Wednesday, January 15

Wafanyabiashara watakiwa  kufuata sheria na kanuni zilizowekwa ili kuondosha usumbufu usiokua wa lazima.

 

NA HANIFA SALIM, PEMBA

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib amewataka wafanyabiashara   kuhakikisha wanafuata sheria na kanuni zilizowekwa ili kuondosha usumbufu usiokua wa lazima.
Alisema, si kosa kwa mfanyabiashara asiefahamu utaratibu na wajibu wao ni kuwafahamisha hivyo, amewaasa wafanyabiashara kutokutumia silaha za aina yoyote kuwatishia maafisa wanapofika katika maduka yao kwa kisingizio cha kutokufahamu utaratibu.
Mkuu huyo wa Mkoa aliyasema hayo kufuatia tukio lililojitokeza kwa maafisa wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar ZRA wakiwa katika kazi zao za kawaida kukutana na kadhia ya kutolewa maneno ya kashfa pamoja na kutishiwa usalama wao kutoka kwa mfanyabiashara wa Mji wa Konde Wilaya ya Micheweni Mkoani humo.
“Niwaase wafanyabiashara wanapokuja maafisa wetu wa ZRA, TRA, ZBS, ZFDA na tume ya ushindani halali ya kibiashara kwenye maduka yetu tuwape mashirikiano, leo limejitokeza hili hatutarajii ndani ya Mkoa wetu kujitokeza suala jengine kama hili”, alisema.
Aidha aliwataka wafanyabiashara wote endapo kutajitokeza tatizo la aina yoyote kuonana na Afisa wa ZRA ndani ya Mkoa wao, Mkurugenzi au kupiga simu kwa Kamishna mwenyewe kwani alisema serikali haina lengo la kuuwa biashara bali ni kuhakikisha wanaongeza wafanyabiashara ndani ya Mikoa.
Akizungumza kwa lengo la kuomba radhi Mfanyabiashara huyo, Abdalla Haroub Said aliwaasa wafanyabiashara wenziwe kutoa mashirikiano kwa maafisa wa ZRA pale wanapofika katika maduka yao pamoja na kutunza kumbukumbu na maelezo yote watakayoulizwa.
“Nakiri kwamba febuari 21 mwaka huu nilitenda kosa la kuwazuia watendaji wa ZRA wasitekeleze kazi zao pamoja na kuwatishia usalama wao natambua kwamba kitendo hichi nilichokifanya ni kosa naomba radhi kwa ZRA, serikali na umma bali sikudhamiria kufanya hivyo ila nilitawaliwa na hasira”, alisema.
Hata hivyo alisema pamoja na kudai haki zao za kusikilizwa na kupewa elimu ya kodi, aliwasisitiza wafanyabiashara wenzake kutokuwazuia maafisa wa ZRA kutekeleza majukumu yao, kutoa taarifa zote zinazohitajika pamoja na kulipa kodi kwa hiari.
Nae Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar ZRA Yusuph Juma Mwenda alisema, ni kosa kuwazuia watumishi wa serikali kutimiza majukumu yao, kuwatishia usalama wao na ni kosa kuonesha kutowajibika kulipa kodi kwa hiari kwa mujibu wa sheria.
Alieleza kwa mujibu wa sheria ya usimamizi na utaratibu wa kodi namba saba ya mwaka 2009 ni makosa na yakithibitika yanatozwa faini ya shilingi Milioni 10 au kifungo kisichopungua miaka mitano au vyote viwili kwa pamoja.
“Kuanzia mwezi Machi tutatoa mafunzo kwa wafanyabiashara na mimi mwenyewe nitafanya ziara katika maduka yetu kusikiliza changamoto zenu, na kundi ambalo litakuja kuondosha malalamiko ya kulipa kodi ndogo na kubwa yaweze kupatiwa ufumbuzi”, alisema.
Hata hivyo alimpongeza mfanyabiashara huyo kwa kukiri kosa na kusema kwamba ZRA imemsamehe lakini hawatomsamehe mtu mwengine yoyote atakaefanya kosa kama hilo, hivyo alisema mfanyabiashara huyo atalazimika kulipa faini ya shilingi Milioni tano badala ya kukubali kosa.
                                MWISHO.