- Waandishi wa habari wanapaswa kuelimisha jamii juu ya umuhimu wake
- Mabadiliko Tabianchi, shughuli za binaadamu zatajwa kuwa chanzo
NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
TANZANIA imebarikiwa kuwa na rasilimali za maliasili na malikale, zenye mchango mkubwa katika uendelezaji utalii, ustawi wa wananchi na ukuaji wa uchumi.
Sekta ya utalii huchangia asilimia 25 ya fedha za kigeni na huzalisha ajira takriban milioni 1.6 moja kwa moja na za muda kwa mwaka.
Mkakati wa kitaifa wa kudhibiti Migogoro ya binaadamu na wanyamapori 2020/2024, watanzania 560 waliuawa na Simba katika kipindi cha mwaka 1990 hadi 2004 huku 308 wakijeruhiwa.
Aidha takwimu zimeendelea kueleza mwaka 2012/2019 watanzania 1,069 wamefariki dunia kwa kushambuliwa na wanyama, huku 204 wamepata ulemavu wa kudumu na mifugo 792 imekufa, huku hekta 41,404 zimeharibiwa na wanyamapori ndani ya kipindi hicho.
Hali hiyo imesababishia hasara kwa serikali kwani ililazimika kutumia zaidi ya shilingi bilioni 4.67 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wahanga wa wanyama.
Ushirikiano kati ya binadamu na wanyamapori ni kipaumbele cha kitaifa, kwa maendeleo endelevu na uhifadhi wa wanyamapori nchini, ongezeko la watu na mahitaji ya ardhi ni changamoto kubwa inayotishia ustawi wa wanyama.
Tumekuwa tukishuhudia miaka ya hivi karibuni migogoro mikubwa baina ya wanyama na binadamu, inayotokana na kuzibwa kwa mapitio ya wanyama (Shoroba).
Chama cha waandishi wa habari za mazingira Tanzania (JET), hivi karibuni, kimewakutanisha waandishi wa habari 25 kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania na Viswani, kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, unaotekelezwa na chama hicho kwa ufadhili wa shirika la misaada la watu wa Marekani (USAID).
HALI YA SHOROBA SASA IKOJE
Meneja ufuatiliaji na Tathmini USADI Tuhifadhi Maliasi John Steven Noronha, amesema Shoroba sasa zinatoweka kutokana na shughuli mbali mbali, zinazofanywa na binaadamu ambazo sio endelevu, kwani zipo zinazopitika na zipo hazipitiki na kutoweka kabisa.
“Mwanzoni zilikuwepo, lakini kutokana na shughuli za wananchi ambazo sio endelevu, shoroba zimetoweka kwa ujumla hali ya sio nzuri sana,”amesema.
Kumekua na matumizi mabaya yanayofanywa na binaadamu katika shoraba, hali inayotishia usalama na maisha ya wanyamapori wanaotumia shoroba kama sehemu ya kupata malisho na huduma nyengine.
Anaona wakati umefika sasa kuwepo kwa mipango mizuri ya matumizi ya ardhi, kwa kuruhusu kuwa na maeneo yatayoruhusu wanyama kupita kutoka eneo moja kwenda jengine, kwenye mfumo wa kiekolojia kila mnyama ana umuhimu.
“Mfano nyuki akipotea kuna madhara makubwa yanatokea hata mimea haitoweza kuzalishwa, lazima kuwaangalia wanyama hawao wasipotee,” anasema.
Aliwataka waandishi wa habari za Mazingira Tanzania, kuwa mstari wa mbele kuibua na kuelimisha jamii juu ya athari zitokanazo na shughuli za kibinadamu zinazofanywa ndani ya shoroba.
Naye Meneja ushirikishwaji wa sekta binafsi wa USAID Tuhifadhi Maliasili Dk. Eliakana Kalumanga, amesema maeneo yaliyohifadhiwa ambayo hutumiwa na wanyamapori (Shoroba), yanapaswa kuendelea kulindwa hata binaadamu maeneo hayo yanawasaidia.
