NA FATMA HAMAD, PEMBA
‘’Namshukuru nimefaulu mtihani wangu wa darasa la kumi na leo nipo darasani na jumuika na wenzangu, kuchota elimu hapa skuli ya sekondari Kinyasini,’’anasema mwanafunzi.
Hayo ni maneno ya mwanafunzi Hussein Abdalla Rashid mwenye ulemavu mchanganyiko mkaazi wa Kwale gongo wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba.
Abdalla ni mwanafunzi ambae anaisaka elimu katika mazingira magumu, kwani anakotoka kijiji cha mbali na kwenye mabonde na milima.
‘’Ninatoka kjiji cha mbali ambapo ni kilo mita 10, kutoka nyumbani kwetu hadi skuli, ila sijali kwani ndoto yangu ni kuwa fundi wa umeme,’’ alisema Abdala.
CHANGA MOTO ZA WANAFUNZI WENYE ULEMAVU
Abdalla Husein Rashid amesema kuwa anatamani siku moja awe fundi mkubwa wa umeme, lakini bado wanakilio kwenye Skuli zao hakuna walimu wa kufundisha wanafunzi wenye ulemavu.
Amesema kitendo cha wanafunzi wenye ulemavu kuchanganywa darasa moja na wasio na ulemavu huku wakiwa hawana mwalimu wa kuwasaidia ni kikwazo kwa wanafunzi wenye ulemavu.
‘’Mfumo wa elimu mjumuishi wa kutuchanganya darasa moja sisi wenye ulemavu na wasio na ulemavu bado hauja tutendea haki kwani hatuna walimu wa kutufundisha,’’ alisema.
Alisema kwa kweli hakua na tamaa ya kufalu darasa la kumi kwa sababu toka anze darasa la kwanza, hadi kufikia hapo hajapatapo mwalimu hata siku moja wa kumsaidia.
‘’Mimi nangalia tu ubaoni kinachoandikwa ndio naweka kichwani si fahamu chochote mwalimu anachofundisha ila tu mungu na rehema zake amenijalia nimefaulu’’.
Hivyo wamemuomba rais wao mpendwa kukiona na kukifanyia kazi kilio chao na kuwawekea mazingira rafiki ili nawao watimize ndoto zao.
Mohamed Karume mwanafunzi wa darasa la saba skuli ya sekondari Utaani Wete Pemba mwenye ulemavu wa viungo ameeleza kuwa anandoto ya kuwa Mhandisi majengo.
Amesema ili aweze kutimiza ndoto yake hiyo ni vyema serikali ikawajengea skuli yao malumu na kuwawekea miundombinu ya kutosha, kama vile walimu wa lugha za amala, vitabu vya kufundishia pamoja na kuwapatia misaada ya viti mwendo.
‘’Licha ya ulemavu wangu lakini nasoma kwa bidi, kwani nina hamu ya kuwa ‘injinia’ mkuu wa majengo, namuomba rais wetu atuangalie kwa jicho la huruma na sisi tunayo haki na tuna uwezo mkubwa wa kuleta maendeleo,’’ alielezea.
WALIMU WA SKULI
Mwalimu mkuu skuli ya Kinyasini iliyopo Wete Pemba Asha Mbarouk Rashid, amekiri kuwepo kwa kadhia hiyo ya ukosefu wa mwalimu anaejua lugha za alama kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu.
Hivyo aliomba Wizara ya elimu na mafunzo ya amali, kuwapa kipaumbele wallimu waliosomea elimu mjumuishi katika ajira jambo ambalo litasaidia kuondosha tatizo hilo maskulini mwa.
WAZAZI WA WANAFUNZI WENYE ULEMAVU
Asha Khamis mzazi wa mtoto mwenye ulemavu wa akili kutoka Micheweni, amesema katika mkoa wao wa kaskazini Pemba, skuli nyingi hazina walimu wa kufundisha elimu mjumuishi.
