Thursday, January 16

Niwakati tusimame imara kutetea sheria mpya, wahanga kupata haki zao

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

NIMATUKO 504 ya udhalilishaji yaliripotiwa Zanzibar, kipindi cha miezi mitatu kutoka Novemba 2022 hadi mwezi Januari, 2023, ambayo yalihusisha vitendo vya ubakaji, ulawiti, vipigo kwa watoto, kutorosha, kutelekeza familia na udhalilishaji wa kijinsia.

Ni matukio mengi ndani ya kipindi kifupi, niwazi sasa kila mmoja anapaswa kuwa makini na kuwa mwanaharakati wakupinga vitendo hivyo kutokuendelea katika jamii.

Mke wa Rais wa Zanzibar mama Mariam Mwinyi, anasema matukio hayo ni mengi na yanazidi kila uchao hivyo, vyombo vya sheria kutekeleza juhudi za Serikali, kwa kutowaachia huru watuhumiwa wa makosa ya udhalilishaji nchini.

“Tunawaomba sana jeshi la polisi wasiwatoe hawa watu wanaotuhumiwa kwa makosa ya udhalilishaji,”amesema.

Makosa yanayohusiana na ‘GBV’ yapo mengi na yanaonekana katika sheria mbali mbali ambazo zimeanzisha makosa hayo, kutokana na hali hiyo ‘TAMWA’ wameona haja ya kuziorodhesha sheria hizo na kuonyesha kasoro za msingi kutokana na mazingira yaliyopo sasa.

Sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018 kifungu 7 kimetoa Mamlaka kwa Hakimu kutoa adhabu isiyozidi miaka 14 na faini isiyozidi shilingi milioni 14, vifungu vya adhabu vimeweka adhabu kubwa zaidi, kwa mfano kubaka adhabu yake ni kifungo cha maisha au isiyopungua miaka 30 pamoja na faini.

Kwa mfano mahakama ya mkoa kaskazini Pemba, kesi namba 36/2022 ilihusisha kosa la kubaka, mshitakiwa ni Ali Hassan Hamad (35) (muathiriwa miaka 11) alifungwa miaka 30 na fidia ya 2,000,000.

Kesi namba 53/2021, kosa la kulawiti, mshitakiwa ni Fadhil Mussa Sharif (35) (muathirika miaka15) alifungwa miaka 30.

Kwa upande wa mahakama ya mkoa kusini Pemba, kesi namba 36/2022, kosa la kubaka, mshitakiwa Ali Makame Khatib (25) (muathirika 11), alifungwa miaka 14 na fidia ya 1,000,000.

Kesi namba 37/2022, kosa la kulawiti, mshitakiwa Masoud Khamis Mussa (23) (muathirika 9) alifungwa miaka 20 na fidia ya 1,000,000.

Wakati mfumo wa adhabu haimsaidii muathirika, sheria nambari 6 ya mwaka 2018, imeweka adhabu ya kifungo pamoja na fidia, lakini katika mwaka 2022, jumla ya washatakiwa 15 walitiwa hatiani katika mahakama ya mkoa wa kusini Pemba, kesi 10 zilitakiwa kulipwa fidia na zote hazikulipwa.

Kwa upande wa Mahakama Mkoa wa Kaskazini amesema kesi 11 zilitolewa hukumu, kesi 10 zilitakiwa kulipwa fidia na zote hazijalipwa.

WAHANGA WA VITENDO HIVYO WANASEMAJE

“Sina tamaa ya kulipwa fidia, lakini familia ya kijana huko mtaani wanasema kuwa, hawalipi chochote kwa sababu wanajua kuwa kitakapomalizika kifungo, ataongezwa tu miezi mitatu ya adhabu kwa kutolipa fidia”,anasema.

Ameiomba Serikali uwepo mfuko maalumu wa fidia, ambao utawasaidia waathiriwa wa vitendo vya udhalilishaji, katika kutatua changamoto zinazowakumba watoto wao.

“Sio kama tunataka watoto wetu wabakwe, ili tulipwe fidia lakini limeshatokea ni vyema na hawa watoto waliodhalilishwa wakafikiriwa,”anasema.

