Wednesday, January 15

RC Kusini Pemba akutana na kuzungumza na wajumbe wa baraza la Biashara wa mkoa, awataka kuhamasisha jamii, juu ya kuzitumia fursa zilizomo ndani ya Kiswa cha Pemba.

NA ABDI SULEIMAN.

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Masoud, amewataka wajumbe wa baraza la Biashara Mkoa huo, kufanya kazi ya pamoja kwenda kuhamasisha jamii, juu ya kuzitumia fursa mbali mbali zilizomo ndani ya Kiswa cha Pemba.

Alisema Kisiwa cha Pemba kimejaaliwa kuwa na fursa nyingi, ambazo bado hazijatumika, kama vile utalii, kilimo cha biashara, uvuvi vitu ambavyo bado havijatumiwa ipasavyo.

Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza hilo, aliyaeleza hayo katika mkutano wa mwanzo wa mwaka wa baraza hilo, uliofanyika mjini Chake Chake.

Alisema hivi sasa wananchi wanapaswa kujikita katika uzalishaji wa matunda mbali mbali ya juisi, ili viwanda vilivyopo Pemba vikianza kutengeneza waweze kuliteka soko hilo na sio matunda kuagiziwa kutoka nje ya kisiwa hicho.

“Sasa hivi hawa AMOS wapo katika hatua za mwisho za kukaguliwa na kuanza kazi ya kuzalisha juisi, vizuri wakulima wakajipanga ipasavyo katika uzalishaji wa matunda pale, kazi inapoanza isiwe shida kupatikana bidhaa,”alisema.

Aidha Mwenyekiti huyo, alisema madhumuni makubwa ni kujadili mambo mbali mbali yanayohusu biashara na maendeleo yake, ili kuweza kuishauri serikali kwa namna gani wananchi wanaweza kuendesha biashara zao.

Alisema dhamira kubwa ni kuleta maendeleo ya kiuchumi katika maeneo yao, kuondosha kila aina ya vikwazo ukwamu unaoweza kupelekea kutokufanyika kwa bishara vizuri na maendeleo ya kiuchumi kuwa ni kikwazo.

“Katika baraza hili tupo wajumbe 12 kutoka sekta za serikali na sekta binafsi, lazima tuwe kitu kimoja katika kuwapatia wananchi maendeleo,”alifahamisha.

Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, aliwataka wafanyabiashara kupatiwa elimu, ambayo itawasaidia kuondokana na kuuza vitu kwa bei ghali na sio kupata faida.

Alisema ataishauri Serikali juu ya kuanzisha vituo vya michezo hapa Zanzibar, ili vijana waweze kujifunza na kupatikana wataalamu wa baadae kupitia michezo.

Naye katibu Tawala Wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, alishuri uwepo wa ushirikishwaji wa wanawake katika baraza hilo, ambao wataweza kuwawakilisha wanawake wenzao kwenye sekta ya biashara.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Baraza la Maji Chake Chake Maulid Mwalimu Ali, alisema wafanyabiashara bado hawajawa tayari kulipa kodi za serikali ikiwemo ukataji wa leseni za biashara, licha ya kukumbushwa kwa barua.

Alisema mji wa chake chake una wanyabishara ya maduka zaidi ya 2000 na tayari wote wametakiwa kukata leseni ya mwaka 2023, lakini hadi sasa waliokata leseni hawazidi 200.

Mjumbe wa baraza hilo Mohamed Abdalla, alisema sekta ya usafiri ndio kila kitu katika kukuza uchumi wa Pemba, hivyo ipo haja ya kupatikana kwa boti za kasi kama ilivyo Unguja Dar.

“Sehemu yoyote yenye mzunguruko mkubwa wa watu basin a shuhuli za kibiashara zitakuwepo, Pemba sasa inapaswa kuwepo na boti za mwendo kasi kama ilivyo Unguja na Dar, boti ambazo zinaweza kwa siku zikafanya safari ya kwenda na kurudi,”alisema.

Hata hivyo aliwataka wajumbe wenzake kushajihisha wawekezaji kuwekeza katika nyumba za kulala wageni ambazo zitakua na bei nafuu kwa wananchi na sio kama ilivyo sasa.

MWISHO