Friday, January 31

Kamati ya skuli ya sekondari furaha yatakiwa kushirikiana na walimu kuondosha changamoto ya utoro wa wanafunzi katika skuli hiyo.

NA HANIFA SALIM, PEMBA.

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud ameitaka kamati ya skuli ya sekondari furaha kushirikiana na walimu ili kuhakikisha wanaondosha changamoto ya utoro wa wanafunzi katika skuli hiyo.
Alisema, kuna baadhi ya wazazi wanadhani jukumu la kumsimamia mtoto kusoma ni la walimu pekee jambo ambalo linasababisha kwa kiasi kikubwa utoro pamoja na matokeo mabaya katika mitihani yao ya taifa.
Akizungumza kwa niaba Mkuu wa Mkoa huyo Katibu Tawala Mkoa wa Kusini Pemba Suleiman Hamad aliyasema hayo, katika sherehe ya mahafali na kuwakabidhi zawadi wanafunzi waliofaulu vizuri kidato cha nne, darasa la saba na la nne iliyofanyika skuli ya Furaha Chake chake.
“Wanafunzi 11 ambao wamefaulu si kidogo lakini pia sio wengi, ni imani yangu mwaka huu 2023 idadi ya ufaulu itaongezeka zaidi, nawapongeza walimu kwa kazi kubwa ambazo wamezifanya za kuhakikisha watoto wanafaulu”, alisema.
Aidha aliwataka, wanafunzi wasome kwa bidii ili waweze kupata mikopo ya elimu ya juu ambayo itawawesha kupata fursa ya kujiendeleza na elimu ya chuo kikuu.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Wawi Bakar Hamad Bakar aliwaahidi wanafunzi kuendelea kufanya shughuli za kuwazawadia zawadi wanafunzi ambao wamefanya vizuri katika mitihani yao.
“Hatutaki tena zero katika skuli yetu ya furaha walimu tushirikiane mwaka 2023 hakuna mwanafunzi atakaepata zero jambo hili linawezekana kwani skuli nyengine imewezekana na sisi hatutoshindwa”, alisema.
Nae Afisa elimu Mkoa wa Kusini Pemba Mohamed Shamte aliwapongeza walimu wa skuli ya furaha kwa kupiga hatua kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuhakikisha wamefanikiwa kufuta alama zero.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Chake chake Ali Mohamed Chande aliwataka wanafunzi wasome kwa bidii huku wakiachana na mambo mengine yasiokua na umuhimu kwao.
Akisoma risala ya sherehe hiyo mwalimu Mwanajuma Nahoda Ali alisema, wanakabiliwa na changamoto mbali mbali katika skuli yao ikiwemo, ukosefu wa skuli ya sekondari ambayo hulazimika wanafunzi kusoma katika madarasa ya msingi, vyoo, maji safi na salama, vitendea kazi, uhaba wa walimu wa kingereza, hesabati na Geography.
                          MWISHO.