RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema taasisi za dini na za kiraia zina mchango mkubwa kwa Serikali hasa kwenye jukumu zima la kuendeleza amani na maendeleo nchini.
Alisema taasisi za dini zina jukumu la kutoa huduma za kiroho, zinasaidia kujenga taifa lenye amani, mshikamano na maadili kwa jamii jambo linaloimarisha amani na maendeleo.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato, jimbo kuu la Kusini mwa Tanzani, Dkt. Godwin Lekundayo aliyefika na uongozi wake kujitambulisha.
Alisema taasisi hizo zimekua na ushirikiano mzuri na Serikali katika ustawi wa jamii bora na kustawisha mshikamano wa imani za kiroho katika kukuza vijana waadilifu.
Amani utulivu, umoja na maridhiano ni mambo ya msingi katika nchi yoyote na kuongeza kuwa amani inapokosekana mambo mengi hushindikana kutekelezwa kwa wakati unaostahiki yakiwemo maendeleo hata uhuru wa kufanya ibada.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliwapongeza viongozi hao kwa kuendelea kuhubiri na kuhamasisha amani kwa imani zao na kueleza licha ya taifa kuwa na mchanganyiko wa waumini wenye imani tofauti lakini linasonga mbele kimaendeleo. Hata hivyo, alizitaka taasisi hizo za dini kuendelea kuisaidia Serikali kulea taifa lenye uadilifu na vijana watiifu ili kujenga taifa lenye viongozi bora.
Naye, Askofu Mkuu wa Kanisa la Sabato Tanzania, Dkt. Godwin Lekundayo alisifu juhudi za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua iliyopiga ndani ya kipindi cha muda mfupi wa na kuzipongeza Serikali zote mbili ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar kwa kuimarisha umoja na mshikamano bila kujali tofauti za imani za wananchi.
Wakati huo huo, Rais Dk. Hussein Mwinyi alishiriki halfa ya ufunguzi wa ubalozi mdogo wa Umoja wa Nchi ya Falme za Kiarabu (UAE), Zanzibar ambapo Balozi Mdogo wa Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Saleh Al Hemeir aliwakaribisha wananchi wa Zanzibar kwenye ofisi hizo kuhudumiwa masuala mbalimbali ya kidiplomasia.
Akitoa salamu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrick Soraga aliipongeza UAE kwa kufungua ubalozi mdogo Zanzibar na kueleza itaimarisha uhusiano wa diplomasia baina ya watu wa pande mbili hizo.