‘’Tunakilio kikubwa sisi wazazi kwani watoto wetu wenye ulemavu hawasomi, tunawaacha tu majumbani kwa sababu hata wakienda skuli, hawafahamu chochote kinachofundishwa wanakwenda wakicheza hakuna walimu wenye taluma,’’ alieleza.
Khatibu Mjaja kutoka Kwale Micheweni alieleza kuwa, yeye mtoto wake anaulemavu mchanganyiko na ameshindwa kumpeleka skuli, kwani hakuna mwalimu anaeweza kuzungumza nae na wakaelewana.
‘’Naumia kuona mtoto wangu huyo anakosa haki yake ya elimu kwa sababu tu ya ulemavu wake, sasa sjui Serikali yetu inampango gani ya kuimarisha miundombinu ya elimu, ili kuona wanafunzi wenye ulemavu wanapata elimu,’’anasema.
Mama mzazi wa mwanaunzi mwenye ulemavu wa viungo kutoka Kijichame Siwawi Omar, alisema kwa kweli walimu wengi wanaofundisha maskulini hawana taaluma za kufundisha watoto wenye ulemavu.
‘’Ni vyema kuwepo na walimu wenye taluma ya kufundisha wanafunzi wenye ulemavu, kwani bila ya hivyo siku zote tutawaacha nyuma kimaendeleo,’’ alisema mzazi
‘njiani tu na ni kuwapa walimu mzigo tu’’ alieleza mzazi.
WANAJAMII
Zahran Mohamed Yussuf mwanajamii kutoka Chake Chake ameeleza kuwa jamii iliokubwa ya watu wenye ulemavu wamekuwa wakikosa haki yao ya elimu na wamekuwa wakiachwa majumbani.
‘’Serikali watu wote ni wake na wote wanahitaji haki sawa hivyo tuikumbushe Serikali yetu ya Zanzibar kuweka mikakati madhubuti ikiwemo kusomesha kwa wingi walimu mjumuishi jambo ambalo litapunguza manun’guniko,’’ alishauri.
Sambamba na hilo aliwataka wadau wanaoshughulikia watu wenye ulemavu kuongeza nguvu ya kuwasemea na kuwatetea watu hao, ili kuona nawao wanapata fursa mbali mbali za kimaendeleo.
JUMUIA ZINAZOSHUHULIKIA WATU WENYE ULEMAVU
Kombo Ali Hamad Katibu wa jumuia ya watu wenye ulemavu wilaya ya Wete mkoa wa kasakazini Pemba, alisema kwa kweli walimu mjumuishi, maskulini ni kilio kikubwa kwa wanafunzi wenye ulemavu.
‘’Wanafunzi wenye ulemavu wanahaki ya kupata elimu na kuajiriwa lakini waliowengi wanakata tamaa hawafikii ndoto zao kutokana na mazingira magumu yaliopo skulini,’’ alieleza
Amesema kwa sasa elimu mjumuishi ni jina tu, lakini watu wenye ulemavu hawafaidiki na dhana hiyo kwani vifaa vya kufundishia na walimu wenye taaluma hiyo hawako.
Mudathir Sharif Khamis Naibu Katibu katika Jumuia ya watu wenye uwalbino kisiwani Pemba, amesema licha ya mchakato mkubwa uliofanyika, ili kuwepo na elimu mjumuishi lakini bado wanafunzi wenye ulemavu, wanaendelea kukumbwa na changamoto.
‘’Katika wilaya yetu ya Chake chake kuna wazazi wamekua wakitoka Ndagoni, Wesha na watoto wao wenye ulemavu kuwapeleka skuli ya Michakaini, ambapo ndio kituo kilichochaguliwa kitoe elimu mjumuishi, ni masafa marefu na maisha yenyewe haya tulionayo,’’ alieleza .
Hivyo ni lazima Serikali ikae itafakari hilo kwani mwisho wa siku kutawafanya wazazi hao kuwakatisha watoto wao na kubaki nao majumbani mwao kutokana na lengo lao walilokusudia la kupata haki yao ya elimu halifikiwi.
