Wednesday, January 15

Wanahabari Mahiri Wa Habari Za Wanawake Na Uongozi Wapatikana

 Radio jamii na mitandao ya kijamii zang’ara

Mshindi wa kwanza kipengele cha magazeti Hussna Mohamed Khamis akikabidhiwa tuzo na Waziri wa habari Zanzibar Tabia Maulid Mwita.
Amina Massod kutoka Redio jamii mkoani Pemba alieibuka kuwa mshindi wa kipengele cha redio jamii.
Zuhura Juma Saidi kutoka mtandao wa Habari portal alieibuka mshindi wa tuzo ya wanahabari kupitia mtandao wa kijamii akikabidhiwa zawadi na katibu mtendaji wa Tume ya utangazaji Zanzibar Suleiman Abdalla.

Jumla ya waandishi wa habari 10 wameibuka kidedea katika tuzo za umahiri za uandishi wa habari za takwimu za wanawake na uongozi zilizoandaliwa na TAMWA, Zanzibar kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO).

Miongoni mwa vipengele ambavyo vilikuwa vinashindaniwa ni pamoja na mwandishi mahiri katika kipengele cha radio za kitaifa, radio za kijamii, magazeti pamoja na mitandao ya kijamii, ambapo kwa upande wa magazeti kulikuwa na washindi watatu, mitandao ya kijamii watatu, radio za kijamii washindi wawili na washindi wawili kutoka katika radio za kitaifa.

 

Katika washindi hao 10 waliopatikana, jumla ya washindi wane (4) wa kwanza kutoka katika kila kipengele walipatiwa zawadi na cheki ya  milioni moja, tuzo pamoja na vyeti vya ushiriki.

 

Washindi hao wanne kutoka katika kila kipengele ni pamoja na Husna Mohammed Khamis kutoka gazeti la Zanzibar Leo, Rehema Juma Mema kutoka radio Asalaam FM, Zuhura Juma Said wa mtandao ya kijamii wa Habari Portal na Amina Masoud Jabir kutoka radio Jamiii Mkoani kisiwani Pemba, ambapo washindi wa pili nao walijipatia vyeti pamoja na cheki ya shilingi laki tano (5) kwa kila mmoja, ambapo mshindi wa tatu katika kila kipengelke alizawadiwa cheti pamoja na cheki ya shilingi laki nne (4).

 

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajauni, Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt Hussein Ali Mwinyi ambaye aliwakilishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Mheshimiwa Tabia Maulid Mwita alisema kuwa kilio cha wanahabari kuhusu mabadiliko ya sheria ya huduma ya habari kuwa Serikali imewasikia na ipo njiani kuzibadilisha ili muifanye kazi yenu kwa umahiri zaidi na bila ya wasiwasi wowote.

 

“Tunataka kuwa na sheria ambayo imetokana na pande mbili yaani wadau wa habari na Serikali”, amesisitiza Waziri Tabia.

 

“Nimekuwa nikifuatilia vyombo vya habari na kuona kuwa  Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 na marekebisho yake ya mwaka 1997 na  Sheria No.8 ya 1997 na marekebisho yake ya mwaka 2010 zikilalamikiwa zaidi kuwa na mapungufu na zinahitaji kurekebishwa pamoja na  sheria nyingine kadhaa zinazohusiana nazo” alisisitiza.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Mkurugenzi wa TAMWA, Zanzibar Dkt.Mzuri Issa aliiomba Serikali kuhakikisha kwamba ile asilimia 40 ya ushiriki wa wanawake inafikiwa katika kila nyanja ya vyombo vya maamuzi ikiwemo kamati, bodi za utendaji, hivyo hakuna budi kuwa na mazingira mazuri ya kuwewezesha wanawake kushiriki katika uongozi katika ngazi zote.

 

“Tunasisitiza pia kuandaa takwimu za wanawake na Uongozi jambo hilo litasaidia kujua hasa tuko wapi katika malengo hayo ambayo ni ya kimilenia, lengo nambari 5 la milenia (sustainable development goal, SDG), na sisi taasisi zetu tunaahidi kutoa mashirikiano ya kina”. Aliongeza Dkt Mzuri Issa.

 

Tuzo hizi za uandishi wa habari za takwimu kwa wanawake na uongozi ni muhimu sana katika kushajihisha waandishi wa habari wa Zanzibar kuandika zaidi habari na makala kuhusiana na masuala ya wanawake na uongozi, lakini pia kutoa takwimu ya idadi sahihi ya wanawake walioko katika uongozi Zanzibar.

 

TAMWA, Zanzibar imeamua kuchukua juhudi mahasusi za kuandaa tuzo hizo ili jamii itambue mchango wa wanawake na uongozi katika sekta mbalimbali ili kuinua hali za wanawake na kuongeza ushiriki wao  katika masuala ya uongozi ili kufikia 50 kwa 50 katika katika ngazi zote za maamuzi kama inavyoelezwa katika katiba nchi yetu na mikataba na itifaki mbali mbali za kimataifa.

 

TAMWA, Zanzibar inatoa wito kwa waandishi wa habari wa zanzibar kuendelea kuandika habari zinazohusu wanawake, takwimu lakini pia vikwazo mbalimbali vinavyomzuia asifikie nafasi za uongozi na kuwa tayari kushiriki katika tuzo zijazo ambazo zitaandaliwa.

 

Tuzo hizo ambazo ni mara ya pili kutolewa zimeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ), kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) na Ubalozi wa Norway.

 

Jumla ya kazi 421 kutoka vyombo vya habari vya aina zote vikiwemo magazeti, redio, televisheni pamoja mitandao ya kijamii, zilipitiwa katika kutafuta washindi hao katika  tuzo hizo zenye kauli mbiu “KALAMU YANGU MCHANGO WANGU KWA WANAWAKE” hivyo waandaji wa tuzo hizo zinawaomba waandishi wa habari kujitahidi kuandika habari za kina za wanawake na uongozi.

 

Dkt. Mzuri Issa

Mkurugenzi

TAMWA, ZNZ.