Na John Mapepele
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaagiza Watendaji Wakuu wa Taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake zinazojishughulisha na uhifadhi wa raslimali kushirikiana na wananchi walio karibu na maeneo wanayoyahifadhi ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima.
Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Machi 7, 2023 alipokaribishwa kujibu hoja za wananchi na Waziri Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa kwenye hafla ya kukabidhi program ya kuhama kwa hiari kwa wananchi kutoka kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kupisha uhifadhi na kuja Msomela kwenye Halmashauri za Handeni na Kilindi, ambapo Mhe Waziri Mkuu amekuwa Mgeni Rasmi.
Aidha, Mheshimiwa Mchengerwa amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa kama kumekuwa na kero yoyote baina ya wananchi na taasisi zilizo chini ya Wizara yake zinakwenda kumalizika kabisa katika kipindi hiki.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kipindi changu naomba nikuhakikishie hakuna kero itakayotushinda kwa kuwa tumekubaliana kufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi kwa kuzingatia msingi wa kuwa wananchi ndiyo wenye raslimali hizo.” Amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Kuhusu suala la wananchi kuvamia maeneo ya yaliyohifadhiwa kisheria Mhe. Mchengerwa amesema Wizara itaendelea kusimamia maeneo hayo kulingana na sheria ambapo amesema kuwa tayari Kamati ya Mawaziri 8 iliyoteuliwa na Mhe. Rais ambayo ilizunguka nchi nzima kutatua migogoro ilishatoa suluhisho la migogoro hiyo na Wizara itaendelea kuzingatia hayo.
Amezishukuru taasisi
hizo kwa kuanza kufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi wanaozunguka maeneo hayo na amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kwenda kuingia kwenye mioyo ya watanzania ili waweze kutambua kuwa raslimali hizo ni mali yao na kwamba zinatakiwa kuhifadhiwa kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Aidha, amesema kazi ya uhifadhi itakwenda kutekelezwa kirahisi kwa kuwa mfumo wa uongozi wa taasisi hizo ni wa kijeshi kwa hiyo wanapopelekewa maelekezo kutoka kwa viongozi wakuu yatatekelezwa kwa shemina za kijeshi.
Pia amemhakikishia Mhe. Waziri Mkuu kwamba kwa upande Wizara yake kuhusu ushiriki wake katika utekelezaji wa agizo la awamu ya pili la kuhama kwa hiari kwa wananchi tayari imejipanga na kwamba itatekeleza jukumu lake kwa wakati.
Katika hafla hiyo Mhe. Waziri Mkuu aliambatana na Mawaziri na manaibu wa Wizara tisa na makatibu wakuu wao ambapo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii Katibu Mkuu Dkt Hassan Abbasi na Naibu wake Anderson Mutatembwa pia walishiriki.