Mama mmoja mkaazi wa Wingwi Wilaya ya Micheweni ambae mtoto wake wa miaka mitatu (3) alibakwa na kijana, amesema alitegemea fedha atakazopatiwa zitamsaidia kumshughulikia mwanae aliathirika kisaikolojia na kimwili, ingawa hajaulizwa chochote tangu kesi hiyo ilipopata hukumu mwaka jana.

“Kinachoniumiza zaidi ni kuona yule mshitakiwa alitakiwa kutumikia chuo cha mafunzo miaka 30, lakini haijatimia mwaka ameshatolewa eti kwa madai kuwa ni mgonjwa wa akili na amekwenda Unguja Mental”, ameeleza.

Anasema sio peke yake hajapata fidia bali, kuna baba ambae mtoto wake wa miaka 11 alibakwa na hukumu kutolewa mwaka jana hajaona fidia iliyotakiwa kulipwa.

Baba huyo mkaazi wa Madungu wilaya ya Chake Chake, amesema mshitakiwa alitakiwa atumikie chuo cha mafunzo kwa miaka saba na alipe fidia ya shilingi milioni mbili, ingawa bado hajalipwa fidia hiyo na wala hana tamaa ya kuipwa.

WANAHARAKATI WA WANAOPINGA UDHALILISHAJI PEMBA

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya TUJIPE Pemba Tatu Abdalla Msellem, amesema kutokuwepo kwa sheria maalum kunafanya masuala kuwa magumu na wahanga kukosa haki zao baada ya hukumu kutolewa, hata ikitolewa haifiki kwa wanaohusika.

Anasema fidia zinazotolewa hazipunguzi machungu, kwani athari yake ni endelevu na mwisho wa siku huathirika kisaikolojia, afya na kupelekea migogoro hata alipwe milioni 10 fidia hiyo haitoshi.

“Niwakati sasa kuwepo na sheria maalumu ikawa madhubuti na utekelezaji wake ukasimamiwa ipasavyo, itasaidia kupunguza joto la masuala hayo, sisi TUJIPE inapeperusha bendera na wahanga kupatiwa haki zao,”anasema.

Naye mwanaharakati Haji Nassor Mohamed, amesema ifike wakati kuwe na kifungu maalum katika sheria, kikasisitiza au kuweka mkazo au kutaja uwepo wa mfuko utakaoweza kuwasaidia wahanga wa vitendo vya udhalilishaji.

Anasema siku moja ifike wakati kuanzishe mfuko maalumu, kama uliopo Kenya na Afrika ya Kusini unaoweka haki ya watu walioathiriwa na matendo ya udhalilishaji, ulawiti, kubakwa baada ushahidi kutolewa, uwe na kiwango kikubwa cha fedha ili uweze kuwasaidia.

“Niwakati sasa kwa vyombo vya habari, wadau na wanasheria kupiga kelele na kuwepo kwa sheria maalumu, pale Mahakama zitakapoamua kuwepo na fidia, basi kuwe na Tume maalumu itakayofuatilia kwenye familia ya mtuhimuwa kama kuna kitu kiweze kuuzwa na kulipiwa fidia,”anasema.

OFISI YA DPP

Akizungumza kwa sharti la kutotaka kutajwa jina lake, mmoja ya Waendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Pemba, amesema hakuna sheria maalum ya fidia, ila vipo vifungu maalum vinaelekeza mahakama kutoza fidia kwa mshitakiwa wa makosa ya kiwemo ya makosa ya kujamiana.

“Kifungu cha 109 (1) cha sheria nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar, kinasema mshitakiwa akitiwa hatiani pamoja na adhabu atakayopewa, pia mahakama imtake alipe fidia kwa muathirika kwa kiwango ambacho mahakama wataona kinafaa,”anasema.

“Kifungu cha 313 (1) (2) na kifungu cha 314 vya sheria nambari ya mwaka 2018 sheria ya mwenendo wa makosa ya Jinai, kinaeleza mahakama itoze fidia kwa muathiriwa wa makosa ya udhalilishaji, baada ya kuombwa na Mwendesha Mashtaka au bila kuombwa,”anasema.

