Wednesday, October 30

ZAIDI ya Shilingi milioni 180 zimetumika kwa mwaka 2020-2022 katika utekelezaji wa shughuli za miradi ya maendeleo katika Jimbo la Wawi.

NA HANIFA SALIM, PEMBA
ZAIDI ya Shilingi milioni 180 zimetumika kwa mwaka 2020-2022 katika utekelezaji wa shughuli za miradi ya maendeleo katika Jimbo la Wawi ikiwa ni sehemu ya ahadi za Mwakilishi wa jimbo hilo Bakar Hamad Bakar alizozitoa kwa wananchi.
Shughuli hizo za kimaendeleo ambazo zimetekelezwa na Mwakilishi huyo ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, masuala ya kielimu, miondombinu ya barabara, kukuza michezo, upatikanaji wa ajira kwa vijana na uimarishaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Aliyasema hayo katika mkutano wa kujieleza kwa kipindi cha miaka miwili tangu kuingia madarakani namna alivoitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa kutimiza ahadi ambazo alizitoa kwa wananchi wakati akiomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo mwaka 2020.
Mkutano huo ambao uliwashirikisha wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM wadi na jimbo pamoja na wajumbe wa kamati za siasa uliofanyika katika ukumbi wa kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake.
Alisema, utekelezwaji huo wa ahadi na Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika jimbo la Wawi umefanywa kupitia mifuko mbali mbali ukiwemo mfuko wa jimbo na fedha zake mwenyewe.
Nae Mbunge wa Jimbo hilo Khamis Kassim Ali alisema, baada ya kuchaguliwa aliweka vipaumbele vyake vitatu ikiwa ni pamoja na miondombinu ya barabara, elimu na masuala ya michezo kwa vijana.
“Katika kipindi cha miaka miwili nimefanya ukarabati wa barabara yenye urefu wa kilomita moja na nusu inayotoka Kibokoni – Mgogoni, kukarabati skuli ya Furaha msingi na Sekondari, kusajili vilabu vya jimbo letu, kuvipatia jezi pamoja na kukarabati viwanja vya michezo”, alisema.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Chake chake ambae ni Mjumbe wa kamati ya siasa ya Wilaya Abdalla Rashid Ali alisema, kikao hicho kitarahisisha kazi katika uchaguzi unaokuja wa mwaka 2025.
“Tunapofanya vikao hivi itakua ni chachu ya ari na moyo kwa viongozi hao wa jimbo kuweza kutekeleza zile ahadi ambazo waliziweka kwa wananchi pamoja na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ipaswavyo”, alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jimbo la Wawi Suleiman Mussa Khamis alisema, lengo la kikao hicho ni kuwaita Madiwani, Mwakilishi na Mbunge wa jimbo hilo kujieleza ndani ya miaka miwili iliyopita namna walivoitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mbele ya wajumbe hao.
Jimbo la Wawi ni miongoni mwa majimbo tisa yaliyomo katika Mkoa wa Kusini Pemba ambalo limepakana na majimbo manne, upande wa kaskazini limepakana na jimbo la Ziwani, Kusini jimbo la Chonga, Mashariki jimbo la Chake chake na Ole upande wa Magharibi.
                                           MWISHO.