Amesema maeneo ya shoroba wanyama huyatumia kwa shuhuli zao za kimaisha, kwa kujipatia chakula na mambo mengine ambapo binaadamu nae hunufaika kwa asilimia kubwa.
Aidha amesema shoroba zinawasaidia wanyama kupata mahitaji ya maji, malisho na hifadhi, binaadamu hupata kuni na madawa, huku akitolea mfano wananchi jamii ya wahazabi.
“Baadhi ya maeneo ya misitu yanavutia watalii, na yanafaida kiuchumi ikiwemo uwekezaji wa mahoteli ya kiutalii, mfano shoroba ya kwakuchinja inaunganisha hifadhi ya Burunge, Tarangire na Ziwa manyara, wananchi wanauza bidhaa za kitalii,”anasema.
“Kwa sasa hali za shoroba zetu mbalimbali nchini si nzuri, kwa mujibu wa takwimu za serikali zipo baadhi zimepotea kabisa, kutokana na shughuli hizo za wananchi zinazofanywa kila siku, kuna haja ya kuendelea kuwaelimisha wananchi,” alisema.
WAANDISHI WANASEMAJE JUU YA SHOROBA
Mwandishi wa habari kutoka Tanzania Daima Janeth Jovin, amesema waandishi bado wanakazi kubwa ya kufanya ili kuwe na usimamizi mzuri wa shoroba ambazo ndizo tegemeo kubwa kwa wanyamapori.
“Iwapo shoroba zitatoweka zote basi watalii hawatokuja tena Tanzania, wamanyama watakosa maeneo yao ya malisho na mahitaji yao,”amesema.
Naye Mwandishi Exuperius Kachenje, amesema waandishi wanamchango mkubwa wakuelimisha jamii juu ya umuhimu wa shoroba, ili kujuwa umuhimu wa uhifadhi na kulinda hifadhi hizo.
Mwanishi wa habari kutoka TBC Swalehe Makoye, amesema jukumu la kuelimisha jamii bado litakua ni waandishi, juu ya umuhimu wa kulinda na kuhifadhi shoroba za wanyamapori nchini, kwani zina mchango mkubwa kwa jamii na wanyama.
Anasema wanyama hupita kwenda kufuata mahitaji yao na binaadamu hutumia kwa ajili ya shuhuli zao za kijamii, sasa athari za madiliko ya tabianchi yameathiri shuhuli za binaadamu na maisha ya wanyamapori.
“Natamani kuona Tanzania inapiga hatua katika suala la uhifadhi wa wanyamapori, waandishi wa habari tunanafasi kubwa kutumia kalamu na sauti zetu kwa kuifikisha elimu kwa jamii iliyokuwa sahihi,”amesema.
WANAHABARI NA MADILIKO TABIANCHI
Mwandishi kutoka Hope Chanel Tanzania Nyamiti Kayora, amesema bado suala la mabadiliko ya tabianchi linaendelea kuathiri binaadamu na wanyamapori, kwani kila mmoja ana mahitaji yake katika ulimwengu.
“Binaadamu anahitaji maji, chakula na kuni hivi vyote vimekua vikiathiriwa na mabadiliko haya, wanyama wanao wanahitaji malisho na maji na yote yanapotea hapo ndio migogoro inapoanza sababu mabadiliko ta tbianchi,”anasema.
Naye mwandishi mkongwe kwenye masuala ya uhifadhi wa wanyamapori na bionuwai Tanzania, Salome Kitomari amesema dunia inapozungumzia mabadiliko ya tabianchi, Tanzania nayo ni sehemu ya nchi ambayo imeathiriwa na mabadiliko hayo.
“Tunapozungumzia mabadiliko tunazungumzia ukame na vipindi virefu mvua ambazo hazitabiriki, hata zikinyesha zinaleta madhara, upatikanaji wa maji nayo ni shida, lazima waandishi wa habari tuwe na uwelewa katika suala la mazingira ili kuelimisha jamii,”amesema.