Anasema shida kubwa katika fidia zinatozwa mahakamani, hasa kwa makosa ya udhalilishaji washitakiwa hawalipi fidia hizo kama ilivyotakiwa.

“Naikumbuka moja ya kesi muathiriwa alikataa kwenda kuchukua alisema shilingi 500,000 zilikuwa kidogo alitaka nyingi zaidi tena sijui kama alienda kuchukua baadae au hakwenda,”amesema Mwendesha mashtaka huyo.

MAHAKAMA KUU PEMBA INAMTAZAMO GANI

Naibu Mrajis wa Mahakama Kuu Pemba Faraji Shomar Juma, amesema ni wakati sasa kuanzishwe kwa vifungu maalum vya kisheria, vitakavyoanzisha mfuko maalumu wa wahanga wavitendo vya udhalilishaji, mfuko ambao serikali itaweza kuchangia au wafadhili watachangia.

“Pale mtu mshtakiwa ameamuliwa kulipa fidia, watu watakwenda kwenye mfuko na fidia itapatikana, kwa kumtegemea mshatikiwa akitoka ndani na sheria haijampa ulazima kama atakapotoka lazima kulipa au laa,”anasema.

Aidha amesema wapo baadhi ya wanakosa fidia, washtakiwa wa makosa ya kubaka wakiwa watoto UN 18, mara nyingi jukumu linabebwa na mzazi na mzazi hulipa faini au fidia ili watoto.

TAMWA

Mratib wa chama hicho Ofisi ya Pemba Fat-hiya Mussa Said, amesema utaratibu uliopo hauwasaidii waathirika licha ya kuwepo kwa sheria nambari 6 ya mwaka 2018 ambayo imeweka adhabu ya kifungo na fidia, wala hazitolewi kutokana na kukosekana kwa sheria maalumu.

“Nadhani kungekuwepo na sheria maalumu ya kuwabana watu wanaopata hukumu ya fidia, ili wahanga waweze kupata haki yao, utaratibu wa fidia unahitaji kuwekewa sheria maalumu na sio kama ilivyo sasa,”alisema.

Ni wakati sasa kwa waandishi kuyasemea haya, ili Serikali iweze kujua kasoro zilizomo katika sheria mbali mbali.

TUME YA KUREKEBISHA SHERIA INAMAONI GANI?

Katibu wa Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar Mussa Kombo, amesema kwa sasa maeneo hayo ndio wanayoyafanyia kazi, ili kuona kunakuwepo na sheria maalum, ambayo itawasaidia waadhirika wa vitendo vya udhalilishaji kupata haki zao.

“Maeneo hayo ndio tunayoyafanyia kazi na tunampango kazi wakukutana na wadau mbali mbali, ili tuone kasoro iko wapi na waathirika waweze kupata fidia zao,”alisema.

NINI KIFANYIKE

Mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hiya Mussa, amesema athari ni kuongezeka kwa uhasama baina ya muhanga na mshtakiwa na kupelekea migogoro na mivutano kwenye jamii.

Mwanaharakati Tatu Abdalla, amesema wanahamu kuona siku moja kunakuwepo na sheria itakayosimamia masuala ya fidia kwa wanga wa udhalilishaji, ili wahanga waweze kupata haki zao na sio kubaki na machungu rohoni.

Afisa sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Ofisi ya Pemba Bakar Omar Ali, amesema nchi zilizoendelea zinamfuko maalum wa kuwafidia waathiriwa wa kesi za jinai, kwani kesi hizo mshitakiwa akipatikana na kosa anafungwa, na huko gerezani hana kitu cha kujipatia kipato.

“Serikali hizo zimeweka mfuko wa namna hiyo, na hapa serikali wanaweza kufanya hilo kwa kuanzisha mfuko maalum wa kuwalipia fidia waathiriwa, ikiwa wale wafungwa wao hawana uwezo wa kulipa fidia,”amesema.

Hivi karibuni Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar, kinatekeleza mradi wakupinga udhalilishaji zanzibar kwa ufadhili wa The Fondation For Civil Sociaty.

MWISHO.

Abdi Juma Suleiman

Journalist/Photographer

Zanzibarleo newspaper

Chake Chake -Pemba

+255774565947 or +255718968355

abdisuleiman33@gmail.com