Mratibu wa Jumuia ya watu wasiona [ZANAB] wilaya ya Chake chake Suleiman Mansur, ameleza kuwa elimu mjumuisho bado haijawanufaisha wanafunzi wenye ulemavu, jambo ambalo linapelekea kufeli kwa masomo yao.
‘’Kuna baadhi ya walimu wanapewa taluma ya kufundisha elimu mjumuishi kwa muda wa miezi mitatu kwa kweli hiyo haitoshi, kama wanataka wenye ulemavu na wao wafaidike na elimu basi ni vyema somo la elimu mjumuishi,’’alieleza.
Mratibu wa ZAPDD Kisiwani Pemba Khalfan Amour Mohamed, ameeleza kuwa bado waalimu waliowengi hawajakuwa na taaluma ya kuwafundisha wanafunzi wote wenye ulemavu kulingana na mahaitaji ya mwanafunzi mwenyewe.
‘’Bado ule ujuzi na uwelewa wa kuwafundisha wanafunzi wenye ulemavu, mfano wenye ulemavu wa akili, na Viziwi hawajakuwa nao wa kutosha,’’ alieleza khalfan.
WANAHARAKATI
Mwanaharakati kutoka chama cha wandishi wa habari Wanawake Tanzania Tamwa ofisi ya Pemba Fath-iya Mussa Said amesema suala la walimu wa elimu mjumuishi bado ni kidogo maskulini watoto wenye ulemavu wanaendelea kuteseka.
‘’Bado watoto wetu hawajapata walimu wa kuwasomesha mana mwalimu mmoja ana madarasa manne matano jee atakua na muda gani wa kuwafundisha wenye ulemavu na wakafahamu bado serikali hili ni tatizo la kuliangalia kwa upeo wa juu zaid’’ alieleza mwanaharakati.
WIZARA YA ELIMU
Mratibu wa Elimu mjumuisho na Stady za maisha ‘EMSM’ Pemba Halima Mohamed Khamis amekiri kuwepo kwa tatizo hilo la walimu hususani waalimu wa kuwafundisha viziwi pamoja na wasiona .
‘’Kwa kipindi cha mwaka jana tulikua tuna idadi ya wanafunzi wenye ulemavu 1710 lakini ukiangalia walimu wote waliosomea elimu mjumuishi ni 69 ndani ya Pemba, hivyo bado shida ipo ukiangalia na idadi ya wanafunzi tulionao’’, alisema Mratib.
Aidha amesema Serikali kwa kuwajali wanafunzi wenye ulemavu tayari imeshachukua idadi ya walimu watakaofundisha elimu mjumuishi kwa ajili ya kuwajiri ili kuondosha tatizo hilo kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum.
KATIBA YA ZANZIBAR
Kifungu cha [10] [g] kinafafanua kwamba Serikali itawekea mazingira rafiki kwa makundi ya wagonjwa, waliojiajiri, Wazee, Watoto na watu wenye ulemavu.
Lakini hata kifungu cha 12 [1] kimesema kuwa watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
Sheria ya watu wenye ulemavu sheria namba 6 ya mwaka 2022 kifungu cha 28 [1] kimesema kuwa watu wenye ulemavu wanastahiki haki zote za msingi za binadamu sawa na watu wengine ikijumuisha, haki ya elimu, ikijumuisha mafunzo ya amali na mafunzo ya kukabiliana na maisha kulingana na aina za ulemavu.
Pia kifungu kidogo cha [2] kimesema kwa kuzingatia masharti ya kifungu kidogo cha kwanza [1] [a] cha kifungu hiki, Baraza kwa kushirikiana na taasisi yenye dhamana na masuala ya elimu itahakikisha; watu wenye ulemavu wanapata elimu na mafunzo ya amali katika ngazi zote na kuwepo na mfumo wa elimu mjumuishi unaozingatia mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu katika ngazi zote za elimu.
MWISHO