, momba leseni (kwa mfano mwandishi wa habari), anapokataliwa kupewa leseni na Katibu Mtendaji wa Tume, akate rufaa kwa waziri, ambae ndie aliyemteua Katibu huyo.

Wadau wa sheria wanasema, jambo hilo lina utata, maana Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangaazaji na waziri anayehusika na utangaazaji, ni kiungo kimoja.

Mwandishi Talib Ussi Hamad, anasema hilo ni sawa na kesi ya Nyani, hakimu kuwa Nyani na mtoa ushahidi Nyani, na uamuzi utakwenda kwa Nyani.

Mwandishi Salim Said Salim, anasema kifungu hichi hakijakaa vyema, kwenye kuimarisha uhuru wa kujieleza na wa kutoa maoni hapa Zanzibar.

Mwandishi wa Shirika la Utangaazaji Zanzibar ‘ZBC’ Khadija Kombo anasema, kama Tume imekataa kutoa leseni, kifungu kingelekeza vyenginevyo, kwa mfano kukimbilia mahakamani.

Kifungu chengine chenye maneno yenye ukakasi na ukuaji wa wa uhuru wa habari ni cha 27 (1), ambapo waziri husika au mwengine aliyeidhinishwa, anaweza kutoa amri kumtaka mpewa leseni (mmiliki wa chombo cha habari), atangaaze jambo lolote ambalo kwa maoni ya Waziri, lina maslahi kwa umma au uslama wa taifa.

Hapa wadau wa habari wanasema, kifungu hicho kipo kishari shari zaidi, maana kimebainisha uwezo wa Waziri, kumlazimisha mpewa leseni kutangaaza jambo ambalo anaona tu ni kwa maslahi ya umma au usalama wa taifa.

Mdhamini wa Baraza la Habaeri Tanzania ‘MCT’ Zanzibar Shifaa Said Hassan, anasema neno kwa maslahi ya umma, sheria hiyo haijalitafsiri, hivyo waziri anaweza kutumia mwanya huo kutangaaza jambo ovu.

Hata Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA- Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali, anasema, neno usalama wa taifa, sheria hiyo kwenye vifungu vyake 30 na sehemu sita halikutajwa.

‘’Hapa mpewa leseni, amewekwa njia panda, maana Waziri akiamka vibaya anaweza kutumia mwanya huo, na kutoa taangazo ambalo halina maudhui na nchi, huku sheria ikimlinda,’’anasema.

Mwandishi wa kituo cha Redio cha Zenj fm Berema Suleiman Nassor, anasema hilo linajenga hofu kuanzia kwa wamiliki wa vyombo vya habari na mwandishi mmoja moja.

Mwanasheria wa Shirika la Magazeti ya serikali Zanzibar na mhariri wa habari wa shirika hilo, Juma Khamis Juma, anasema kwenye utekelezaji na tafsiri za vifungu vya sheria, hakutakiwi kuwepo neneo lenye utata.

‘’Kwa mfano neno waziri anaweza, akiona inafaa, akihisi na mengine yanayofanana na hayo, huwa ni hatari kuwepo kwenye maelezo ya utekelezaji wa sheria,’’anasema.

Ndio maana Mratibu wa Shirika la Internews Zanzibar, Zaina Mzee, anasema vifungu ambavyo vinampa uwezo mkubwa waziri, au vina maneno yenye utata, kwa sasa wanasimama kutaka viondolewe.

Kama sheria ni haki ya kikatiba, ni vyema isiwe na maneno au amelezo yanayoashiria kumpa mtu mmoja uwezo, kama vile anajiamulia kufanya mambo yake binafsi.

‘’Muda wa kuwa na sheria yenye maneno ya kukuza uhuru wa habari na uhuru kujieleza ndio huu kwa Zanzibar, na ndio maana tumeungana na TAMWA-Zanzibar na waandishi wa habari kuhakikisha hilo linafanyika,’’anasema.

‘’Nguvu ya kutaka sheria mpya ya habari, sisi tunavitegemea vyombo vya habari, na ndio maana tunavishirikisha kila hatua, ili kusaidia kuzieleza mamlaka ubaya wa sheria zinazosimamia habari ulivyo,’’anaeleza.

WANANCHI

Khamis Iddi Mabrouk na mwenzake Issa Haji Khamis wa Kangagani, wanasema waandishi wasipokuwa huru, hata wananchi hawatokuwa huru, kufanya uamuzi sahihi.

Hidaya Mjaka Ali wa Vitongoji mwenye ulemavu wa viungo, anasema, wanavitarajia mno vyombo vya habari, kuibua changamoto za jamii, na hilo litawezekana ikiwa wako huru.

Sheha wa shehia ya Mchanga mdogo Asaa Makame Said, anasema vyombo vya habari, havipaswi kuwekewa sheria zenye utata, kwani watashindwa kutekeleza kazi zao vyema.

NINI ATHARI YAKE?

Moja wadau wanasema, ni kuwafanya waandishi wa habari kufanyakazi kwa woga na nidhamu iliyopindukia mipaka, huku ikieleweka kuwa, wao kazi yao ni kuitekeleza Katiba.

Mwandishi Malik Shahran wa ZCTV anasema, suala la habari ni haki ya binadamu, si vyema kuwepo kwa sheria inayoonesha nguvu za mtu mmoja kufanya uamuzi.

‘’Maneno kama Waziri akiwezaatakavyoona inafaa au kwa maoni yake, yanapekelea wengine kukosa hamu ya kuingia kwenye sekta ya habari,’’anasema.

Mwandishi wa Mwanahalisi mtandaoni Jabir Idrissa, anasema athari kubwa ni wawekezaji sekta ya habari, kukosa hamu ya uwekezaji, na kundi kubwa kukosa ajira.

Miraji Manzi Kae wa redio Jamii Makunduchi, anasema woga wa waandishi kukosa kufichua maovu, wakati mwengine, hutokana na uwepo wa sheria kandamizi.

NINI KIFANYIKE?

Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari Zanzibar ‘ZPC’ Abdalla Mfaume, anasema moja ni kuzisemea sheria na vifungu kandamizi, ili waandishi wa habari wafanyekazi zao kama ilivyo, kwa makundi mengine.

Rahma Suleiman wa Gazeti la Nipashe, anasema waandishi na wadau wa habari, waungane kusindikiza mswada wa sheria habari Zanzibar ulipofikia, upelekwe hatua nyingine.

Mchambuzi wa sheria za habari Zanzibar Imane Duwe, anasema maneno kama ‘uwezo wa Mkurugenzi, Waziri, akiona inafaa, akihisi, kwa maoni yake’ kwenye sheria mpya ya habari yasitumike.

Mdhamini wa Baraza la Habari Tanzania ofisi ya Zanzibar Shifaa Said Hassan anasema, wakati umefika Zanzibar kuwa na sheria bora na rafiki.

Mkurugenzi wa TAMWA-Zanzibar Dk. Mzur Issa Ali, anasema ujio wa sheria mpya ya habari, vifungu vinavyompa uwezo mkubwa waziri vifutwe.

Hata mwandishi wa Redio Jamii Mkoani Khadija Rashid Nassor, anasema kila mmoja akitekeleza wajibu wake, sheria hiyo kandamizi itaondoka.

                              Mwisho