Anasema iwapo uwelewa utakuwepo wa hali ya juu, basi habari za mazingira hifadhi, mapori ya akiba, mapori tengefu, WMA zitaandikwa kwa wingi na jamii kuweza kufahamu umuhimu wake.
Aidha amesema ni wakati sasa waandishi wanapaswa kuelekeza nguvu katika uwandishi wa habari za uhifadhi, ili kutunza mazingira kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kinachokujwa.
MABADILIKO YA TABIANCHI HALI IKOJE?
Akiwasilisha mada mabadiliko ya Tabinachi na bionuai Joseph Olila, kutoka USAID Tuhifadhi Maliasili, amesema mabadiliko hayo yanapelekea upungufu wa maji, katika maeneo wanyama wanayotegemea na kupelekea kuingia katika maeneo ya binaadamu na kusababisha migogoro.
“Wanayama hufuata maji nje ya hifadhi zao na kuingia katika makazi ya binaadamu, hupelekea kusababisha migogoro na wakati mwengine kutokea madhara,”amesema.
Anasema wakati mwengine binaadamu wanapoteza mazao ndio tegemeo kwao, kutokana na wanyama kusogelea kupata malisho na maji, hali inayopelekea jamii kuendelea kubakia maskini kufuatia mazao yao kuharibiwa na wanyama.
Aidha amesema baadhi ya bionuai za viumbe vidogo vidogo, kama chura na kinyonga vipo hatarini kupotea kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoikubwa Tanzania.
“Viumbe hivi haviwezi kusafiri masafa marefu kutafuta mahitaji yao, mabadiliko yanapozidi baadhi ya viumbe vinaweza kupotea kwa kushindwa kuhimili mabadiliko hayo,”amefahamisha.
Aidha kupotea kwa bionuai hizo, zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa taifa, hivi sasa sekta ya utalii imekua na mchango mkubwa katika kuchangia pato la taifa kupotea kwake ni hasara kwa nchi.
Naye afisa misitu mkuu na kiungo wa Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania Dk. Freddy Manyika, amesema miongoni mwa athari za mabadiliko Tabianchi ni ukame wa muda mrefu, unaopelekea kukosekana kwa malisho ya wanyama, matukio ya moto, kubadilika kwa miongo ya mvua, hali inayowalazimu wafugaji kuvamia kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kupelekea migogoro.
Amesema mabadiliko ya tabianchi hayabaguwi eneo lililohifadhiwa au halijahifadhiwa, tayari athari zake zimeshaonekana katika maeneo mengi, hali inayopeleka kuathiri mahusiano baina ya taasisi zinazohusika na uhifadhi na wananchi.
“Joto la bahari likipanda viumbe vilivyomo baharini vinapotea, maji yanaongezeka na kuathiri viumbe wengine zikiwemo fukwe kuliwa, baadhi ya visiwa kuanza kupotea,”amesema.
JET INAMTAZAMO GANI
Mkurugenzi Mtendaji wa cahama cha waandishi wa habari za mazingira Tanzania (JET), John Chikomo amesema kumekuwa na ongezeko la wanyamapori katika baadhi ya hifadhi, jambo ambalo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na uhifadhi wa wanyamapori.
“Hata ongezeko la watalii wanaoingia nchini ni mafanikio yanayotokana na elimu ya uhifadhi wa mazingira na wanyamapori inayotolewa mara kwa mara kwa waandishi wa habari hapa nchini,” alisema.
Naye mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru amesema wakati sasa kwa vyombo vya habari kujikitaka katika habari za uhifadhi na utunzaji wa mazingira, ili wananchi waweze kuona umuhimu wa utunzaji wa shoroba kwa maslahi ya taifa.
Amesema uchumi wa buluu uko kwenye Bioanuwai, udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi kila mtu anahusika kwa nafasi yake, ni wakati sasa kuelimishwa umuhimu wa uhifadhi kwa faida yake ya kiuchumi, kiutamaduni na vizazi vya sasa na vijavyo, ili uhifadhi kuwa endelevu.
Abdi Juma Suleiman
MWISHO